SARATANI: Mlo/Chakula/Ulaji unaofaa

Saratani

Saratani ni ugonjwa unaotokana na seli za mwili zilizopoteza mfumo wake wa kugawanyika na hivyo hazipo katika hali yake ya kawaida. Huweza kugawanyika bila mpangilio maalum na kuharibu mkusanyiko wa seli nyingine. Seli za saratani hutokea sehemu moja ya mwili na zinaweza kusambaa sehemu nyingine za mwili kupitia mfumo wa damu na limfu. Saratani inaweza kuwa ya kurithi au kusababishwa na hali ya mazingira ya vitu mbalimbali kama vile ulaji wa vyakula vyenye visababishi vya saratani (carcinogenic compounds), ulaji usiofaa, unywaji wa pombe, uvutaji sigara au mionzi hatari, “asbestos”, lisasi (lead), uranium na zebaki. Zipo pia baadhi ya saratani zinazosababishwa na virusi kama hepatitis B ambayo huleta saratani ya ini na human papiloma inahusishwa na saratani ya shingo ya kizazi. Saratani huweza kutokea kwenye sehemu mbalimbali za mwili kama vile mapafu, matiti, ovari, kibofu cha mkojo, shingo ya uzazi, utumbo, koo, kinywa, tezi dume, ini na ngozi.

Ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha ni vigezo muhimu sana katika kuzuia saratani na pia ni sehemu muhimu ya matibabu na kudumisha maisha bora baada ya kupata matibabu. Matumizi ya baadhi ya vyakula huweza kuongeza uwezekano wa kupata baadhi ya saratani na vyakula vingine hupunguza uwezekano wa kupata saratani. Uzito wa mwili ukiwa mkubwa unaweza pia kuongeza uwezekano wa kupata baadhi ya saratani. Ni muhimu kufuata mtindo bora wa maisha kwani ni bora kuzuia kuliko kutibu.

Mambo yanayohusiana na mtindo wa maisha yanayoweza kuchangia katika kupata sarataniSaratani

Tafiti zinaonesha kwamba saratani za kurithi ni chache sana ila saratani nyingi hutokana na sababu za kimazingira. Tafiti nyingi zimeonesha kuwa kiasi cha asilimia 40 hadi 60 za saratani husababishwa na mtindo wa maisha usiofaa hasa ulaji usiofaa na kutofanya mazoezi ya mwili.

Haya ni mambo yaliyo katika uwezo wa kila mtu kuyadhibiti. Mtindo wa maisha usiofaa unajumuisha:

 • Ulaji wa vyakula vyenye nishati-lishe kwa wingi ambavyo husababisha unene. Unene umeonekana kuhusiana na saratani ya mji wa kizazi, matiti, figo, tezi dume, utumbo mpana na kibofu cha mkojo; ­
 • Ulaji wa nyama nyekundu kwa wingi na zile zilizosindikwa vimehusishwa na saratani ya tezi dume, utumbo mpana, mapafu, kinywa na koo; ­
 • Utumiaji wa pombe kwa wingi huongeza hatari ya kupata saratani ya mdomo, koo, koromeo, utumbo mpana, kongosho, ini na matiti;
 • Vyakula vilivyosindikwa kama soseji, jibini na bia na baadhi ya vyakula vya makopo vina kemikali zinazoitwa nitrosamines ambazo husababisha saratani za kinywa, koo, tezi la kiume, utumbo mpana, mapafu na tumbo; ­
 • Vyakula vilivyoota ukungu, kama karanga, mkate na nafaka huwa na kemikali zinazojulikana kama aflatoxins ambazo husababisha saratani ya ini; ­
 • Uvutaji wa sigara na bidhaa za tumbaku husababisha saratani ya mapafu, kinywa na koo ­
 • Kutofanya mazoezi ya mwili kunahusishwa na saratani ya utumbo mpana, matiti, kizazi, mapafu na tezi la kiume.

Ushauri wa chakula na lishe wa jinsi ya kukabiliana na matatizo ya kiafya yanayoambatana na kuwa na saratani au tiba yake

Matatizo mbalimbali yanaweza kujitokeza kutokana na hatua ya ugonjwa au aina ya matibabu mgonjwa anayopata, hasa dawa za saratani au mionzi. Baadhi ya matatizo yanayojitokeza huweza kuathiri ulaji wa chakula au kudhibitiwa kwa chakula, hivyo mgonjwa anahitaji ushauri. Matatizo hayo ni kama kukonda, upungufu wa damu, kukosa hamu ya kula, kichefuchefu, kutapika, kuhara, kukosa choo, vidonda kinywani, matatizo ya kumeza na matatizo ya ngozi.

Kukonda

Wagonjwa wengi wa saratani wanapungua uzito wakati wa matibabu. Hii inaweza kusababishwa na madhara ya saratani yenyewe, ongezeko la mahitaji ya virutubishi mwilini, kukosa hamu ya kula, aina ya matibabu anayopata mgonjwa (dawa, mionzi au upasuaji). Yafuatayo huweza kusaidia katika kukabiliana na tatizo hili: –

 • Kuzingatia ulaji wa mlo kamili na ulaji wa aina mbalimbali za vyakula; –
 • Kuongeza ulaji wa vyakula vyenye protini kwa wingi yenye asili ya wanyama (isipokuwa nyama nyekundu) na mimea
 • Kula vyakula vilivyo laini vilivyoboreshwa kwa kuongezewa vyakula vyenye protini na nishati-lishe kwa wingi
 • Kula milo midogo midogo mara kwa mara na kuongeza asusa zenye virutubishi vingi;
 • Kujitahidi kula wakati una hamu ya kula au ukiwa na njaa kali na kula vyakula vile vyenye virutubishi kwa wingi;
 • Kufanya mazoezi kabla ya kula (kama vile kutembea) ili kuongeza hamu ya kula na kusaidia uyeyushwaji wa chakula;
 • Kula taratibu, usile kwa haraka bali jipe muda wa kutosha wakati wa kula; – Kutumia viungo vyenye harufu unayoipenda;
 • Kutumia vinywaji kati ya mlo na mlo na sio wakati wa kula kuepuka tumbo kujaa na hivyo kushindwa kula chakula cha kutosha; na
 • Kutumia vinywaji vyenye virutubishi vingi na nishati-lishe.

Upungufu wa damusaratani

Upungufu wa wekundu wa damu huweza kusababishwa na saratani yenyewe au matibabu yake. Pia huweza kutokana malaria, minyoo na ulaji duni hususani kula vyakula vyenye upungufu wa madini chuma. Upungufu wa wekundu wa damu huweza kukabiliwa kwa:-

 • Kula vyakula vyenye madini chuma kwa wingi hususan vyenye asili ya wanyama (epuka nyama nyekundu). Aina ya madini chuma iliyopo katika mayai na maziwa haifyonzwi na mwili kwa ufanisi.
 • Kula matunda kwa wingi kila siku. Tumia matunda yenye Vitamini C kwa wingi pamoja na mlo kwani husaidia ufyonzwaji wa madini chuma yanayopatikana kwenye vyakula vyenye asili ya mimea.
 • Kuepuka vinywaji vyenye kafeini kama chai, kahawa au soda wakati wa mlo, kwani huzuia ufyonzwaji wa madini chuma yanayopatikana kwenye vyakula vya mimea;
 • Kutumia vinywaji kama togwa, rozela, mtindi au uji wa kimea kwani vinaongeza ufyonzwaji wa virutubishi muhimu; na – Kufuata ushauri wa mtaalam wa afya kuhusu matumizi ya vidonge vya madini chuma na foliki asidi na kutibiwa magonjwa kama vile malaria na minyoo.

Kukosa hamu ya kula

Kukosa hamu ya kula ni moja ya matatizo yanayoweza kusababishwa na saratani yenyewe au matibabu yake. Yafuatayo yanaweza kuongeza hamu ya kula:

 • Kujaribu vyakula vya majimaji au vilivyopondwa;
 • Kula milo midogo midogo mara nyingi kwa siku badala ya kula chakula kingi kwa mara moja;
 • Kutumia vyakula vyenye nishati – lishe kwa wingi;
 • Kuongeza asusa na kuziweka sehemu ambayo ni rahisi kuchukua mtu anaposikia hamu;
 • Kunywa vinywaji mbalimbali kama juisi halisi ya matunda, supu na vinginevyo, kidogo kidogo mara kwa mara;
 • Kufanya mazoezi ya mwili kwani husaidia kuongeza hamu ya kula
 • Kutumia viungo kwa kiasi katika chakula;
 • Kujaribu kubadili aina na ladha ya vyakula unavyotumia; na
 • Kula pamoja na watu wengine kama familia.

Kichefuchefu

Kichefuchefu huweza kujitokeza kutokana na matibabu ya saratani kama upasuaji, dawa au mionzi. Mara nyingi kichefuchefu huisha baada ya matibabu kumalizika. Kichefuchefu kinasababisha kutoweza kula chakula cha kutosha. Ili kupunguza kichefuchefu yafuatayo yaweza kusaidia:

 • Jaribu vyakula ambavyo ni rahisi kuyeyushwa tumboni kama mtindi au uji wa kimea;
 • Jaribu vyakula vikavu kama mkate uliochomwa (toast) lakini usiungue, viazi vya kuchemsha, wali, biskuti, au mkate mkavu;
 • Epuka vyakula vyenye mafuta mengi au vilivyokaangwa, vyakula vyenye sukari nyingi kama keki na vile vyenye viungo vikali au harufu kali;
 • Kula kiasi kidogo kidogo, taratibu na mara kwa mara;
 • Jaribu vinywaji vyenye viungo kama tangawizi, ndimu au minti;
 • Wakati wa kula kaa sehemu yenye hewa safi na ya kutosha na epuka chumba kisichokuwa safi, chenye joto, au chenye harufu ya vyakula ambayo vinaweza kukuletea kichefuchefu; Lishe na Saratani 11 Vidokezo Muhimu
 • Kunywa vinywaji kati ya mlo na mlo ili kupunguza kiu wakati wa mlo;
 • Kula zaidi vyakula unavyopenda;
 • Kula vyakula vilivyopoa au vyenye joto kidogo, na pumzika baada ya kula;
 • Safisha kinywa kabla na baada ya kula na jaribu kufyonza limau au ndimu kidogo, kumumunya ubuyu au ukwaju;
 • Kama kichefuchefu kinatokea wakati wa matibabu ya saratani, acha kula saa moja au mbili kabla ya matibabu kuanza, na siku ya matibabu kula vyakula visivyo na harufu kali au viungo vikali; na
 • Jaribu kukumbuka ni wakati gani kichefuchefu hukutokea (angalia chakula au mazingira yanayoongeza kichefuchefu) na kama inawezekana jaribu kubadili mpangilio wa kula na mshirikishe daktari wako.

Mabadiliko ya ladha

Tatizo hili hujitokeza zaidi wakati wa tiba ya mionzi.

 • Jaribu vinywaji vilivyoongezwa ladha kwa limau, ndimu au matunda mengine yenye uchachu;
 • Ongeza matumizi ya matunda; na
 • Matumizi ya viungo kwenye chakula au vinywaji huweza kuongeza ladha.

Kutapika

Kutapika huweza kutokea baada ya kichefuchefu, pia huweza kusababishwa na aina ya matibabu, harufu ya chakula au kujaa kwa gesi tumboni. Iwapo kutapika kunazidi au kunaendelea zaidi ya siku moja au mbili baada ya matibabu ya saratani, muone daktari. Ushauri ufuatao unaweza kukusaidia usitapike zaidi:

 • Baada ya kutapika keti au lala ukiwa umejiegemeza/umeinua mgongo;
 • Subiri kidogo kutapika kupungue ndio uanze kunywa kidogo kidogo;
 • Anza kwa kutumia vinywaji kama supu nyepesi, supu ya kuku aliyechemshwa, juisi nyepesi au maji;
 • Unapoweza kumudu, jaribu chakula laini, kwa mfano: matunda yaliyopondwa, juisi, maziwa ya mgando, supu zitokanazo na mbogamboga, uji ulioongezwa limau au ndimu; na
 • Unapojisikia umerudi kwenye hali ya kawaida, rudia kula chakula cha kawaida.

Kuharisha

Kuharisha kunaweza kutokana na matibabu ya saratani kama dawa, mionzi sehemu ya tumbo, uambukizo, kupatwa na mshituko wa kihisia; pia kuondolewa kwa sehemu ya tumbo, kongosho, utumbo mwembamba au mpana. Kuharisha kukiendelea kunaweza kusababisha upungufu wa maji, upotevu wa virutubishi mwilini au hata matatizo mengine ya afya. Yafuatayo huweza kupunguza tatizo la kuharisha:

 • Usiogope kunywa vitu vya maji-maji;
 • Kunywa maji safi na salama kwa wingi ili kuzuia upungufu wa maji mwilini (zaidi ya lita moja na nusu (glasi 8) kwa siku);
 • Tumia vyakula/vinywaji vya maji-maji kwa wingi zaidi. Vinywaji kama supu ya mchele, madafu, togwa, supu, juisi ya matunda halisi na maji yenye mchanganyiko wa sukari na chumvi (ORS) vinaweza kutumika;
 • Kula ndizi mbivu na mboga-mboga zilizopikwa kama karoti au maboga. Vyakula hivi hurudisha mwilini madini na vitamini zinazopotea kutokana na kuharisha;
 • Tafuna chakula kwa muda mrefu au kula vyakula vilivyo laini kwani ni rahisi kumeza na huyeyushwa kwa urahisi;
 • Kula vyakula vyenye uvuguvugu na sio vya moto sana au baridi sana;
 • Epuka vyakula vyenye mafuta mengi, viungo vingi au pilipili nyingi kwani vyakula hivi huweza kuzidisha kuharisha;
 • Wakati huu epuka kutumia matunda yasiyoiva vizuri au yenye uchachu mkali kama nyanya, ndimu, limau kwani wakati mwingine huweza kuongeza tatizo;
 • Epuka vyakula na vinywaji vinavyosababisha gesi kwa wingi tumboni kama maharagwe, kabichi au soda;
 • Epuka vinywaji vyenye kafeini kama chai, kahawa na soda kwani hivi husababisha upotevu zaidi wa maji, badala yake jaribu vinywaji vyenye viungo kama tangawizi, mchaichai, hiliki nk.;
 • Epuka matumizi ya pombe kwani huzuia baadhi ya virutubishi kufyonzwa na huongeza upotevu wa maji mwilini;
 • Epuka maziwa freshi kama yanasababisha kuharisha na jaribu kutumia mtindi;
 • Wakati huu epuka vyakula vyenye makapi-mlo kwa wingi kama nafaka zisizokobolewa, jamii ya kunde, maganda ya matunda, kwani haviyeyushwi kwa urahisi na hivyo huongeza kuharisha;
 • Jaribu vyakula kama wali, mkate au viazi vya kuponda, nyama ya kuku, samaki au yai la kuchemsha; Lishe na Saratani 13 Vidokezo Muhimu
 • Jaribu kuchanganya vitunguu saumu vilivyopondwa kwenye vinywaji kama supu na vinginevyo vilivyochemshwa;
 • Kula milo midogo midogo mara nyingi ili kurudisha virutubishi vinavyopotea na kukidhi mahitaji ya mwili kilishe;
 • Ukizidi kuharisha mwone daktari mapema kwa ushauri zaidi; na
 • Mara unapoacha kuharisha rudia kula vyakula vyote kama kawaida.

Kukosa choo au kupata choo kigumu sanaSaratani

Kukosa choo au kupata choo kigumu ni tatizo mojawapo linaloweza kujitokeza kwa watu wenye saratani. Hii huweza kusababishwa na matumizi ya dawa, kutokula chakula cha kutosha na chenye makapi-mlo kwa wingi.

Mgonjwa anashauriwa kufanya yafuatayo:

 • Kunywa maji mengi yaliyo safi na salama angalau lita moja na nusu kwa siku (glasi 8) au zaidi;
 • Kunywa vinywaji vya moto vyenye viungo kama tangawizi, ndimu, nk.;
 • Kutumia vyakula vinavyotokana na nafaka ambazo hazijakobolewa kama dona, unga wa ngano au mchele usiokobolewa sana n.k.;
 • Kula matunda na mboga-mboga kwa wingi, pia vyakula vya jamii ya kunde kama kunde, choroko, maharagwe n.k. kwani huwa na makapi-mlo kwa wingi;
 • Kutumia matunda kama papai, parachichi au embe kwani vimeonekana kusaidia kulainisha choo;
 • Kutumia matunda yaliyokaushwa kama yanapatikana;
 • Jaribu kufanya mazoezi (kama kutembea) kwani husaidia chakula kuyeyushwa;
 • Jipe muda wa kutosha chooni wakati wa kujisaidia, usiwe na haraka;
 • Jaribu kutumia choo muda uleule kila siku hata kama hujisikii km. mara baada ya kula; na
 • Tatizo likizidi mwone daktari kwa matibabu zaidi.

Vidonda kinywani au kooni

Vidonda vya kinywani au kooni huweza kufanya ulaji wa vyakula kuwa mgumu na hivyo kupunguza kiasi cha chakula anachoweza kula mgonjwa. Yafuatayo huweza kusaidia:

 • Kula vyakula vilivyopondwa au laini kama mtindi, mtori, uji ulioboreshwa au matunda kama parachichi, papai, ndizi, n.k.;
 • Epuka vyakula vyenye viungo vikali au ladha kali;
 • Epuka vyakula vya moto au vyenye pilipili kali;
 • Epuka vyakula vyenye sukari nyingi kwani sukari huchochea vidonda kuongezeka;
 • Kusukutua kinywa kwa kutumia maji yaliyochemshwa yenye kitunguu saumu au mdalasini. Rudia kila baada ya saa 3 hadi 4;
 • Inapowezekana, tumia mrija wakati wa kunywa au kula;
 • Jaribu kumung’unya barafu (iliyotengenezwa kwa maji safi na salama) kama zinapatikana kwani huweza kupunguza maumivu kinywani; na
 • Jaribu kutumia maziwa ya mgando (mtindi) mara kwa mara, kwani mtindi hutuliza maumivu na pia huzuia ukuaji wa fangasi.

Tatizo la kumeza

Tatizo la kumeza linaweza kutokana na aina ya saratani au matibabu anayopata mgonjwa, kama upasuaji wa sehemu za kichwani au shingoni. Tatizo hili linaweza kutokana pia na sababu nyingine. Unapokuwa na tatizo la kumeza muone daktari mapema kwa matibabu au ushauri.

Yafuatayo yanaweza kurahisisha umezaji:

 • Vuta ndani pumzi kabla ya kujaribu kumeza, kisha meza halafu toa pumzi au kohoa kidogo;
 • Kula kidogo kidogo lakini mara kwa mara;
 • Kula chakula kilichopondwa. Ongeza ulaini kwa kutumia maziwa au supu, ili pia kuongeza ubora wa chakula;
 • Hakikisha unakunywa maji ya kutosha kwa siku (angalau glasi 8), unaweza kutumia pia vinywaji vingine vya majimaji kama juisi ya matunda halisi, madafu au togwa. Vinywaji vitumike kati ya mlo na mlo ili visijaze tumbo wakati wa kula chakula;
 • Vinywaji vya uvuguvugu ni rahisi zaidi kumeza kuliko vile vya baridi sana au moto sana; Lishe na Saratani 15 Vidokezo Muhimu
 • Mtu anapotumia vyakula vya majimaji ana hatari ya kutotumia vyakula vyenye makapi-mlo kiasi cha kutosha. Ni muhimu kuhakikisha vyakula vilivyopondwa au kusagwa ni pamoja na mboga-mboga, aina mbalimbali za kunde au maharage. Uji uwe wa dona, ulezi, uwele au mtama usiokobolewa; na
 • Kama unapomeza unakabwa, unapaliwa au unakohoa muone daktari mapema.

Homasaratani

Homa husababishwa na uambukizo mbalimbali unaompata mtu yeyote ikiwa ni pamoja na mtu mwenye saratani. Yafuatayo husaidia:

 • Kunywa maji na vinywaji vingine kwa wingi mara kwa mara kupunguza joto la mwili na kuepuka upotevu wa maji mwilini. Tumia pia vinywaji kama madafu, togwa, juisi ya matunda halisi, vinywaji vinavyoongezwa viungo kama minti nk;
 • Kula milo midogo midogo mara nyingi ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya mwili wakati wa homa;
  • Kupunguza nguo nzito mwilini;
  • Kuoga kwa maji ya uvuguvugu; na
  • Mwone daktari kwa ushauri na matibabu.

