MJAMZITO au ANAYENYONYESHA: Lishe/Mlo/Chakula kinachofaa

Umuhimu wa lishe kwa wajawazito na wanaonyonyesha

Lishe ya wanawake wakati wa ujauzito na kunyonyesha ni muhimu kwa afya ya mama, mtoto aliye tumboni na hata afya ya mtoto mchanga baada ya kuzaliwa. Lishe katika Siku 1,000 za maisha ya mtoto (tangu kutungwa kwa mimba hadi mtoto anapofikia umri wa miezi 24) hutoa taswira ya ukuaji na maendeleo yake katika maisha yake yote.

Lishe duni wakati wa ujauzito huweza kusababisha athari mbalimbali kwa mama na mtoto aliye tumboni:

 • Kuzaa mtoto mwenye uzito pungufu yaani chini ya kilo 2.5
 • Kuzaa mtoto kabla ya wakati
 • Kupata matatizo wakati wa kujifungua kama vile kushindwa kujifungua
 • Kuzaa mtoto mwenye ulemavu wa ubongo au mwenye ulemavu wa viungo

Lishe

Ongezeko la uzito wakati wa ujauzito

Kuongezeka uzito wakati wa ujauzito ni muhimu sana kwani ni kiashiria cha lishe nzuri. Mama anatakiwa kuongezeka wastani wa kilo 12 kwa kipindi chote cha ujauzito. Sehemu ya akiba ya mafuta yatatumika kwa ajili ya unyonyeshaji katika miezi michache ya mwanzo.

Ni muhimu kuzingatia kwamba wanawake walio na uzito uliozidi au viribatumbo kabla ya kupata ujauzito hawatakiwi kuongezeka uzito kiwango sawa na wanawake waliokuwa na uzito wa kawaida kabla ya kupata ujauzito.

Mwanamke mjamzito anapaswa kuongezeka kilo 1–2 kila mwezi kuanzia mwezi wa 4 hadi mwezi wa 9 wa ujauzito. Ongezeko katika uzito litamsaidia kuwa na akiba ya mafuta. Sehemu ya akiba ya mafuta itatumika kwa ajili ya kutengeneza maziwa katika miezi sita ya mwanzo baada ya kujifungua. Mjamzito anahitaji kupumzika zaidi ili kuboresha hali yake ya lishe na kuongeza uzito wa mtoto.

Mjamzito pia anahitaji virutubishi kwa wingi hasa aina ya vitamini na madini ili kumkinga asipate maradhi na kumkinga na vifo ambavyo huweza kujitokeza wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na wakati wa kunyonyesha.

Nishati lishe na virutubishi vinavyoshauriwa

Wanawake wanashauriwa kula chakula mchanganyiko na cha kutosha kutoka katika makundi yote ya chakula wakati wa ujauzito na kunyonyesha ili kupunguza athari za kuzaa mtoto mwenye uzito pungufu na matatizo mengine. Wanawake wanaonyonyesha ni muhimu waongeze ulaji wa vyakula vyenye nishati lishe na utomwili kwa wingi zaidi kuliko kiwango kinachoshauriwa kwa wajawazito. Hii ni muhimu kwa sababu mama anayenyonyesha anahitaji nishati lishe ya ziada kwa aili ya kutengeneza maziwa. Mahitaji ya nishati lishe na virutubishi vingine wakati wa ujauzito huongezeka kwa ajili ya:

 • Kukidhi ongezeko la mahitaji ya mwili wa mama kama vile kuongezeka uzito, kuupa nguvu mwili wakati wa ujauzito na kuweka hifadhi ya nishati lishe ya kutosha itakayotumika wakati wa kunyonyesha
 • Ukuaji wa mtoto aliye tumboni, kondo la nyuma la uzazi na tishu za mfuko wa uzazi
 • Mabadiliko ya utendaji kazi wa moyo na mfumo wa hewa kwa mama
 • Kuweka uwiano sahihi wa uzito wa mama na kuupa nguvu mwili wakati wote wa ujauzito

Athari za uzito uliozidi wakati wa ujauzito

Endapo mama atakuwa na uzito uliozidi au kiribatumbo kabla ya ujauzito, au ameongezeka uzito zaidi ya kiwango kinachoshauriwa wakati wa ujauzito anaweza kupata madhara kama vile:

Mwongozo kwa Wanawake Wajawazito na Wanaonyonyesha

Mahitaji ya nishati lishe, protini na mafuta kwa wanawake wajawazito ni makubwa zaidi ukilinganisha na wale ambao hawajapata ujauzito. Hii husaidia kupunguza uwezekano wa kuzaa watoto wenye uzito pungufu.

Pia wanawake wanaonyonyesha ulaji wa vyakula vyenye nishati lishe lazima uongezeke hata zaidi ya mwanamke mjamzito. Hii ni muhimu kwa sababu wanawake wanaonyonyesha huhitaji nishati zaidi ili kutengeneza maziwa.

Mahitaji yao yanaweza kutoshelezwa kwa kufanya yafuatayo:

 • Wanahitaji kula chakula kingi katika kila mlo au kula milo midogo midogo mara kwa mara;
 • Kula asusa kati ya mlo na mlo;
 • Kula matunda na mboga mboga kwa wingi katika kila mlo;
 • Kunywa maji ya kutosha kila siku (glasi 8 au lita 1.5); na
 • Kuepuka kunywa chai au kahawa pamoja na mlo kwani huzuia ufyonzwaji wa madini ya chuma na huweza kusababisha upungufu wa damu. Ni vyema kunywa chai au kahawa saa moja kabla au baada ya kula.

Mimba

Matumizi ya vitamini na madini ya nyongeza

Shirika la Afya Duniani linapendekeza matumizi ya vitamini na madini ya nyongeza hasa madini chuma na aside ya foliki ili kuzuia upungufu wa wekundu wa damu kwa wanawake wajawazito na wanao nyonyesha, kuzuia kujifungua watoto wenye uzito pungufu, njiti pamoja na kujifungua watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.

Mwanamke mjamzito mwenye upungufu wa damu anapaswa apewe rufaa ya kwenda katika kituo cha kutolea huduma za afya kupata ushauri ikiwa ni pamoja na kupewa vidonge vya kuongeza damu na tiba ya malaria na minyoo.

Wanawake wajawazito wanapaswa kuhudhuria kliniki mara nne. Hudhurio la kwanza linatakiwa kufanyika katika miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito. Hudhurio la pili linatakiwa kufanyika wiki ya 24 hadi 26. Hudhurio la tatu ni lazima lifanyike wiki ya 32

Hudhurio la nne ni vema likafanyika siku chache kabla ya tarehe ya matarajio ya kujifungua. Wajawazito wenye matatizo ya upungufu wa damu, kisukari, maambukizi ya VVU au kifua kikuu na matatizo mengine kama yalivyoanishwa kwenye miongozo wanatakiwa kuhudhuria kliniki zaidi ya mara nne.

Vyanzo

https://www.tfnc.go.tz/publications/9

Comments
 • Mimi mke wangu toka amepata ujauzito ni mtu wa kutapika tu mara kwa mara
  Je tufanyeje na Hana ugonjwa wowote

  • Pole sana, kutapika wakati wa ujauzito ni jambo la kawaida. lakini kama mama anatapika sana mpaka anaishiwa nguvu, hapo kunakuwa na tatizo. anaweza kuhitaji kupewa dawa za kuzuia kutapika na kama inahitajika kuongezewa maji kwenye mishipa.

   kama unaona tatizo hili linamsumbua sana, ni vyema akaongea na daktari ili apate dawa.

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi