SARATANI YA MATITI:Sababu,dalili,matibabu,kuzuia

Maelezo ya jumla

Saratani ya matiti ni kansa ya matiti inayotokea kwenye tishu za matiti. Inatokea kwa wanaume na wanawake. Saratani ya matiti kwa wanaume hutokea kwa nadra. Dalili zake ni pamoja na; Kuvimba titi, kuchubuka au kubonyea kwa ngozi ya titi, maumivu ya titi/chuchu, kurudi ndani kwa chuchu (retraction), wekundu, kukakamaa kwa ngozi ya titi na kutokwa na majimaji kwenye matiti (tofauti na maziwa). Matibabu hujumuisha upasuaji, tiba ya mionzi, tibakemikali, tiba ya homoni na tiba za kulenga seli za kansa ”targeted therapy”.

Je, nini dalili za kansa ya matiti?

Dalili zinaweza kujumuisha uvimbe ndani ya titi, mabadiliko ya ukubwa au umbo la titi na chuchu kutoa majimaji.

 • Kuvimba kwa sehemu ya titi au titi lote (hata kama hakuna bonge unaloligusa)
 • Kuchubuka na kubonyea kwa ngozi ya titi
 • Maumivu ya titi au chuchu
 • Kurudi ndani kwa chuchu
 • Wekundu na kukakamaa kwa chuchu na ngozi ya titi
 • Kutokwa na majimaji

Matatizo mengine ya kiafya yanaweza kusababisha dalili hizi. Ni daktari pekee anayeweza kutofautisha kwa uhakika. Mtu yeyote mwenye dalili hizi anapaswa kumwona daktari ili tatizo lake ligunduliwe mapema iwezekanavyo.

Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata saratani ya matiti?

Hakuna mtu anayejua sababu halisi ya saratani ya matiti. Mara nyingi madaktari hawawezi kueleza kwa nini mwanamke mmoja anapata kansa ya matiti na mwingine hapati. Madaktari wanajua kuwa kugonga,kugusa,kukwaruza au kushikashika au kunyonywa matiti hakusababishi saratani hii. Kansa ya matiti haimbukizwi.
Tafiti zinaonesha kuwa, wanawake fulani wako kwenye hatari zaidi ya kupata saratani ya matiti kuliko wengine. Kuna sababu kadhaa zinazoongeza hatari ya kupata saratani hii.