Matatizo ya ngozi

Matatizo ya ngozi huweza kumpata mtu yeyote. Pia zipo aina za saratani ambazo huathiri ngozi zaidi. Hata hivyo baadhi ya matatizo ya ngozi husababishwa na upungufu wa baadhi ya vitamini kwa mfano Vitamini A na B6 . Ni muhimu mgonjwa kumwona daktari na kupata matibabu kulingana na sababu za tatizo lake.

Pamoja na matibabu, ulaji wa vyakula vyenye Vitamini A na/au Vitamini B6 kwa wingi huweza kupunguza tatizo. Vyakula vyenye vitamini A kwa wingi ni mboga zenye rangi ya kijani, mawese, maini, mayai, maziwa, jibini, matunda na mboga zenye rangi ya manjano kama embe, papai, karoti na maboga. Vyakula vyenye Vitamini B6 kwa wingi ni kama maharagwe, mboga za kijani, karanga, mahindi, nyama na parachichi.

Kujaa maji mwilini

Baadhi ya wagonjwa wa saratani wanaweza kuwa na tatizo la kujaa maji mwilini. Uzito unaongezeka, lakini hautokani na unene bali ni kuvimba mwili (idima). Tatizo hili linaweza kutokana na dawa anazotumia mgonjwa au tatizo lingine. Ni vema kumwona daktari kwa matibabu au ushauri mapema unapoona tatizo hili.

Yafuatayo ni muhimu

 • Endelea kunywa maji ya kutosha kama kawaida kila siku;
 • Fanya mazoezi ya mwili kadiri inavyowezekana, kama kutembea au shughuli nyingine zinazotumia viungo vya mwili;
 • Punguza matumizi ya chumvi kwani huongeza kujaa maji mwilini;
 • Unapoketi weka miguu sehemu iliyoinuka ( miguu isining’inie); na
 • Mwone daktari kwa matibabu zaidi.

Mbinu za kupunguza uwezekano wa kupata sarataniSaratani

Mtindo wa maisha usiofaa huchangia kwa kiasi kikubwa aina nyingi za saratani. Kufuata kwa makini ulaji na mtindo bora wa maisha kutakuwezesha kupunguza uwezekano wa kupata saratani. Huu ni uamuzi ambao kila mmoja anaweza kuufanya. Yafuatayo ni muhimu:

Tumia zaidi vyakula vitokanavyo na mimea:

Tafiti zimeonesha kuwa, vyakula hivi vinaweza kupunguza uwezekano wa kupata karibu aina zote za saratani.

 • Kula mbogamboga na matunda kwa wingi kila siku;
 • Kula mbogamboga za kijani, njano, nyekundu, zambarau na rangi nyingine zilizopikwa angalau ujazo wa kikombe kimoja katika kila mlo. Kutumia pia mboga zisizopikwa, kama vile saladi, nyanya, matango na kuchanganya mboga au matunda ya rangi mbalimbali kwani huongeza ubora wake;
 • Kula matunda ya aina mbalimbali (kama topetope, mastafeli, zambarau, embe, pera, chungwa, ubuyu, nk,) angalau tunda moja katika kila mlo. Kula tunda ni bora kuliko kunywa juisi;
 • Kujenga tabia ya kutumia nafaka zisizokobolewa kama vile unga wa dona, mchele wa brauni, unga wa ngano usiokobolewa, pia ulezi, mtama au uwele katika kila mlo;
 • Kutumia vyakula mbalimbali vya jamii ya kunde kama vile maharagwe, kunde, njugu mawe, dengu, choroko na mbaazi.

Kunyonyesha watoto

Wanawake wawe na tabia ya kunyonyesha watoto kwani tafiti zimethibitisha kuwa mwanamke anayemnyonyesha mtoto anapunguza uwezekano wa kupata saratani ya matiti na ovari. Pia mtoto aliyenyonya maziwa ya mama kama inavyoshauriwa anapunguza uwezekano wa kuwa na uzito wa mwili unaozidi kiasi (unene) utotoni, na hivyo kupunguza uwezekano wa unene ukubwani, kwa maana hiyo anapunguza uwezekano wa kupata saratani.

