SARATANI YA NJIA YA HAJA KUBWA

SARATANI YA NJIA YA HAJA KUBWA

 • October 23, 2020
 • 0 Likes
 • 416 Views
 • 0 Comments

Maelezo ya jumla

Kansa ya njia ya haja kubwa ni kansa kwenye mfumo wa kumeng’enya chakula. Mkundu ni sehemu ya mfumo wa kumeng’enya chakula ,inayoruhusu kinyesi kutoka nje. Imeundwa kwa aina tofauti za seli, na kila aina inaweza kuwa na kansa. Squamous cell carcinoma ndio aina ya saratani ya njia ya haja kubwa inayowapata watu wengi zaidi kuliko zingine. Dalili hujumuisha kutokwa na damu, maumivu, uvimbe, kuwashwa na kutoa uchafu kwenye njia ya haja kubwa . Uchaguzi wa matibabu ni pamoja na upasuaji, tiba ya mionzi, tibakemikali, au muunganiko wa njia hizo. Uchaguzi wa tiba yako utategemea kama saratani yako imeenea, hatua iliyofikia, ukubwa na eneo ilipo.

Je, nini dalili za kansa ya njia ya haja kubwa?

Mwanzoni kansa ya njia ya haja kubwa inapoanza haina dalili yoyote. Kansa inapokua kubwa, watu wenye saratani ya njia ya haja kubwa huanza kupata dalili. Bawasiri (hemorrhoids) au matatizo mengine ya kiafya yanaweza pia kusababisha dalili hizi. Ni daktari pekee anayeweza kusema/kutofautisha kwa uhakika. Mtu yoyote mwenye dalili hizi anapaswa kumwambia daktari ili matatizo yatambuliwe na matibabu kuanza mapema iwezekanavyo.

 • Kutokwa na damu kwenye njia ya haja kubwa
 • Mabadiliko katika tabia ya tumbo au mabadiliko katika ukubwa wa kinyesi
 • Maumivu kwenye njia ya haja kubwa au chini ya kitovu
 • Kuwashwa au kutokwa uchafu kwenye njia ya haja kubwa
 • Uvimbe kwenye njia ya haja kubwa

Nani yuko kwenye hatari zaidi?

Tafiti zimegundua mambo kadhaa ambayo yanaweza kuongeza hatari ya kupata kansa ya njia ya haja kubwa. Katika miaka ya hivi karibuni, wanasayansi wanaelezea kuwa maambukizi ya Human papillomavirus (HPV)  ni sababu kuu ya kansa ya njia ya haja kubwa. Maambukizi ya HPV na mambo mengine yanayoongeza hatari yanaweza kufanya kazi kwa pamoja kuongeza hatari zaidi.

 • Human papillomavirus (HPV): Virusi hawa wanapokua kwenye njia ya haja kubwa, wanaweza kusababisha kutokea kwa dutu (warts),ambazo huhusishwa na kansa ya njia ya haja kubwa. Virusi hivi vya HPV huenezwa kwa njia ya ngono, hasa kufanya ngono kinyume na maumbile.
 • Kuwa na washirika wengi wa ngono
 • Ngono kinyume na maumbile (anal sex)
 • Nasuri/fistula kwenye njia ya haja kubwa.
 • Kudhoofika kwa mfumo wa kinga: Maambukizi ya virusi vinavyosababisha UKIMWI au kutumia madawa yanayosababisha kudhoofika kwa mfumo wa kingamwili, huongeza hatari ya kupata kansa ya njia ya haja kubwa.
 • Jinsia: Data za tafiti mabalimbali zinaonesha wanawake wana hatari kubwa kuliko wanaume.
 • Umri: Kama vile saratani nyingine za mfumo wa kumeng’enya chakula, watu walio na miaka 50 au zaidi.
 • Uvutaji wa sigara: Kama kansa nyingine, uvutaji wa sigara pia huongeza hatari ya kansa ya njia ya haja kubwa.

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Mwone mtoa huduma wa afya kama una dalili za kansa ya njia ya haja kubwa. Kama mtu ataona dalili zifuatazo, atafute huduma ya matibabu haraka iwezekanavyo:

 • Maumivu makali sana ya tumbo, tumbo kuongezeka ukubwa na kufunga choo: Kuziba kwa utumbo mkubwa ndio sababu ya kuwepo dalili hizi kwa mtu mwenye kansa ya njia ya haja kubwa. Hii ni matokeo ya ukuaji wa uvimbe kwenye ukuta wa rektamu. Upasuaji utafanyika kwa haraka.
 • Kupata kinyesi chenye damu : Hii ni matokeo ya saratani kuvamia mishipa ya damu ya kwenye kuta za rektamu na mkundu. Kupotea kwa damu nyingi kunaweza kusababisha mshtuko na kifo. Unahitaji kwenda hospitali haraka iwezekanavyo.

Utambuzi

Kama magonjwa mengine ya saratani, madaktari wanahitaji kutumia vipimo vingi ili kuchunguza kama kansa yako imeenea kwenda sehemu zingine za mwili. Kwa aina nyingi za saratani, biopsy (kuchukua sampuli ya sehemu iliyoathirika na kuipima) ni njia bora ya kufanya utambuzi wa uhakika wa kansa. Ikiwa biopsy haiwezekani, vipimo vingine vya picha vinapendekezwa kama computed tomography (CT) scan, Magnetic resonance imaging (MRI) au Positron emission tomography (PET) scan

 • Digital rectal examination (DRE): Hiki ndicho kipimo cha msingi na muhimu zaidi katika uchunguzi wa kansa ya njia ya haja kubwa. Katika kipimo hiki, daktari huingiza kidole kwenye njia yako ya haja kubwa ili kuangalia kama kuna uvimbe, kutokwa damu au shida nyingine yoyote.
 • Anoscopy, proctoscopy na biopsy: Baada ya uchunguzi wa rektamu (DRE), ikiwa daktari atahisi eneo lolote linalotia mashaka, ataingiza bomba nyembamba yenye kamera kwenye njia ya haja kubwa, ili kuichunguza sehemu hiyo, na kama akiliona tatizo atachukua sampuli ndogo ya eneo hilo (biopsy) kwa ajili ya uchunguzi. Sampuli hizi zitachunguzwa chini ya darubini ili kutambua kama kuna saratani au la. Utahitaji dakika 20 hadi 30 kwa ajili ya kipimo hiki.
 • Computed tomography (CT) scan: Kipimo hiki hutumia kompyuta na nguvu ya mionzi kupiga picha inayoweza kuonesha vyema kuta za rektamu,hii humpa fursa daktari kufanya uchunguzi wa kina kuhusu ukubwa wa kansa.
 • Magnetic resonance imaging (MRI): Kipimo hiki hutumia kompyuta na nguvu ya sumaku kupicha inayoweza kuonesha vyema kuta za rektamu. Kipimo hiki ni tofauti na CT scan na hupiga picha za kina zaidi
 • Positron emission tomography (PET) scan: Wakati wa kufanya kipimo hiki, kiasi kidogo cha miali nunurishi (radioactive) huingizwa kwenye damu na hufyonzwa na viungo na tishu zote mwilini. Miali hii nunurishi hutoa mionzi ambayo inaweza kurekodiwa na kuzalisha picha.
 • Complete blood count (CBC): Kipimo hiki hufanyika kutambua kama kuna maambukizi au upungufu wa damu.
 • Uchunguzi wa kinyesi

Uchaguzi wa matibabu

Wagonjwa wenye kansa ya njia ya haja kubwa wana chaguo nyingi za matibabu. Machaguo ni upasuaji, tiba ya mionzi, tibakemikali (chemotherapy ), au njia mchanganyiko. Aina ya matibabu ya kansa, hutegemea aina ya saratani, na ni kwa kiasi gani imeenea.

 • Kabla ya kuanza kwa matibabu, waulize madaktari kuhusu madhara ya matibabu na kwa kiasi gani yanaweza kubadili mfumo wako wa maisha. Hii ni kwa sababu matibabu ya saratani mara nyingi huharibu seli na tishu zenye afya pia, madhara ni ya kawaida. Madhara hayafanani kwa kila mtu, na yanaweza kubadilika badilika.
 • Wagonjwa walio na kansa ya njia ya haja kubwa ilio katika hatua za mwanzo,kansa ambayo haijaenea kwenda sehemu nyingine za mwili, inaweza kutibiwa kwa upasuaji.
 • Kwa wagonjwa wenye kansa ilio katika hatua za mwisho, kansa iliyoenea kwenda sehemu nyingine za mwili ,wanapaswa kutibiwa kwa tibakemikali na tiba ya mionzi pekee au baada ya upasuaji.
 • Ikiwa mgonjwa hawezi kupewa tibakemikali au tiba ya mionzi, upasuaji unaweza kupendekezwa. Upasuaji pia unaweza kupendekezwa ikiwa kansa itabakia baada ya matibabu ya awali au kurudi baada ya matibabu kumalizika.

Magonjwa yenye dalili zinazofanana

Matatizo mengine ya afya yanaweza kusababisha dalili zinazofanana na zile za kansa ya njia ya haja kubwa. Mwone daktari ili kuthibitisha ugonjwa wako mapema iwezekanavyo. Magonjwa yenye dalili sawa ni pamoja na:

Kuzuia

Kwa sababu ,sababu ya saratani ya njia ya haja kubwa haijulikani na baadhi ya watu wenye kansa ya njia ya haja kubwa hawana sababu inayojulikana, hakuna njia ya uhakika ya kuzuia kansa hii. Takwimu za kiepidemolojia zinaonyesha kufanya mambo yafuatayo kunaweza kupunguza hatari ya kupata kansa hii.

 • Epuka maambukizi ya HPV, hasa kwa kuepuka kuwa na washirika wengi wa ngono na kuepuka ngono nzembe kinyume na maumbile
 • Pata chanjo ya HPV (hili linafanyika kwa washichana wa shule katika nchi kadhaa za Afrika mashariki)
 • Acha kuvuta sigara

Nini cha kutarajia ?

Matarajio kwa kansa ya njia ya haja kubwa yanatofautiana sana. yanategemea mambo yafuatayo:

 • Ukubwa wa saratani
 • Eneo kansa ilipo kwenye njia ya haja kubwa
 • Kama kansa imeenea kwenda mbali
 • Kama mgonjwa ana Virusi vya ukimwi
 • Kama saratani imebakia baada ya matibabu ya awali au imerudia tena

Vyanzo

 • Share:

Leave Your Comment