ROVU

 • August 15, 2020
 • 0 Likes
 • 171 Views
 • 0 Comments

Maelezo ya jumla

Rovu (goitre) ni hali ambayo husababisha kuvimba kwa tezi dundumio (thyroid gland ). Sababu  kubwa inayosababisha kuvimba kwa tezi dundumio ni ukosefu wa madini ya joto (iodine) katika mlo. Pia inaweza kusababishwa na magonjwa mengine mengi kama vile ugonjwa wa Graves, ugonjwa wa Hashimoto na saratani ya tezi dundumio. Ishara na dalili za kawaida za rovu ni uvimbe unaotokea shingoni, hisia ya kubanwa koo, kikohozi, kukwaruza kwa sauti na kuishiwa pumzi. Vipimo vya damu kupima kiwango cha homoni zinazotengenezwa na tezi dundumio, picha ya ultrasound na picha zingine za tezi zinaweza kusaidi katika utambuzi . Matibabu ya rovu (goitre) hutegemea sababu na ukubwa wa uvimbe.

Je, nini dalili za Rovu (Goitre)?

Sio kila rovu husababisha ishara na dalili. Lakini dalili zikitokea zinaweza kujumuisha:

 • Uvimbe shingoni, uvimbe huu huonekana kwenye sehemu ya chini ya shingo, uvimbe huu unaweza kuanza ukiwa mdogo na kuongezeka kuwa mkubwa kabisa.    
 • Hisia ya kubanwa kooni
 • Kukohoa    
 • Kukwaruza kwa sauti
 • Kupata shida kumeza    
 • Kupumua kwa shida/ kuishiwa pumzi
 • Uchovu   
 • Kuongezeka kwa hamu ya kula   
 • Hofu    
 • asiyetulia    
 • Kupungua kwa uzito    
 • Kubana kwa misuli

 Nani yuko kwenye hatari zaidi?

Rovu inaweza kumpata mtu yeyote. Baadhi ya sababu zinazoongeza hatari ya kupata goiter ni pamoja na:    

 • Ukosefu wa madini ya joto (iodine) kwenye chakula: Takwimu zinaonyesha kuwa watu wanaoishi katika maeneo yenye ukosefu wa madini joto na wasiopata iodine ya kutosha kwenye chakula huwa katika hatari kubwa ya kupata goiter.    
 • Jinsi ya kike: Tafiti zinaonesha kwamba wanawake wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata matatizo kwenye tezi dundumio kuliko wanaume.    
 • Umri zaidi ya miaka 50    
 • Historia binafsi au ya familia: Historia binafsi au ya familia ya kuwa na ugonjwa unaotokana na kinga ya mwili (Autoimmune disease) huongeza hatari ya kupata rovu. Kwa mfano: Hashimoto’s disease ~ mwenye ugonjwa huu, kinga ya mwili huharibu kabisa seli za tezi dundumio na kusababisha tezi kushindwa kufanya kazi, hii hupelekea kutokea kwa Rovu na Graves’ disease ~ mwenye ugonjwa huu, kinga ya mwili husababisha tezi dundumio kufanya kazi kuliko kawaida na kusababisha tezi kutengeneza homoni zake kwa wingi kupita kiasi, hii hupelekea kutokea kwa Rovu.   
 • Dawa fulani: Dawa zingine, kama vile immunosuppressants (dawa za kupunguza kinga ya mwili), antiretrovirals (dawa za kupunguza makali ya UKIMWI), amiodarone (hizi hurekebisha mapigo ya moyo yanapovurugika) na lithium (hutumika kutibu magonjwa ya akili), zinaweza kuongeza hatari ya kupata goitre.
 • Mionzi: Tafiti mbalimbali zimeonesha kuwa hatari ya kupata rovu huongezeka kama wagonjwa wametibiwa kwa tiba ya mionzi kwenye eneo la shingo au kifua. Hatari hii huongezeka pia kama wamepata mionzi katika kituo cha nyuklia wakati wa majaribio au hata kwa ajali.

Utambuzi   

 • Uchunguzi wa kiwango cha homoni: Vipimo vya damu hufanyika kuangalia kiwango cha homoni zinazotengenezwa na tezi dundumio, hii husaidia kutambua kama mtu ni mgonjwa. Kwa kawaida, viwango vya kawaida vya thyroid hormone (T3, T4) na thyroid-stimulating hormone (TSH) hugunduliwa. Lakini baadhi ya rovu husababisha tezi dundumio kutengeneza homoni kwa wingi kuliko kawaida na kusababisha kuongezeka kwa thyroid hormone (T3, T4) na kupungua kwa thyroid-stimulating hormone (TSH) kwenye damu.
 • Kipimo cha kingamwili (antibody): Kwa baadhi ya sababu za rovu kama vile ugonjwa wa hashimoto’s  na ugonjwa wa graves’  vipimo vya damu kuangalia kingamwili (antibodies) husaidia katika kufanya utambuzi.
 • Ultrasonography: Kipimo hiki hakisababishi maumivu na hutumia mawimbi ya sauti kuunda picha ya viungo vya ndani ya mwili. Wakati wa kipimo, transducer huwekwa juu ya shingo yako ili kuunda picha kwenye skrini ya kompyuta. Picha hizi zinaweza kuonesha ukubwa wa tezi na kama tezi ina vinundunundu.    
 • Thyroid gland scans: Kipimo hiki hutumia dawa yenye nguvu za kinyukilia. Wakati wa kipimo, isotopu ya miali nunurishi (Radioactive isotope) huchomwa kwenye mshipa wa mgonjwa. Kisha, kamera maalum hutoa picha ya tezi dundumio kwenye skrini ya kompyuta. Thyroid gland scan hutoa taarifa za nyongeza kuhusu asili na ukubwa wa tezi yako.

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Mwone mtoa huduma wa afya ikiwa una dalili za ugonjwa huu. Fuata mapendekezo ya mtoa huduma wa afya.

Uchaguzi wa matibabu

Matibabu ya rovu yanategemea sababu, ukubwa wa rovu, ishara na dalili za mgonjwa. Matibabu ya kawaida ni pamoja na dawa, upasuaji na radioactive iodine.    

 • Kuangaliwa tu: matibabu ya kumweka mgonjwa chini ya uangalizi hupendekezwa kwa mgonjwa ambaye rovu ni ndogo, na haisababishi matatizo yoyote, na vipimo vya homoni kwenye damu ni kawaida.
 • Madawa:   
  • Ukosefu wa madini joto (iodine): Kwa wale ambao rovu ni matokeo ya upungufu wa iodini, Lugol’s iodine au potassium iodine solution zinaweza kupendekezwa ili kuongeza madini hayo mwilini.    
  • Hypothyroidism: Ikiwa rovu imetokana na kuathiriwa kwa tezi dundumio, kulikosababisha isitengeneze homoni za kuutosha mwili, matibabu yake ni  kuongeza homoni hizo mwilini.
  • Kuvimba kwa tezi dundumio: Kwa wagonjwa wenye kuvimba tezi, dawa za aspirin au corticosteroid zinahitajika kupunguza uvimbe.    
  • Hyperthyroidism: Kwa rovu zinazosabaisha tezi dundumio kufanya kazi kupita kiasi na kutengeneza homoni nyingi kuliko mwili unavyohitaji, dawa za kudhibiti tezi dundumio kama vile propylthiouracil na methimazole zinahitajika kudhibiti viwango vya homoni.    
 • Upasuaji: Upasuaji unaweza kutumika kwa wagonjwa walio na    
  • Rovu kubwa ambayo inasumbua au kusababisha shida kupumua au kumeza
  • Rovu isiyo ya kawaida,yenye vinundunundu na inayosababisha hyperthyroidism (inayosababisha tezi dundumio kutengenezwa homoni nyingi kuliko kawaida)     
  • Saratani ya tezi dundumio
 • Radioactive iodine: Tiba hii hutumia iodini yenye miali nunurishi ili kuharibu seli za tezi dundumio inayotengeneza homoni kwa wingi kupita kiasi. Matibabu haya yanaweza kusababisha tezi hii kushindwa kutengeneza homoni tena baada ya matibabu, kwa sababu hii mgonjwa kuhitaji kutumia homoni ya kutengenezwa viwandani maisha yake yote. Homoni kama levothyroxine huhitajika ili kukabiliana na athari baada ya matibabu.

Jinsi ya kuzuia rovu    

 • Kutumia chumvi yenye madini joto husaidia kuzuia kupata rovu inayosababishwa na upungufu wa iodini.    
 • Kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa tezi dundumio kama ulivyoelekezwa na daktari kama unatumia dawa kama vile immunosuppressants, antiretrovirals, amiodarone na lithium.
 • Kuepuka au kupunguza kukutana na mionzi.

Nini cha kutarajia?

Matokeo ya goitre yanategemea sababu za ugonjwa huo. Matokeo ya goitre inayosababishwa na saratani ya tezi dundumio ni mabaya zaidi kuliko ya ile inayosababishwa na magonjwa mengine, kama vile Grave’s disease, Hashimoto disease na upungufu wa madini joto.

Vyanzo

http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/ency/article/001178.htm

 • Share:

Leave Your Comment