Inashauriwa mtoto anyonyeshwe maziwa ya mama pekee bila kupewa kitu kingine chochote (hata maji) katika miezi sita ya mwanzo. Baada ya miezi sita aendelee kunyonyeshwa na kupewa chakula cha nyongeza hadi atimize umri wa miaka miwili au zaidi.

Kuwa na uzito wa mwili ulio sahihi:

Uzito wa mwili uliozidi unachangia kupata saratani hasa zile za kinywa, koo, matiti, utumbo mpana, ini, kongosho na kizazi. Unene pia huongeza hatari ya uvimbe wa saratani kurudi tena hata pale ambapo ulishatolewa.

Fanya mazoezi ya mwili

Tafiti zimeonesha kuwa kufanya mazoezi ya mwili husaidia kupunguza uwezekano wa kupata saratani hasa zile za matiti, tezi dume, utumbo mpana, mapafu, kongosho na kizazi. Kufanya mazoezi pia huchangia kuzuia au kupunguza unene ambao pia unahusishwa na saratani za aina nyingi. Pia mazoezi huusaidia mwili kuwa mkakamavu na husadia chakula kufanya kazi vizuri mwilini na kuwezesha mwili kutumia nishati – lishe ya ziada.

Punguza matumizi ya nyama nyekundu

Utumiaji wa nyama nyekundu kwa wingi umeonekana kuongeza uwezekano wa kupata saratani hasa za utumbo mpana, kinywa, koo, mapafu na kongosho. Kama unatumia nyama nyekundu hakikisha isiwe zaidi ya nusu kilo kwa wiki. ­

Epuka matumizi ya nyama zilizosindikwa

Tafiti zimethibitisha kwamba nyama iliyosindikwa, hata inapoliwa kwa kiasi kidogo huongeza sana uwezekano wa kupata saratani hasa zile za utumbo mpana, kinywa, koo, mapafu na tezi ya kiume. Nyama zilizosindikwa ni pamoja na zile zilizohifadhiwa kwa kuongezwa chumvi, mafuta, kemikali au kukaushwa kwa moshi. Nyama hizo ni pamoja na nyama za kopo, soseji, bekoni, salami n.k.

Punguza matumizi ya chumvi

Chumvi huongeza uwezekano wa kupata saratani hasa ya tumbo. Mahitaji ya chumvi kwa siku ni wastani wa gramu 5 (kijiko kimoja cha chai). Vyakula vingi huwa na chumvi ya asili. Jaribu kuongeza ladha kwenye chakula kwa kutumia viungo mbalimbali badala ya chumvi. Gundua chumvi iliyojificha kwenye vyakula vilivyosindikwa na usiongeze chumvi kwenye chakula wakati wa kula.

Epuka vyakula vilivyoota fangasi au ukungu

Vyakula vilivyoota fangasi au ukungu vimeonekana kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya ini. Vyakula hivyo hutoa sumu iitwayo aflatoxin ambayo inahatarisha afya na pia huweza kuongeza uwezekano wa kupata saratani.

Epuka utumiaji wa tumbaku au sigara

Utumiaji wa tumbaku au sigara huongeza hatari ya kupata saratani hasa zile za mapafu, kinywa na koo. Uvutaji wa sigara pia huingilia na kudhoofisha mfumo wa kinga ya mwili. Kumbuka hata unapokuwa karibu na mtu anayevuta sigara wewe pia unavuta ule moshi hivyo unapata madhara pia.

Epuka matumizi ya pombe

kupita kiasi Matumizi ya pombe aina yoyote huongeza uwezekano wa kupata saratani hasa zile za kinywa, koo, utumbo mpana, matiti na ini. Pombe huweza kuingilia umeng’enywaji wa chakula na ufyonzwaji wa virutubishi mwilini. Pia huingilia uhifadhi wa baadhi ya vitamini na madini mwilini.

Vyanzo

https://www.tfnc.go.tz/publications/9

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi