PUMU

PUMU

 • August 15, 2020
 • 0 Likes
 • 259 Views
 • 0 Comments

Maelezo ya jumla

Pumu (asthma), ni ugonjwa  unaosababishwa na mkazo wa ghafla (spasm) na kuvimba kwa njia ya hewa, hii husababisha, kifua kubana, kukorota, kupumua kwa shida na kukohoa.

Je, nini dalili za Pumu?    

 • Watu wengi wenye pumu, huwa wanapata shida ya kupumua wakati wa shambulio na baada ya shambulio la pumu mgonjwa hurudi katika hali yake ya kawaida mpaka atakapopata shambulio lingine.
 • Mashambulizi ya pumu yanaweza kudumu kwa dakika kadhaa mpaka siku kadhaa, na yanaweza kuwa hatari kama njia ya hewa imezuiliwa/imeziba.

Dalili ni pamoja na:    

 • Kikohozi kikavu au chenye makohozi.
 • Kuvutwa ndani kwa ngozi ilio katikati ya mbavu wakati kupumua
 • Kupumua kwa shida, kunakoongezeka baada ya kufanya mazoezi au shughuli nzito.
 • Kukorota/kuforota (wheezing):       
  • Hutokea kwa vipindi ,mgonjwa huwa hana dalili mpaka atakapopata shambulio.
  • Kukorota kunaweza kuongezeka zaidi  usiku au asubuhi sana.       
  • Kukorota kunaweza kutokea na kisha kutoweka bila dawa yoyote.
  • Kunaweza kupungua kwa kutumia madawa yanayofungua njia ya hewa (bronchodilators)       
  • Kukorota kunaongezeka mtu akivuta pumzi/ hewa baridi        
  • Kunaongezeka ukifanya mazoezi
  • Kunaongezeka mgonjwa akipata kiungulia         
  • Kwa kawaida huanza ghafla

Dalili za dharura:   

 • Rangi ya kibuluubuluu kwenye midomo na uso –hali hii huashiria kuwa mgonjwa anakosa hewa ya kutosha    
 • Kupungua kwa uchangamfu na kusinziasinzia au kuchanganyikiwa wakati wa shambulio   
 • Kupata shida sana kupumua.    
 • Mapigo ya moyo yanayoenda mbio.  
 • Uwoga/wasiwasi uliopitiliza unaotokana na kupumua kwa shida
 • Kutokwa jasho sana.

Dalili zinazohusiana zinajumuisha:    

 • Kupata shida kupumua (kutoa hewa nje kunachukua zaidi ya mara mbili ya muda na nguvu inaotumika kuvuta hewa ndani)
 • Huacha kupumua kwa muda   
 • Maumivu ya kifua    
 • Kutanuka kwa pua     
 • Kifua kubana

Pumu husababishwa na nini?    

 • Pumu husababishwa na kuvimba kwa njia hewa. Wakati shambulio la pumu linapotokea, misuli inayozunguka njia ya hewa hubana na sehemu ya ndani ya njia ya hewa huvimba na kusababisha kupungua kwa upana wa njia ya hewa. Hii inapunguza kiasi cha hewa kinachoweza kupita na kuyafikia mapafu.
 • Kwa watu ambao ni sensitive (wenye hisi kali), dalili za pumu zinaweza kuchochewa kwa kuvuta hewa yenye vitu vinavyosababisha mzio (allergy).
 • Vitu vya kawaida vinavyochochea kutokea kwa shambulio la pumu ni pamoja na:        
  • Nywele za wanyama
  • Vumbi        
  • Mabadiliko ya hali ya hewa (mara nyingi hali ya hewa ya baridi )        
  • Kemikali katika hewa au katika chakula        
  • Mazoezi        
  • Chavua         
  • Maambukizi kwenye mfumo wa hewa, kama mafua       
  • Hisia kali/msongo wa mawazo
  • Kuvuta tumbaku   
 • Kwa wagonjwa wengine aspirini na madawa mengine aina ya nonsteroidal anti-inflammatory drugs(NSAIDs) huchochea kupata shambulio la pumu.

Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata pumu?

Watu wengi wenye pumu wana historia binafsi ya kuwa na mzio au mwanafamilia ambaye ana historia ya mzio kama vile mafua yaletwayo na vumbi (Allergic rhinitis) au ukurutu (eczema). Hii inamaanisha watu wenye historia ya mzio wako kwenye hatari kubwa ya kupata pumu, ila hiyo haimaanishi ni wote, wapo wengine walio na pumu lakini hawana historia ya mzio.

Utambuzi    

 • Kwa kawaida dalili za pumu hutokea kipindi cha shambulio tu, na dalili hizo hutoweka baada ya shambulio na mgonjwa kuendelea na maisha kama kawaida. Ila kuna baadhi yao huwa na pumu yenye dalili za kudumu ,dalili hizi zinakuwepo wakati wote na mgonjwa anahitaji dawa kuzidhibiti. Kwa wagonjwa wa aina hii upimaji wa mzio unaweza kufanyika ili kutambua ni vitu gani vinavyosababisha mzio kwa mgonjwa huyo.
  • Visababishi vya mzio (allergens) ni pamoja na manyoya ya wanyama wa kufugwa, vumbi,mzio unaosababishwa na mende, na chavua.        
  • Kwa kawaida vitu vinavyosabisha harara kwenye njia ya hewa ni pamoja na kuvuta tumbaku, uchafuzi wa mazingira, na moshi unaotokana na moto au gesi.    
 • Daktari atatumia stethoscope (kifaa anachotumia daktari kusikiliza kifua ) ili kusikiliza mapafu. Sauti zinazohusiana na pumu zinaweza kusikika. Hata hivyo, sauti za mapafu ni za kawaida kama hakuna shambulio.
 • Vipimo vinavyoweza kufanyika ni pamoja na:         
  • Arterial blood gas- (kipimo hiki hupima kiwango cha gesi zilizopo kwenye damu)
  • Vipimo vya damu, kupima hesabu ya eosinophil (hii ni aina ya seli nyeupe ya damu ambayo huongezeka wakati wa mzio) na IgE (aina ya protini ya mfumo wa kinga inayoitwa immunoglobulin, hii pia huongezeka wakati wa shambulio).
  • Picha ya X-ray ya kifua        
  • Vipimo vya kupima kama mapafu yanafanya kazi yake vyema (lung function tests)        

Ni wakati gani utafute matibabu ya haraka?    

 • Mwone mhudumu wa afya ikiwa unaona dalili za pumu zinajitokeza.    
 • Nenda kwenye chumba cha huduma ya dharura ikiwa:        
  • Shambulio la pumu linahitaji dawa zaidi kuliko ilivyopendekezwa ili kutulia        
  • Dalili zinazidi kuwa mbaya au haupati nafuu hata baada ya kutumia dawa uliyopewa na daktari.
  • Unapata shida kupumua ,unashindwa kumaliza sentensi bila kuvuta pumzi unapozungumza.        
 • Nenda kwenye chumba cha dharura ikiwa:        
  • Umeanza kushikwa usingizi au umeanza kuhisi kuchanganyikiwa wakati wa shambulio la pumu.
  • unapata shida sana ya kupumua japo umepumzika/bila kufanya kazi/shughuli.
  • Una maumivu makali ya kifua

