Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maelezo ya jumla
Mtindio wa ubongo (cerebral palsy),ni hali inayosababishwa na matatizo ya ubongo inayopelekea kuvurugika kwa shughuli za mfumo wa neva kama vile kujongea, kujifunza, kusikia, kuona na kufikiri.
Neno utindio wa ubongo linatumika kuwakilisha matatizo yote ya mfumo wa neva yanayotokea utotoni na yanayothiri mjongeo na misuli ya mtoto. Hali ya mtoto mwenye tatizo hili haibadiliki. Japo mtindio wa ubongo huathiri zaidi misuli, hausababishwi na matatizo kwenye misuli au neva. Mtindio wa ubongo husababishwa na matatizo kwenye maeneo ya ubongo yanayodhibiti mjongeo.
Kuna aina mbalimbali za tatizo hili, aina hizi ni pamoja na mtindio wa ubongo unaosababisha kukaza kwa misuli, mtindio wa ubongo unaosababisha kulegea kwa misuli, n.k
Je, nini dalili za mtindio wa ubongo?
Dalili hutofautiana sana kati ya watu wenye mtindio wa ubongo. Dalili zinaweza:
- Kuwa za kadiri sana au kali sana
- Kuhusisha upande mmoja wa mwili au pande zote mbili
- Kuwa kwenye mikono au miguu, au mikono na miguu kwa pamoja
Dalili za mtindio wa ubongo unaosababisha kukaza kwa misuli, hii ndiyo aina inayowapata watu weng, ni pamoja na:
- Misuli inakaza na inakuwa ngumu kuinyoosha. Misuli inaweza kuendelea kukaza zaidi kadri muda unavyokwenda.
- Kutembea kusiko kwa kawaida: Kutembea akiwa ameweka mikono sawa, magoti yanaweza kuwa yanavukana au yanagusana, miguu huwa kama “mkasi” wakati wa kutembea au kutembelea vidole vya miguu.
- Viungo vinakuwa vigumu na visivyofunguka mpaka mwisho
- Misuli inaweza kuwa dhaifu au na hata baadhi kupooza kabisa.
- Dalili zinaweza kuathiri mkono mmoja au mguu, upande mmoja wa mwili, miguu yote, au mikono na miguu kwa pamoja
Aina nyingine za mtindio wa ubongo zinaweza kuwa:
- Mjongeo usiokuwa wa kawaida (kusongoa, mkutuo, au mfurukuto) wa viganja, mikono au miguu wakati akiwa macho na kuzidi zaidi wakati wa msongo
- Kutetemeka
- Kutembea akiwa anayumbayumba
- Kupungua kwa uratibu wa mwili
- Misuli iliyolegea, hasa wakati wa mapumziko, na viungo visivyotulia
Dalili nyingine za ubongo na mfumo wa neva ni pamoja na:
- Kupungua kwa uwezo wa kujifunza na kufikiri, lakini wakati mwingine uwezo wa kufikiri unaweza kuwa sawa.
- Matatizo ya kuongea
- Matatizo ya kusikia au kuongea
- Degedege
- Maumivu, hasa kwa watu wazima (inaweza kuwa vigumu kuyadhibiti)
- Matatizo wakati wa kula na matatizo ya mfumo wa chakula
- Kushindwa kunyonya au kula kwa watoto wachanga, au kushindwa kutafuna na kumeza kwa watoto wakubwa na watu wazima
- Matatizo ya kumeza chakula (kwa rika zote)
- Kutapika na kufunga choo
Dalili nyingine:
- Kutokwa na mate
- Kukua taratibu kuliko ilivyo kawaida
- Kupumua kusiko kwa kawaida
- Kujikojolea
Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata mtindio wa ubongo?
Kwa baadhi ya watu wenye mtindio wa ubongo, sehemu fulani za ubongo huharibika kwa sababu ya kukosa oksijeni. Haijulikani kwa nini hili hutokea. Watoto njiti wako kwenye hatari zaidi ya kupata mtindio wa ubongo. Mtindio wa ubongo unaweza pia kutokea utotoni kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na:
- Kuvuja damu ndani ya ubongo
- Majeraha ya kichwa
- Maambukizi kwenye ubongo (kuvimba ubongo, kuvimba kwa utando unaofunika uti wa mgongo na ubongo, maambukizi ya herpes)
- Maambukizi kwa mama wakati wa ujauzito (rubella)
- Manjano kali sana
Kwa hali nyingine, sababu ya kutokea kwa ugonjwa huu wa mtindio wa ubongo haijulikani kabisa.
Wakati gani utafute matibabu ya haraka?
Mwone mtoa huduma ya afya kama una dalili za mtindio wa ubongo, hasa kama unajua ulipata majeraha wakati wa kuzaliwa au utotoni.
Utambuzi wa mtindio wa ubongo
Uchunguzi wa neurolojia ni muhimu. Kwa wazee, kupima uwezo wa kujitambua ni muhimu. Vipimo vifuatavyo vinaweza kufanyika pia:
- Vipimo vya damu
- CT Scan ya kichwa
- Electroencephalogram (EEG)
- MRI ya kichwa
- Vipimo vya macho
Uchaguzi wa matibabu ya mtindio wa ubongo
- Mtindio wa ubongo hauwezi kuponywa, lakini matibabu mara nyingi huboresha uwezo wa mtoto. Watoto wengi wanaweza kuishi maisha angalau kama kawaida wanapokuwa watu wazima kama watapata matibabu sahihi. Kwa kawaida, kadiri matibabu yanavyowahi kutolewa ndivyo na matokeo huboreka.
- Matibabu yanaweza kujumuisha mazoezi, kujifunza kazi, kujifunza kuongea, madawa kudhibiti degedege, madawa kulegeza misuli iliyokakamaa, madawa ya maumivu, upasuaji kuondoa kasoro zilizopo, viatu maalumu, kiti cha magurudumu na vifaa vya mawasiliano kama kompyuta n.k.
- Lengo la matibabu ni kumsaidia mtu kujitegemea kwa kadri inavyowezekana. Matibabu huhitaji ushirikiano wa wataalamu wa fani mbalimbali, hii ni pamoja na: Madaktari wa kawaida, madaktari wa meno (wanapaswa kuangaliwa meno kila baada ya miezi 6), watu wa utawi wa jamii, wauguzi, wataalamu wa kufundisha kazi, wataalamu wa mazoezi, wataalamu wa kufundisha kuongea, madaktari bingwa wa mfumo wa neva, madaktari bingwa wa mapafu na mfumo wa upumuaji, madaktari bingwa wa mfumo wa kumeng’enya chakula, madaktari wa ukarabati.
Kujitunza mwenyewe nyumbani
- Kupata chakula cha kutosha na lishe bora
- Kuweka mazingira ya nyumba salama
- Kufanya mazoezi yaliyopendekezwa na watoa huduma za afya
- Kulinda viungo vyako visiumie
- Inashauriwa kumweka mtoto asome katika shule ya kawaida, isipokuwa pale tu ulemavu wa kimwili au maendeleo ya kiakili yatakapofanya isiwezekane. Kumpeleka katika shule maalumu kunaweza kusaidia.
Mawasiliano na huduma ya kujifunza
- Miwani
- Vifaa vya kumsaidia kusikia
- Vifaa vya kuitegemeza misuli na mifupa-braces
- Vifaa vya kumsaidia kutembea
- Viti vya magurudumu
- Mazoezi ya kimwili, kujifunza kufanya kazi, msaada kutoka kwa mtaalamu wa mifupa au matibabu mengine yanaweza pia kuhitajika ili kusaidia shughuli za kila siku na huduma.
Madawa
- Madawa ya kudhibiti degedege hupunguza uwezekano wa kupata degedege
- Sumu ya botulinum husaidia kulainisha misuli iliyokakamaa na kupunguza kutokwa mate.
- Madawa ya kulegeza misuli kama baclofen husaidia kupunguza kutetemeka na kukaza kwa misuli.
Upasuaji
- Kudhibiti kubweua –gastoesophageal reflux
- Kukata baadhi ya mishipa ya fahamu ili kupunguza maumivu na kulegeza misuli.
- Ili kuweka mirija ya kusaidia kumpa mgonjwa chakula
- Ili kufungua viungo vilivokazwa na misuli –contractures
Nini cha kutarajia mwanao akiwa na mtindio wa ubongo ?
- Mtindio wa ubongo sio kwamba mara zote unasababisha ulemavu mkubwa. Hata hivo, husababisha matatizo yanayodumu maisha yote ya mgonjwa. Uangalizi wa muda mrefu unaweza kuhitajika. Kiwango cha ulemavu hutofautiana kati ya mtu na mtu.
- Mtoto mmoja aliye na mtindio wa ubongo anaweza kushindwa kutembea na akahitaji uangalizi wa kina maisha yake yote. Mtoto mwingine mwenye mtindio wa ubongo wa kadiri anaweza kuonekana wa ajabu kidogo na asihitaji msaada wowote maalumu.
- Watu wengi wazima wanaweza kuishi katika jamii, ama kwa kujitegemea au kwa usaidizi. Kama hali ni mbaya zaidi, mgonjwa anaweza kuwekwa katika taasisi maalumu zinazoshughulika na matatizo haya. Matibabu, madawa na upasuaji vinaweza kumsaidia mgonjwa kuboresha ujuzi na uwezo wa kuwasiliana na ulimwengu.
Matatizo yanayoweza kutokea
- Kudhoofu kwa mifupa
- Kuziba kwa utumbo
- Kuteguka kwa mfupa wa nyonga na maambuikizi kwenye viungo vilivyo kwenye nyonga
- Majeraha yanayotokana na kuanguka
- Kukaza kwa viungo
- Nyumonia inayosababishwa na kupaliwa
- Lishe duni
- Kupungua kwa uwezo wa mawasiliano (wakati mwingine)
- Kupungua kwa uwezo wa kufikiri (wakati mwingine)
- Kupinda mgongo
- Degedege
- Unyanyapaa wa kijamii
Leave feedback about this