Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maelezo ya jumla
Ngiri (hernia) ni hali inayotokea kama kuna uwazi au udhaifu kwenye ukuta wa tumbo na kusababisha viungo vya ndani ya tumbo kuchoropoka na kutokeza nje ya ukuta wa tumbo. Ukuta wa tumbo umeundwa na safu imara ya fascia inayoizunguka misuli ya tumbo, na kazi yake kubwa ni kulinda na kuzuia vinavyopaswa kuwa ndani ya tumbo vibaki ndani.
Kuna aina kadhaa za ngiri, aina hizi hutokea sehemu mbalimbali:
- Ngirii inayotokea sehemu ya juu ya paja (femoral hernia)- hii huwapata zaidi wanawake kuliko wanaume,na huonekana kama uvimbe au mwinuko sehemu ya juu ya paja.
- Ngirii inayotokea tumboni (hiatal hernia) – hii hutokea sehemu ya juu ya tumbo.
- Ngirii inayotokea kwenye mkato wa upasuaji (incisional hernia) – hii hutokea kupitia kwenye kovu la upasuaji wa tumbo uliofanyika zamani.
- Ngirii inayotokea kwenye kinena (inguinal hernia) – hii huonekana kama uvimbe kwenye kinena. Aina hii huwapata zaidi wanaume kuliko wanawake. Uvimbe unaweza kwenda mpaka kwenye pumbu.
- Ngirii inayotokea kwenye kitovu (umblical hernia)- uvimbe huonekana kwenye kitovu. Aina hii hutokea kwa sababu ya udhaifu wa kuta za tumbo, uliosababishwa na misuli ya tumbo kwenye eneo la kitovu kushindwa kufunga vizuri.
Je! Nini dalili za ngiri?
Mara nyingi hakuna dalili. Hata hivyo, wakati mwingine mgonjwa anaweza kujisikia vibaya au kuhisi maumivu. Mgonjwa hujihisi vibaya zaidi akijinyoosha, akijikamua, au akiinua vitu vizito.
Japo mara nyingi ngiri haisababishi usumbufu mkubwa, inaweza kukua mpaka kukandamizwa na upenyo ilikopitia, hii huzuia damu kufika kwenye tishu. Mgonjwa huhitaji upasuaji wa dharura ili kurejesha mtiririko wa damu.
Ngiri husababishwa na nini?
Kwa kawaida, huwa hakuna sababu ya dhahiri ya kutokea kwa ngirii. Wakati mwingine ngiri hutokana na kuinua vitu vizito. Mtu anaweza kuzaliwa na ngirii, lakini uvimbe ukaanza kuonekana baada ya miaka mingi. Baadhi ya wagonjwa huwa na historia ya ngirii kwenye familia.
Watoto wachanga na watoto wadogo huzaliwa na ngirii. Hii hutokea kwa sababu ukuta unaofunika viungo vya tumbo hushindwa kufunga vizuri kabla ya kuzaliwa. Karibu watoto 5 kati ya 100 wana ngirii inayotokea kwenye kinena (wavulana zaidi kuliko wasichana). Watoto wengine wanaweza wasipate dalili yoyote mpaka utu uzima.
Shughuli yoyote au tatizo lolote linaloongeza shinikizo kwenye tishu za ukuta wa tumbo na misuli linaweza kusababisha kutokea kwa ngirii, hii ni pamoja na:
- Kufunga choo kwa muda mrefu husababisha mgonjwa kujikamua sana ili kupata kinyesi.
- Kikohozi sugu.
- Kuongezeka kwa ukubwa wa tezi dume husababisha mtu kujikamua sana ili kukojoa
- Unene au uzito mkubwa.
- Kuinua vitu vizito.
- Lishe duni.
- Uvutaji wa sigara.
- Korodani ambazo hazijashuka toka tumboni kwenda kenye pumbu
Wakati gani utafute matibabu ya ngiri haraka?
Mwone daktari mara moja kama:
- Una ngirii inayouma na vilivyomo kwenye uvimbe haviwezi kusukumwa na kurudishwa polepole tumboni kwa kidole
- Una kichefuchefu, unatapika, au homa pamoja na ngirii inayouma.
- Una ngirii ambayo imekuwa nyekundu, zambarau, nyeusi, au yenye rangi isiyoelezeka.
- Una maumivu kwenye kinena na uvimbe.
- Una uvimbe kwenye kinena au kitovu, au kwenye eneo ulilofanyiwa upasuaji.
Utambuzi
Daktari anaweza kuthibitisha uwepo wa ngiri wakati wa uchunguzi wa mwili. Uvimbe unaweza kuongezeka mgonjwa akikohoa, akijikunja, akiinua, au kujikamua.
Ngiri inaweza isionekane dhahiri kwa watoto wachanga, lakini, inaweza kuonekana mtoto akilia au kukohoa. Katika baadhi ya kesi, ultrasound inaweza kuhitajika kuangalia kama kuna ngiri.
Uchaguzi wa matibabu ya ngiri
Upasuaji ndio tiba peke inayoweza kurekebisha ngiri. Hata hivyo, ngiri ndogo isiyosababisha dalili yoyote huangaliwa kwanza kabla ya kuamua kufanya upasuaji. Upasuaji unaweza kuwa na athari zaidi kwa wagonjwa wenye matatizo mengine ya kimatibabu.
Upasuaji mara nyingi hufanyika kwa ngiri ambayo inaongezeka ukubwa na kusabaisha maumivu. Upasuaji huziba upenyo na kuimarisha tishu za ukuta wa tumbo zilizokuwa dhaifu. Siku hizi, karibia kila upenyo wa ngiri huzibwa kwa kitambaa maalumu imara ili kuhakikisha kuwa haufunguki tena.
Ngiri inayotokea kwenye kitovu (umblical), ambayo imeshindwa kuziba yenyewe mpaka mtoto anapofikisha umri wa miaka 5, Â inapaswa kurekebishwa kwa upasuaji.
Upasuaji wa dharura mara nyingine huhitajika kama utumbo au viungo vingine vilivyochoropoka na kusababisha ngiri, vimebanwa kwenye upenyo vilipotokea na kusababisha kukatishwa kwa mtiririko wa damu. Kama upasuaji hautafanyika mapema ili kunasua na kurejesha mtiririko wa damu, tishu huanza kufa.
Badala ya upasuaji wa wazi (open surgery), baadhi ya ngiri hurekebishwa kwa upasuaji wa kutumia kamera (laparoscopic). Matumizi ya kamera kwenye upasuaji huwa na faida zifuatazo:
- Huwa na mikato midogo
- Hupunguza muda wa kukaa hospitalini ili kuuguza kidonda
- Maumivu huwa kidogo baada ya upasuaji.
Nini cha kutarajia ukiwa na ngiri?
Matokeo kwa kawaida huwa ni mazuri baada ya matibabu. Kurudi kwa ngiri baada ya upasuaji ni nadra (1-3%).
Matatizo yanayoweza kutokea
Kwa nadra, katika hali isiyo ya kawaida, upasuaji wa kurekebisha ngiri unaweza kusababisha uharibifu wa viungo vingine vivyohusiana na utendaji kazi wa korodani za mwanaume.
Hatari nyingine ya upasuaji wa kurekebisha ngiri ni uharibifu wa neva, ambao unaweza kusababisha kupoteza uwezo wa kuhisi katika eneo la kinena. Hatari kubwa zaidi ya upasuaji wa kurekebisha ngiri ni ngiri nyingine, ambayo inaweza kutokea miaka mingi baadaye.
Kuzuia ngiri
- Tumia mbinu sahihi kuinua mizigo.
- Punguza uzito kama we ni mnene.
- Epuka kufunga choo kwa kula vyakula vyenye nyuzinyuzi kwa wingi, kunywa maji ya kutosha, nenda chooni mara tu baada ya kubanwa kunya na fanya mazoezi mara kwa mara.
- Wanaume wanapaswa kumwona mtoa huduma wa afya kama wanapata shida au kujikamua wakati wa kukojoa. Hii inaweza kuwa dalili ya tezi dume
Leave feedback about this