Uchaguzi wa matibabu    

 • Jambo muhimu zaidi ni kujaribu kuepuka vitu vinavyochochea au kusababisha shambulio la pumu, lakini pia tiba huwa na lengo la kupunguza kuvimba (inflammation) kwenye njia ya hewa. Ni muhimu wewe na daktari wako kuandaa na kutekeleza mpango wa matibabu, utakaokusaidia kuepuka mambo yanayosababisha shambulio na utakaoainisha jinsi ya kufuatilia dalili zako.
 • Kuna aina mbili za msingi za dawa za kutibu pumu:        
  • Dawa zinazazotumiwa kwa matibabu ya muda mrefu ili kuzuia mashambulizi ya pumu (Long-acting medications)    
  • Dawa zinazotumiwa kwa ajili ya kuleta nafuu kwa haraka wakati wa mashambulizi ya pumu  (Quick-relief medications)
 • Watu wenye pumu isiyo na mashambulizi ya mara kwa mara, wanaweza kutumia dawa za kuleta nafuu wakati wa shambulio wanapozihitaji ,baada ya kupata nafuu wagonjwa hawa hawahitaji dawa yoyote mpaka watakapopata shambulio lingine.
 • Wale wenye pumu ya kudumu wanapaswa kutumia dawa za kudhibiti pumu wakati wote kama alivyoelekeza daktari, ili kuzuia dalili . Mashambulizi makubwa ya pumu yanahitaji kuchunguzwa na daktari na, labda hata kulazwa hospitalini, kupewa oksijeni, na kuchomwa dawa kupitia mshipa.    
 • Peak flow meter ni kifaa rahisi kinachotumika kupima ni kwa kasi kiasi gani mgonjwa anaweza kutoa/kupumua hewa kutoka kwenye mapafu.
 • Inaweza kukusaidia kujua kama shambulio linakuja, wakati mwingine hata kabla dalili yoyote haijaonekana. Peak flow meter inaweza kusaidia kutambua wakati  gani unahitaji kutumia dawa au kuchukua hatua nyingine inahitajika kuchukuliwa.        
 • Kiwango cha peak flow cha 50-80%  ni ishara ya shambulizi la pumu la wastani, wakati kiwango chini ya 50% ni ishara ya shambulio kali.

Udhibiti wa pumu wa muda mrefu    

 • Madawa yanayotumika kwa muda mrefu ili kudhibiti pumu hutumiwa mara kwa mara ili kuzuia mashambulizi ,na si kuponya. Madawa haya hutumiwa na wagonjwa wanaopata mashambulio mara kwa mara.    
 • Madawa ya muda mrefu ya kudhibiti pumu ni pamoja na:        
  • Inhaled Corticosteroids (kama vile Azmacort, Vanceril, AeroBid, Flovent),unapovuta haya madawa yanazuia kuvimba kwa njia ya hewa. 
  • Leukotriene inhibitors (kama vile Singulair na Accolate)
  • Long-acting bronchodilators (kama vile Serevent) ,dawa hizi husaidia kufungua njia ya hewa        
  • Omalizumab, ambayo inazuia njia ambayo mfumo wa kinga ya mwili hutumia ili kusababisha dalili za pumu        
  • Cromolyn sodium au nedocromil sodium       
  • Aminophylline au theophylline (haitumiwi mara kwa mara kama zamani)    
 • Wakati mwingine dawa moja ambayo imechanganya steroids na bronchodilators hutumiwa (Advair, Symbicort)

Dawa zinazotumiwa kuleta nafuu ya haraka wakati wa shambulio (Quick-relief Medications)  

 • Dawa hizi,hutumiwa ili kupooza dalili wakati wa mashambulio na kuleta nafuu.    
 • Madawa ya kuleta nafuu haraka ni pamoja na:        
  • Short –acting bronchodilators (inhalers), kama vile Proventil, Ventolin, Xopenex, na zingine        
  • Corticosteroids, kama vile methylprednisolone, inaweza kuchomwa moja kwa moja kwenye mshipa, wakati wa shambulio kali, pamoja na dawa nyingine za kuvuta

Jinsi ya kujitunza nyumbani ukiwa na pumu.   

 • Ujuzi/mambo ya muhimu unayoitaji kuyafahamu ili kujitunza vyema ukiwa na pumu ni pamoja:
  • kujua dalili za pumu
  • kujua jinsi ya kujipima kwa peak flow meter vyema ukiwa nyumbani,na jitahidi kujua ina maanisha nini
  • Kuwa na namba ya simu ya daktari au mtoa huduma wa afya ,inaweza kuwa ya msaada wakati wa dharura.
  • kujua mambo ambayo husababisha /kuchochea pumu yako kuwa mbaya zaidi na nini cha kufanya wakati hili linapotokea.    
 • Watoto wenye pumu wanahitaji msaada mkubwa shuleni. Wanaweza kuhitaji msaada kutoka kwa wafanyakazi wa shule ili kudhibiti pumu.

Dawa za kuepuka ukiwa na pumu

Wagonjwa wanaopatikana na pumu wanapaswa kuepuka kutumia dawa zifuatazo:

 • Carvedilol
 • Diflunisal
 • Fluticasone
 • Labetalol
 • Nabumetone
 • Naproxen and esomeprazole magnesium
 • Olodaterol
 • Oxycodone
 • Penbutolol
 • Promethazine
 • Propranolol
 • Sotalol
 • Sulindac
 • Timolol

Ikiwa umegunduliwa kuwa una pumu,wasiliana na daktari wako kabla ya kuanza au kuacha dawa yoyote.

Kuzuia dalili za pumu   

 • Dalili za pumu zinaweza kupunguzwa kwa kuepuka vitu vinavyochochea kutokea kwa shambulio, kama una mzio na kitu flani na kinakuletea matatizo kiepuke.
 • Matandiko ya kulalia yanapaswa kufunikwa vyema ili yasipate vumbi. Ondoa mazulia kwenye vyumba vya kulala na safisha mara kwa mara. Vifaa na dawa za kusafishia nyumba visiwe na harufu kali.    
 • Jitahidi kupunguza unyevunyevu ndani ya nyumba, rekebisha sehemu zinazovuja ,hii itazuia kufunda kwa nyumba. Jitaidi kufanya usafi wa nyumba na kumbuka kufunika na kuweka mabaki ya chakula nje ya chumba cha kulala ,hii itasaidia kupunguza mende, ambao wanaweza kuchochea/kusababisha shambulio la pumu kwa watu wengine.    
 • Ikiwa mtu ana mzio (allergic) kwa mnyama ambaye hawezi kuondolewa nyumbani, mnyama huyo asiruhusiwe kuingia kwenye chumba chake cha kulala, na kama ikiwezekana mnyama huyo aondolewe kabisa kwenye nyumba anayokaa mgonjwa.
 • Jambo muhimu zaidi ambalo familia ya mtoto mwenye pumu inaweza kufanya ni kuondoa moshi wa tumbaku nyumbani. Kuvutia sigara nje ya nyumba haitoshi. Wanafamilia na wageni ambao wanavuta sigara ,japo wamevutia nje wanabeba mabaki ya moshi ndani ya nguo na nywele zao na kuuleta ndani, – hii inaweza kusababisha dalili za pumu.    
 • Watu wenye pumu pia wanapaswa kuepuka hewa iliochafuliwa, vumbi ya viwandani, na mvuke inaokera unaotoka viwandani na majumbani,kwa kadri inavyowezekana.

Nini cha kutarajia nikiwa na pumu ?

Hakuna tiba ya pumu inayoweza kukuponyesha kabisa. lakini dalili wakati mwingine hupoa kabisa baada ya muda fulani wa matibabu. Kwa usimamizi ulio bora, kujitunza binafsi na matibabu, watu wengi wenye pumu wanaweza kuishi maisha ya kawaida kabisa.

Matatizo yanayoweza kutokea ukiwa na pumu

Matatizo yatokanayo na pumu yanaweza kuwa makali. Baadhi ni pamoja na:    

 • Kifo    
 • Kupungua kwa uwezo wa kufanya mazoezi na kushiriki katika shughuli nyingine    
 • Ukosefu wa usingizi kutokana na dalili wakati wa usiku    
 • Mabadiliko ya kudumu ya utendaji kazi wa mapafu  
 • Kikohozi kisichokoma    
 • Kupata shida kupumua kunakohitaji mgonjwa kusaidiwa kupumua kwa mashine (ventilator)

Vyanzo   

http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/ency/article/000141.htm

 • Share:

Leave Your Comment