Last Updated on October 12, 2023 by Dr Mniko
Sababu ya magonjwa sugu
Magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza yanayohusiana na mtindo wa maisha yamekuwa yakiongezeka kwa kasi katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania. Awali, magonjwa haya yalikuwa yakiwaathiri zaidi watu wenye umri mkubwa (zaidi ya miaka 45) lakini kwa sasa magonjwa haya yanazidi kuathiri watu wenye umri mdogo wakiwemo watoto.
Magonjwa sugu makuu sita yasiyo ya kuambukiza (kisukari, shinikizo kubwa la damu, magonjwa ya moyo, magonjwa ya figo, saratani, magonjwa sugu ya njia ya hewa) yanajitokeza kwa wingi katika nchi zenye uchumi mdogo na wa kati.
Hali hii inatokana na mtindo wa maisha na ulaji ambao umebadilika kwa kasi kulinganisha na hali ilivyokuwa huko nyuma. Kwa mujibu ya Shirika la Afya Duniani (WHO), mitindo ya maisha isiyo bora ndio chanzo kikubwa cha kuongezeka kwa magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza duniani ambayo yamekuwa yakisababisha mamilioni ya vifo vya mapema kila mwaka.
Maendeleo ya kiuchumi ambayo ni pamoja na kuongezeka kwa kipato, ambacho huwapa watu uwezo wa kumudu gharama za nyenzo mbalimbali za kurahisisha kazi za kutumia nguvu ikiwa ni pamoja na magari, vifaa vya kutendea kazi, kompyuta, televisheni n.k ni miongoni ya mambo yanayochangia kuongezeka kwa magonjwa haya.
Matumizi ya nyenzo za kufanyia kazi au kutofanya mazoezi ya mwili huwafanya watu kulimbikiza nishati-lishe mwilini ambazo husababisha ongezeko la uzito wa mwili ambao huchangia kuongeza uwezekano wa kupata magonjwa hayo.
Mambo mengine yanayochangia magonjwa haya ni kuongezeka kwa watu wanaohamia mijini na mabadiliko ya tabia ya ulaji. Mabadiliko ya tabia na mtindo wa ulaji yamefanya jamii kubadilisha namna ya ulaji na aina ya vyakula vinavyoliwa.
Mabadiliko haya huifanya jamii kuachana na utaratibu wa kutumia vyakula vya asili, kutopika chakula kwa njia za asili, kutumia kwa wingi vyakula vyenye mafuta mengi, sukari na chumvi nyingi pamoja na nafaka ambazo zimekobolewa.
Matokeo ya mabadiliko haya ni ongezeko la magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza ambayo huathiri ubora wa maisha.
Vyanzo
https://diabetesatlas.org/upload/resources/previous/files/3/Diabetes-Atlas-3rd-edition.pdf
Leave feedback about this