 • Umri: Hatari ya kupata saratani huongezeka kadri umri unavyoongezeka. Kesi nyingi za saratani ya matiti hutokea kwa wanaweke wenye umri zaidi ya miaka 60. Ni kwa mara chache sana utaukuta ugonjwa huu kabla ya damu ya hedhi kukata
 • Historia binafsi ya kuwa na saratani ya matiti: Mwanamke aliyekuwa na saratani katika titi lake moja, ana hatari kubwa ya kupata kansa katika titi lake jingine.
 • Historia ya familia: Hatari ya mwanamke kupata ugonjwa huu, ni kubwa kama mama, dada, au binti yake alikuwa na saratani ya matiti. Hatari ni kubwa zaidi kama mwanafamilia alipata saratani ya titi kabla ya miaka 40. Kuwa na jamaa wengine wenye saratani ya titi (katika upande wa mama au baba) inaweza pia kuongeza hatari ya kupata saratani..
 • Baadhi ya mabadiliko kwenye matiti: Wanawake wengine wana seli zisizo za kawaida kwenye matiti. Wanawake wenye seli hizi zisizo za kawaida ”hyperplasia atypical na lobular carcinoma in situ ” huwa katika hatari zaidi ya kupata saratani ya matiti.Uchunguzi wa seli za matiti hufanyika kwa kutumia darubini
 • Mabadiliko ya kijenetiki: Mabadiliko katika jeni fulani huongeza hatari ya kupata saratani ya matiti. Jeni hizi ni pamoja na BRCA1, BRCA2, na zingine. Vipimo wakati mwingine, vinaweza kuonesha uwepo wa mabadiliko maalum ya jeni katika familia yenye wanawake wengi wenye saratani ya matiti. Watoa huduma za afya wanaweza kupendekeza njia za kujaribu kupunguza hatari ya saratani hii, au kuhakikisha ugunduzi wa mapema kwa wanawake ambao wana mabadiliko haya katika jeni zao.
 • Historia ya uzazi na hedhi:
  • Kadri mwanamke anavyochelewa kupata mtoto wa kwanza ,ndivyo na hatari yake ya kupata saratani ya matiti inavyoongezeka.
  • Wanawake waliopata hedhi yao ya kwanza (waliovuja ungo) kabla ya umri wa miaka 12 wako kwenye hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti.
  • Wanawake ambao damu ya hedhi ilikata baada ya umri wa miaka 55 wako kwenye hatari zaidi ya kupata saratani ya matiti.
  • Wanawake ambao hawajawahi kuzaa mtoto, wako kwenye hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti.
  • Wanawake wanaotumia tiba ya homoni yenye estrojeni na progestin, baada ya damu kukata (menopausal hormone) wako kwenye hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti.
  • Tafiti nyingi sana zimefanyika na hazijapata kama kuna uhusiano wa saratani ya matiti na utoaji wa mimba (arbotion) au mimba kutoka (misscarriage).
 • Asili: Saratani ya matiti mara nyingi inawapata wanawake wa kizungu kuliko wa Afrika,Latina,au Asia.
 • Tiba ya mionzi kifuani: Wanawake ambao walipata tiba ya mionzi kwenye kifua kabla ya umri wa miaka 30 wako kwenye hatari zaidi ya kupata saratani ya matiti. Tafiti zinaonesha kuwa mwanamke anayepata tiba ya mionzi katika umri mdogo sana huongeza maradufu uwezekano wa kupata saratani ya matiti hapo baadae.
 • Unene au kitambi baada ya damu ya hedhi kukata: Uwezekano wa kupata kansa ya matiti baada ya damu ya hedhi kukata (menopause) huongezeka zaidi kama mwanamke ni mnene sana au ana kitambi.
 • Ukosefu wa mazoezi: Wanawake ambao hafanyi mazoezi katika kipindi chote cha maisha yao, huongeza hatari ya kupata saratani ya matiti. Kufanya mazoezi husaidia kupunguza hatari kwa kuzuia unene na kitambi.
 • Unywaji wa pombe: Tafiti zinaonesha kuwa, kwa kadri mwanamke anavyokunywa pombe,ndivyo na hatari ya kupata saratani ya matiti inavyoongezeka.

kansa ya matitiUkiwa na saratani ya matiti ni wakati gani utafute matibabu haraka?

Mwone mtoa huduma ya afya, kuhusu mabadiliko kwenye matiti kama:

 • Una uvimbe/donge ndani/karibu na titi au kwapa la mkono wako
 • Tishu ngumu ndani au karibu na titi au kwapa la mkono wako
 • Kuna majimaji yanatoka kwenye chuchu
 • Kuna maumivu kwenye chuchu
 • Chuchu imerudi ndani kwenye titi
 • Unawashwa ngozi, kuna mabadiliko kwenye ngozi kama vile wekundu, kukakamaa na kudumbukia kwa ngozi
 • Kuna mabadiliko ya ukubwa na umbo la titi

 Utambuzi wa saratani ya matiti

Kama una dalili zinazoashiria kuwa una saratani ya matiti, daktari wako atalazimika kugundua kama dalili hizo zimesababishwa na saratani au sababu nyingine. Daktari atahitaji kujua historia yako binafsi na ya familia yako. Anaweza pia kukufanya uchunguzi wa mwili.
Daktari anaweza kuagiza ufanye mammogram au kipimo kingine cha picha .Vipimo hivi hupiga picha tishu za ndani ya titi. Baada ya vipimo, daktari wako anaweza kuamua kama unahitaji vipimo vingine au la. Daktari pia anaweza kupendekeza urudi hospitalini siku nyingine kwa ajili ya kufuatilia hali yako. Au huenda ukaagiza ufanyae biopsy kuangalia  kama kuna seli za kansa.

