MTOTO NJITI

MTOTO NJITI

 • January 19, 2021
 • 0 Likes
 • 27 Views
 • 0 Comments

Maelezo ya jumla

Mtoto njiti (premature infant) ni mtoto anayezaliwa kabla ya wiki 37 za ujauzito.

Je! Nini dalili za kujifungua mtoto njiti?

 • Viungo vya watoto njiti havijakomaa vizuri. Mtoto huyu anahitaji uangalizi maalumu katika mazingira maalumu mpaka viungo vyako vitakapokomaa na kuweza kuendeleza maisha bila msaada wa mashine. Uangalizi huu unaweza kuchukua wiki kadhaa mpaka mwezi.
 • Katoto kabichi/ mtoto njiti atakuwa na uzito mdogo kuliko mtoto wa kawaida. Sifa za mtoto njiti ni pamoja na:
  • Kuwa na nywele mwilini (lanugo)
  • Kupumua kusiko kwa kawaida (kupumua kwa kutumia nguvu nyingi, kusita au kuacha kupumua kwa muda-apnea)
  • Kama ni mtoto wa kike anakuwa na kinembe au kisimi kikubwa kuliko kawaida
  • Mtoto hupata shida kupumua kwa sababu mapafu hayajakomaa au anaweza kupata nyumonia
  • Misuli iliyolegea, kuzubaa au kuwa tepetepe tofauti na mtoto aliyefikisha umri wa kuzaliwa
  • Matatizo ya kula kama vile kushindwa kunyonya au kumeza au kupumua.
  • Huwa na mafuta kidogo mwilini- mafuta mwilini husaidia kuutia mwili joto
  • Mtoto wa kiume huwa na pumbu ndogo, pumbu zake zinakuwa hazina mikunjo mikunjo kama pumbu za watoto wa kawaida, korodani zake huwa hazijashuka pia.
  • Sikio laini na linalokunjika kirahisi sana
  • Ngozi nyembamba, nyepesi na wazi-unaweza kuona mishipa ya damu chini ya ngozi.
  • Hata hivyo, sio watoto wote njiti wana dalili hizi.

Ni nini husababisha mtoto kuzaliwa njiti?

 • Wakati wa kuzaliwa, mtoto huwekwa katika mojawapo ya makundi yafuatayo:
  • Mtoto njiti (huzaliwa chini ya wiki 37 za ujauzito)
  • Mtoto aliyefikisha muda wake wa kuzaliwa (huzaliwa ndani ya wiki 37 mpaka 42)
  • Mtoto aliyepitisha muda wa kuzaliwa (huzaliwa baada ya wiki 42 za ujauzito)
  • Kama mwanamke akipata uchungu wa kujifungua kabla ya wiki 37 huwa amewahi hii huitwa premature labor
  • Mara nyingi sababu za kuwahi kwa leba hazijulikani, lakini 15% ya wanawake mwenye ujauzito wa mapacha, watoto watatu au zaidi hupata watoto njiti.
  • Matatizo ya kiafya ya mama na matukio kadhaa yanaweza kuchangia mtoto kuzaliwa njiti:
  • Ugonjwa wa sukari
  • Ugonjwa wa moyo
  • Maambukizi (kama maambukizi kwenye njia ya mkojo au maambukizi ya chupa (membrane) inayozunguka na kutengeneza majimaji yanayomzunguka mtoto)
  • Ugonjwa wa figo

Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata mtoto njiti?

 • Shida tofauti tofauti zinaweza kuongeza uwezekano wa kupata mtoto njiti
 • Kama mlango wako wa kizazi umelegea unaweza kuleta shida hii
 • Matatizo au kasoro kwenye uterasi/ mji wa mimba
 • Historia ya kupata mtoto njiti
 • Mlo usio mzuri kabla au wakati wa ujauzito
 • Viashiria vya kifafa cha mimba kama vile shinikizo la juu la damu na protini kwenye mkojo kabla ya wiki 20 za ujauzito
 • Kupasuka chupa mapema kuliko ilivyo kawaida
 • Sababu nyingine zinazoweza kuongeza uwezekano wa kupata mtoto njiti ni pamoja na:
  • Asili, watu weusi wana uwezekano mkubwa zaidi- hili halihusiani na hali ya kiuchumu ya mwanamke
  • Umri, kuwa na umri chini ya miaka 16 au zaidi ya miaka 35
  • Ukosefu wa huduma nzuri wakati wa ujauzito
  • Hali ya kiuchumi ya mwanamke
  • Matumizi ya tumbaku, kokaini au amphetamines

Wakati gani utafute matibabu haraka?

 • Nenda kituo cha afya kilicho karibu yako kama unahisi unapata leba mapema kuliko ilivyotarajiwa
 • Kama wewe ni mjamzito na haupokei matunzo na huduma unazotakiwa kupata wakati wa ujauzito, mwone mtoa huduma za afya. Nchi yetu ina program maalumu za huduma kwa wajawazito.

Utambuzi

 • Mtoto anaweza kupata shida ya kupumua n ahata kushindwa kudhibiti joto la mwili.
 • Baadhi ya vipimo vinavyofanyika kwa mtoto njiti ni pamoja na:
  • Vipimo vya kuangalia kiwango cha gesi kwenye damu
  • Vipimo kuangalia kiwango cha sukari, kalsiamu na bilirubin kwenye damu
  • Eksirei ya kifua
  • Kufuatilia upumuaji na mapigo ya moyo ya mtoto

Uchaguzi wa matibabu

 • Kama utapata leba mapema kabla ya wakati wake na haiwezi kuzuilika, watumishi wa afya watajiandaa kwa ajili ya uzazi ulio mgumu. Unaweza kuhamishwa hospitali na kupelekwa kwenye kituo chenye vifaa maalumu vya kuwalea na kuwasaidia watoto njiti (Kitengo cha utunzanji watoto mahututi –NICU)
 • Baada ya kuzaliwa mtoto atalazwa ili kunagaliwa kwa ukaribu. Atawekwa chini ya warmer au ndani incubator ili kumpatia joto. Vifaa mbali mbali vitafuatilia mapigo yake ya moyo, upumuaji wake na kiwango cha oksijeni kwenye damu.
 • Watoto hawa mara nyingi wanashindwa kunyonya na kumeza, hasa wakizaliwa kabla ya wiki 34 za ujauzito. Kwa hiyo, mtoto atawekewa mpira mdogo kupitia puani au mdomoni mpaka tumboni kwa ajili ya kumlishia. Kwa watoto wengine ambao wanaumwa sana, wanaweza kupewa chakula kupitia mishipa yao mpaka watakapo kuwa tayari kulishwa chakula.
 • Kama mtoto ana matatizo ya kupumua:
  • Bomba ndogo inaweza kuwekwa ndani ya koo. Machine inayoitwa Ventilator itamsaidia mtoto kupumua.
  • Baadhi ya watoto ambao matatizo yao sio makubwa sana, wanaweza kupokea hewa kupitia kwenye bomba ndogo iliyowekwa puani badala ya kooni-Continous positive airway pressure (CPAP)- au wanaweza kupewa oksijeni ya ziada pekee.
  • Oksijeni ya ziada inaweza kutolewa kwa mashine ya ventilator, CPAP, nasal prongs au oxygen hood.
  • Matunzo maalumu yataendelea mpaka mtoto atakapoweza kupumua, kula na kuweza kudhibiti joto lake la mwili mwenyewe bila kuhitaji msaada na kuanza kuongezeka uzito. Kwa watoto wadogo sana, matatizo mengine yanaweza kutokea na wakakaa kwa muda mrefu zaidi hospitalini.

Nini cha kutarajia?

Kuzaliwa njiti ilikuwa chanzo kikubwa sana cha vifo vya watoto. Maendeleo ya kitabibu na mbinu za uuguzi zimeongeza ufanisi na uwezekano mkubwa wa kuishi. Kadri umri wa mimba unavyoongezeka ndivyo na uwezekano wa mtoto kuishi unavyoongezeka.

Kuzaliwa njiti kunaweza kusababisha matatizo ya kudumu. Watoto njiti wengi, huwa na matatizo ya kitabibu, matatizo ya ukuaji au matatizo ya kitabia yanayoendelea mpaka utotoni au mpaka utu uzima. Mtoto anapozaliwa katika umri mdogo zaidi au uzito mdogo zaidi,  ndivyo na uwezekano wa kupata matatizo unavyoongezeka. Hata hivyo, ni ngumu sana kutabiri matokeo ya baadae ya mtoto kwa umri wa mimba wakati kuzaliwa pekee.

Matatizo yanayoweza kutokea

 • Matatizo yanayoweza kutokea wakati mtoto akiwa hospitali ni pamoja na:
  • Upungufu wa damu
  • Kuvuja damu ndani ya ubongo au kuharibika kwa sehemu ya ubongo
  • Maambukizi
  • Kupungua kwa kiwango cha sukari kwenye damu
  • Matatizo ya upumuaji
  • Manjano
  • Matatizo ya moyo
  • Matatizo ya tumbo
 • Matatizo yanayoweza kudumu kwa muda mrefu ni pamoja na:
  • Bronchopulmonary dysplasia
  • Mtoto hudumaa na kuchelewa kukua
  • Matatizo ya macho au upofu

Kuzuia kupata mtoto njiti

 • Kuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito hupunguza uwezekano wa kuzaa mtoto njiti. Takwimu zinaonesha wazi kuwa, kuhudhuria kliniki na kufuata malekezo ya watumishi wa afya hupunguza uwezekano wa kujifungua kabla ya muda.
 • Madaktari wanaweza kuzuia au kuchelewesha mtoto kuzaliwa kwa kutumia dawa zinazopunguza mkandamizo wa uterasi. Lakini mara nyingi, jitihada hizi hazizai matunda.
 • Bethamethasone ni dawa anayopatiwa mama mjamzito ili kupunguza matatizo ya mtoto atakapozaliwa. Dawa hii huharakisha ukuaji wa mapafu kabla mtoto hajazaliwa.

Vyanzo

http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/ency/article/001562.htm

 • Share:

Leave Your Comment