Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maelezo ya jumla
Ugonjwa wa pepopunda au tetenasi ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria. Bakteria hawa huishi kwenye udongo, mate, vumbi na mbolea. Bakteria hawa mara nyingi huingia mwilini kupitia kwenye kidonda, mfano unapojikata na kisu au unapochomwa na msumari.
Je! Nini dalili za pepopunda?
Maambukizi ya ugonjwa huu husababisha misuli ya mwili mzima kukaza na kukakamaa. Inaweza kusababisha kukaza kwa taya za mdomo na kusababisha mgonjwa ashindwe kufungua mdomo au kumeza. Ikiwa hii itatokea, unaweza kufa kwa kukosa hewa.
- Kukaza kwa misuli ya taya kunakosababisha mtu ashindwe kufungua mdomo
- Kukaza na kukakamaa kwa misuli ya usoni kunakosababisha mgonjwa kukodoa macho (mwonekano wa mjusi aliyebanwa na mlango)
- Kukaza au kukakamaa kwa misuli ya shingo – shingo huwa ngumu
- Misuli ya kifua na miguu kukaza
- Kupata shida au ugumu kumeza
- Joto la mwili huongezeka
- Kuvuja jasho sana
- Kuongezeka kwa shinikizo la damu
- Mapigo ya moyo huongezeka kwa vipindi na kisha hurejea kawaida
- Kukaza kwa misuli kunaweza kutokea mara kwa mara na kudumu kwa dakika kadhaa, mwili wa mgonjwa hujikunja kuelekea nyuma (mgongo wa mgonjwa hupinda kuelekea nyuma )
- Pepopunda ya utotoni ni aina maalumu ya pepopunda inayowapata watoto wachanga.
Pepopunda husababishwa na nini?
Pepopunda mara nyingi huhusishwa na kutu, hasa misumari yenye kutu, lakini dhana hii inapotosha. Vitu venye kutu mara nyingi hupatikana nje au katika maeneo ambayo huhifadhi bakteria aina ya clostridium tetani. Kutu yenyewe haiwezi kusababisha pepopunda. Vyuma vyenye kutu hutoa mahala pazuri pakukaa kiiniyoga wa bakteria hawa, na msumari unapokuchoma huwaingiza mwilini . Kiiniyoga wa clostridum tetani hukua vyema katika maeneo yasiyo na oksijeni ya kutosha. Kidonda kisiposafishwa vyema, uwezekano wa bakteria hawa kukua ni mkubwa sana. Kama msumari uliokutoboa au kitu kilichokuchoma hakitatolewa na kidonda kusafishwa vyema, bakteria hawa huongezeka kwa haraka na wanaweza kuleta madhara makubwa.
Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata pepopunda?
Watu wanaoishi nchi zinazoendelea kama Tanzania, Kenya, Uganda n.k wako kwenye hatari kubwa kwa sababu ya kukosa chanjo.
Wakati gani utafute matibabu ya pepopunda haraka?
Jeraha lolote linapaswa kutibiwa haraka iwezekanavyo.
Utambuzi wa ugonjwa wa pepopunda
- Daktari mara nyingi hahitaji vipimo kutambua Pepopunda- dalili na ishara zinatosha kabisa
- Anaweza pia kufanya “Spatula test” – Daktari hutumia kifaa safi na kujaribu kugusa kilimi chako (sehemu ya nyuma ya ulimi) na kisha hutazama matokeo. Kama una pepopunda misuli ya taya zako itakaza na utakiuma kifaa hicho.Kama hauna pepopunda utabeua (kama unataka kutapika) ili kukiondoa kifaa hicho.
Uchaguzi wa matibabu
- Jeraha linapaswa kusafishwa.
- Kidonda kinapaswa kusafishwa vyema na tishu zilizooza kwenye kidonda kuondolewa kwa vifaa safi. Unaweza kuhitaji dawa za maumivu kwa zoezi hili.
- Utapewa dawa za antibiotiki- hasa metronidazole ili kusaidia kupunguza idadi ya bakteria wanaoleta madhara mwilini, dawa hizi japo zinapunguza idadi ya bakteria, hazisaidii kuondoa sumu ya bakteria hao mwilini.
- Penicillin ilitumika kutibu tetanasi hapo zamani, lakini haitumiki sana siku hizi kwa sababu ya hatari ya kuongeza kukaza kwa misuli.
- Anti-tetanus serum hutolewa ili kupambana na sumu ya clostridium tetani Serum hii husawazisha sumu ya bakteria hawa.
- Wagonjwa wote wa tetanasi wanapaswa kupewa chanjo dhidi ya ugonjwa huu
Kama hali ya mgonjwa wa tetanasi si mbaya sana:
- Anaweza kuchomwa sindano yenye kinga mwili dhidhi ya tetanasi kwenye msuli au kwenye mshipa
- Sindano ya metronidazole kwenye mshipa kwa siku 10
- Diazepam- Dawa hii hupunguza mkazo wa misuli ya mwili
Tetanasi kali
- Dawa yenye kinga mwili dhidi ya sumu inaweza kuchomwa moja kwa moja kwenye uti wa mgongo (hii huongeza uwezekano wa kupata nafuu toka 4% hadi 35%)
- Daktari anaweza kufanya upasuaji shingoni na kutoboa koromoa ili kufunga mashine ya kumsaidia mgonjwa kupumua –misuli ya shingo inaweza kukaza mpaka kufunga njia ya hewa – mgonjwa anaweza kupumua kwa mashine hii kwa wiki 3 hadi 4
- Dawa aina ya Magnésiamu, inaweza kutolewa kama drip ili kupunguza mkazo wa misuli ya mwili
- Diazepam inaweza kutolewa kama drip pia ili kupunguza mkazo wa misuli.
- Ukweli ni kuwa hali ya mgonjwa wa pepopunda hubadilika badilika na ni ngumu kuidhibiti (wakati mwingi joto la mwili hupanda na kushuka, shinikizo la damu huongezeka na kushuka wakati wowote) na unaweza kuhitaji dawa nyingi, kama labetalol, magnesiamu, clonidine, au nifedipine.
- Kwa sababu mgonjwa hawezi kupumua vyema bila msaada, daktari atahakikisha anapata oksijeni ya kutosha kwa kutumia mashine ya kusaidia kupumua. Atahakikisha pia anapata chakula cha kutosha – mara nyingi chakula hutolewa kupitia mrija wa chakula uliwekwa kupitia mdomoni mpaka tumboni/ mrija uliowekwa moja kwa moja tumboni kwa upasuaji. Kupona kunaweza kuchukua wiki 4 hadi 6.
Nini cha kutarajia ukiwa na tetenasi?
Ukiwa na pepopunda ,matibabu huchukua muda mrefu. Chanjo ya tetanasi inaweza kuzuia tetanasi, lakini ulinzi wake haudumu milele. Watu wazima wanapaswa kupata chanjo ya tetanasi, au nyongeza ya chanjo, kila baada ya miaka 10. Ukipata jeraha au ukiumia mwone daktari, unaweza kuhitaji chanjo.
Matatizo yanayoweza kutokea ukiwa na pepopunda
- Kifo
Asilimia 20-40 za watu wazima na 60-89 asilimia ya watoto wachanga wanaougua pepopunda hufa hata kama watatibiwa vizuri sana
Leave feedback about this