 • Uchunguzi wa matiti; Mtoa huduma ya afya atabonyabonya titi ili kuhisi kama kuna uvimbe wowote ndani yake. Kama una uvimbe,daktari atataka kujua ukubwa,umbo na texture ya uvimbe. Daktari ataangalia pia kama uvimbe unaweza kusogezwa kiurahisi. Uvimbe unaosababishwa na kansa na usiosababishwa na kansa unatofautiana. Mara nyingi,uvimbe laini,nyororo,mviringo na unaoweza kusogezwa kwa urahisi hautokani na kansa. Uvimbe mgumu, wenye umbo lisilo la kawaida,ambao umejishikiza kabisa ndani ya tishu za titi (hauwezi kusogezwa) unaweza kuwa saratani.
 • Diagnostic Mammogram; Hiki ni kipimo kinachotumia mionzi (x-ray) kupiga picha ya matiti. Madaktari hutumia kipimo hiki kuchunguza maeneo ya matiti yanayotia wasiwasi, kama vile uvimbe, maumivu, kukakamaa, kutokwa majimaji kwenye chuchu, au mabadiliko ya ukubwa na umbo la matiti. Kipimo hiki kinapiga picha za kina na nzuri zaidi kuliko zinazopigwa na screening mammograms.
 • Ultrasound; Kifaa cha ultrasound hutuma mawimbi ya sauti ambayo watu hawawezi kuyasikia. Mawimbi hayo hurudishwa kama mwangwi baada ya kukutana na tishu za ndani ya mwili. Kompyuta hutumia mwangwi huo kuunda picha. Daktari anaweza kuiona picha hiyo kwenye kompyuta. Picha itaonesha kama kuna uvimbe, na kama upo, ukoje?. Baada ya kipimo, daktari anaweza kuhifadhi picha hiyo kwa video au kuchapisha.
 • Magnetic Resonance Imaging; MRI scan hutumia nguvu ya sumaku kuunda picha kwenye kompyuta. MRI hupiga picha za kina za tishu za matiti. MRI inaweza kutumika sambamba na mammogram.
 • Biopsy; Majimaji au tishu huchukuliwa kutoka kwenye titi ili kusaidia kujua kama kuna kansa. Madaktari wanaweza kuchukua tishu kutoka kwenye titi kwa njia tofauti tofauti:
 • Fine-needle aspiration: Daktari hutumia sindano nyembamba kuchukua majimaji kutoka kwenye uvimbe. Mwanapatholojia huchunguza majimaji hayo kwa darubini ili kuangalia kama kuna seli za saratani.
 • Core biopsy: Daktari hutumia sindano nene ili kuchukua tishu kwenye matiti. Mwanapatholojia huichunguza tishu hiyo kuona kama kuna seli za kansa. Utaratibu huu kwa jina jingine huitwa needle biopsy.
 • Surgical biopsy: Daktari hupasua titi na kuchukua sampuli ya tishu, kisha mwanapatholojia huichunguza kuona kama kuna seli za saratani.
 • Incisional biopsy: daktari hukata kipande kidogo cha uvimbe kwa ajili ya kukipima.
 • Excisional biopsy: daktari hukata na kuondoa uvimbe wote na kisha kuupeleka maabara kwa ajili ya uchunguzi.

saratani ya matitiUchaguzi wa matibabu wa kansa ya matiti

Kuna aina tofauti tofauti za matibabu kwa wagonjwa wa saratani ya matiti. Lakini kuna aina kuu nne zinazotumiwa:

 • Upasuaji :Wagonjwa wengi wenye saratani ya matiti hufanyiwa upasuaji ili kuondoa kansa. Baadhi ya tezi za limfu (lymph nodes) kwenye kwapa huondolewa na kuchunguzwa kwa darubini pia,ili kuona kama zina seli za kansa.

Upasuaji unaonusuru titi (breast-conserving surgery) – ni upasuaji unaoondoa kansa bila kuondoa titi lote

 • Lumpectomy: Upasuaji hufanyika kuondoa uvimbe pekee na sehemu ndogo ya tishu inayouzunguka.
 • Partial mastectomy: Upasuaji hufanyika kuondoa sehemu ya titi yenye kansa na kubakiza sehemu isiyo na kansa.

Kwa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa kunusuru matiti,tezi za limfu za kwenye kwapa huondolewa pia kwa ajili ya uchunguzi.
Aina nyingine za upasuaji ni pamoja na:

 • Simple mastectomy: Huu ni upasuaji unaofanyika kuondoa titi lote lenye kansa. Baadhi ya tezi za limfu kwenye kwapa zinaweza kuondolewa pia kwa ajili ya uchunguzi.
 • Modified radical mastectomy: Huu ni upasuaji unaofanyika kuondoa titi lote lenye kansa, tezi nyingi za limfu zilizo kwapani, kifuniko cha misuli ya kifua na baadhi ya misuli ya kifua.
 • Radical mastectomy: Huu ni upasuaji unaofanyika kuondoa titi lote lenye kansa, misuli yote ya kifua iliyo chini ya titi na tezi zote za limfu zilizo kwapani.

Hata kama daktari ataondoa saratani yote inayoonekana wakati wa upasuaji, wagonjwa wengine wanaweza kupewa tiba ya mionzi, tibakemikali (chemotherapy), au tiba ya homoni baada ya upasuaji ili kuua seli yoyote ya saratani iliyobakia.
Kama matiti ya mgonjwa yataondolewa ,daktari anaweza kuweka mpango wa kumtengenezea mgonjwa matiti mapya (reconstruction). Daktari anaweza kufanya hivyo kwa kutumia tishu za mgonjwa kutoka maeneo mengine au kwa kutumia silicone/saline implants.

 • Tiba ya mionzi: Tiba hii hutumia nguvu ya mionzi ya x-rays kuua seli za saratani au kuzuia zisiendelee kukua. Kuna aina mbili za tiba ya mionzi.
  • Tiba ya mionzi ya nje (External radiation therapy) – hutumia mashine iliyowekwa nje ya mwili na kuelekeza mionzi kwenye saratani.
  • Tiba ya mionzi ya ndani (Internal radiation therapy) – Vifaa mbalimbali, kama vile sindano, mbegu, waya au mipira yenye dutu inayotoa mionzi, huingizwa ndani ya mwili na kuwekwa karibu kabisa na eneo ilipo saratani.

Njia inayotumika kutoa mionzi hutegemea ni aina gani ya kansa na iko katika hatua gani.

 • Tibakemikali: Ni aina ya matibabu ya kansa ambayo hutumia madawa ili kuzuia ukuaji wa seli za kansa au kuziua.
 • Unapokunywa au kuchomwa dawa kwenye mishipa, huingia kwenye mzunguko wako wa damu na kuzifikia seli zote za kansa kote mwilini (systemic chemotherapy).
 • Lakini dawa ikichomwa moja kwa moja kwenye uti wa mgongo, kiungo au eneo lolote la uwazi kama tumbo, dawa huathiri hasa seli za saratani katika eneo hilo (Regional chemotherapy).

Njia inayotumika kutoa tibakemikali hutegemea aina na hatua (stage) ya saratani.

 • Tiba ya homoni: Ni tiba ya kansa ambayo hupunguza homoni mwilini au kuzuia homoni zisifanye kazi ili kupunguza ukuaji wa seli za saratani. Baadhi ya homoni husababisha kansa fulani kukua kwa haraka zaidi. Homoni ya estrojeni inayotengenezwa na ovari husababisha kansa ya matiti kukua haraka zaidi. Tiba ya homoni hutolewa ili kupunguza uzalishwaji wa estrojeni.

Tamoxifen mara nyingi hutolewa kwa wagonjwa wenye hatua za mwanzo za saratani ya matiti na wale walio na saratani ya matiti iliyoenea kwenda maeneo mengine ya mwili. Kwa sababu Tamoxifen huathiri seli mwilini kote, inaweza kuongeza hatari ya kupata kansa ya kizazi (endometrial cancer). Wanawake wanaotumia tamaoxifen wanapaswa kufanyiwa uchunguzi wa mwili angalau mara moja kwa mwaka

Dawa za kuepuka unapokuwa na saratani ya matiti

Kwa wanaume wenye saratani ya matiti wanapaswa kuepuka kutumia dawa zifuatazo:

 • Androderm
 • Oxandrolone

Kama we ni mwanaume na utambuliwa kuwa una saratani ya matiti, shauriana na daktari kabla ya kuanza au kuacha kutumia dawa yoyote.

Magonjwa yenye dalili zinazofanana na kansa ya matiti

 • Mkusanyiko wa mafutamafuta (lipoma)
 • uvimbe uliojaa maji (Cyst)
 • Jipu kifuani

Nini cha kutarajia unapokuwa na kansa ya matiti?

 

Matatizo yanayoweza kutokea ukiwa na saratani ya matiti

Unaweza kupata madhara au matatizo kutokana na matibabu ya saratani. Kwa mfano, tiba ya mionzi inaweza kusababisha matiti na maeneo ya karibu kuvimba na kuuma kwa muda.
Kuvimba (lymphedema) kunaweza kuanza wiki 6 hadi 8 baada ya upasuaji au baada ya tiba ya mionzi.
Kunaweza pia kuanza polepole baada ya matibabu yako ya kansa kumalizika. Unaweza usione dalili miezi 18 hadi 24 baada ya matibabu. Wakati mwingine inaweza kuchukua miaka mingi kujitokeza.
Muulize daktari kuhusu madhara unayoweza kupata wakati wa matibabu.

Kuzuia kansa ya matiti

Sababu zifuatazo zinaweza kupunguza hatari ya kupata saratani ya matiti:

 • Mazoezi: Kufanya mazoezi kwa angalau masaa 4 kwa wiki kunasaidia kupunguza homoni mwilini na kupunguza hatari ya kupata saratani ya matiti.
 • Estrojeni: Kupungua kiwango cha homoni ya estrogen mwilini husaidia kuzuia saratani ya matiti.

Hali zifuatazo zinapunguza homoni ya estrojeni mwilini:

 • Mimba: Viwango vya estrojeni hupungua wakati wa ujauzito. Hatari ya kupata saratani ya matiti inaonekana kupungua zaidi kwa wananwake waliozaa mtoto wa kwanza kabla ya umri wa miaka 20.
 • Kunyonyesha: Viwango vya estrogen hubaki chini wakati mwanamke anaponyesha.
 • Kuondoa ovari: Ovari hutengeneza estrojeni. Kuondoa ovari moja au zote mbili hupunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha estrojeni. Pia, kuna madawa yanaweza kupunguza kiwango cha estrojeni kinachotengenezwa na ovari.
 • Kuchelewa kuvunja ungo: Kuanza kupata hedhi katika umri wa miaka 14 au zaidi kunapunguza uwezekano wa kupata kansa ya matiti.
 • Damu ya hedhi kuwahi kukata: Mwanamke anapopata hedhi kwa miaka michache tu, uwezekano wa kupata saratani ya matiti hupungua. Hedhi inapokatika mapema (early menopause) estrojeni hupungua pia.
 • Madawa:Madawa kama Tamoxifen na Raloxifene yaliyo kwenye kundi la antiestrogen, hupunguza kiwango cha estrojeni mwilini na kupunguza hatari ya saratani ya matiti. Wanawake walio katika hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti hutumia dawa hizi kupunguza uwezekano wa kupata saratani ya matiti.

Kabla haujatumia dawa hizi ongea na daktari wako kuhusu madhara mabaya ya dawa hizi. Japo Tamoxifen inaweza kukukinga na saratani ya matiti, inaweza pia kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya mji wa mimba, kiharusi, mtoto wa jicho na matatizo mengine.

 • Kuondoa matiti (prophylactic mastectomy): Baadhi ya wanawake walio kwenye hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti, huamua kufanyiwa upasuaji ili kuondoa matiti kabla hayajapata kansa yoyote. Ni muhimu kuwa kabla mwanamke hajafanya uamzi huu wa kuondoa matiti, achunguze na kuambiwa kuhusu chaguzi zingine zilizopo za kuzuia saratani. Kwa wanawake wengine, baada ya kufanyiwa upasuaji na kuyaondoa matiti, hughubikwa na woga na wasiwasi mwingi kuhusu mwonekano wao na Msongo wa mawazo.

Vyanzo

  http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/breastcancer.html

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi