Magonjwa ya wanawake

SARATANI YA SHINGO YA MLANGO WA KIZAZI:Dalili,matibabu..

Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko

Maelezo ya jumla

Saratani ya shingo ya mlango wa kizazi (cervical cancer) ni aina ya saratani ambayo huathiri tishu za shingo ya kizazi (shingo ya kizazi ni kiungo kinachounganisha uke na mji wa mimba. Ni saratani ambayo kwa kawaida hukua taratibu sana na kwa kificho, inaweza isisababishe dalili yoyote mwanzoni, lakini inaweza kugunduliwa kwa kufanya kipimo kinachoitwa ”Pap test” (wakati wa kipimo hiki, Seli hukwanguliwa kwa utaratibu maalumu toka kwenye mlango wa kizazi na kisha huchunguzwa kwa darubini).
Ugonjwa huanzia sehemu ya juu ya kizazi na kisha huvamia tishu za ndani na zinauzozunguka mji wa mimba. Seli za kansa zinaweza kuenea kupitia mishipa ya damu au mishipa ya limfu na kusambaa kwenda kwenye tishu zingine za mwili. Seli hizi za saratani zinazosafiri kwenye mishipa ya damu zinaweza kugota kwenye tishu za maeneo mengine na kisha kukua na kusababisha kansa inayoweza kuharibu tishu za mahala hapo.

Je, nini dalili za saratani ya shingo ya mlango wa kizazi?

Kwa kawaida, mwanzoni ugonjwa wa kansa ya kizazi inaweza isisababishe dalili yoyote. Saratani (uvimbe) inapokua kubwa, wanawake wanaweza kuona mojawapo au zaidi ya dalili hizi:

  • Kutokwa na damu isivyo kawaida ukeni
  • Kutokwa na damu katikati ya vipindi vya hedhi (kutokwa na damu tarehe ambazo sio za hedhi)
  • Kutokwa na damu baada ya tendo la ngono, baada ya kujiingiza vidole au baada ya kufanyiwa uchunguzi na dakitari.
  • Vipindi vya hedhi vinavyodumu kwa muda mrefu sana na damu nyingi isivyo kawaida
  • Kuanza kuvuja damu tena baada ya damu kukata uzeeni ”menopause”
  • Kuongezeka kwa ute ute/maji maji ukeni
  • Maumivu ya nyonga
  • Maumivu wakati wa ngono

Maambukizi au matatizo mengine ya kiafya yanaweza kusababisha dalili hizi pia. Daktari tu ndiye anaweza kutofautisha kwa uhakika. Mwanamke mwenye dalili yoyote iliyo hapo juu anapaswa kumwambia daktari ili tatizo lake litambuliwe na apewe matibabu yanayositahili haraka iwezekanavyo.

Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata saratani ya shingo ya mlango wa kizazi?

Tafiti zimegundua mambo kadhaa yanayoweza kuongeza hatari ya kupata saratani ya kizazi, maambukizi ya virusi vya HPV (human papillomavirus) ndiyo sababu kuu ya saratani ya mlango wa kizazi. Maambukizi ya virusi vya HPV na sababu nyingine huongeza hatari mara dufu ya kupata saratani ya shingo ya mlango wa kizazi.

  • Maambukizi ya HPV:
    • HPV ni kundi la virusi vinavyoweza kuathiri mlango wa kizazi . Maambukizi ya HPV ambayo hayaponi yanaweza kusababisha saratani ya kizazi kwa baadhi ya wanawake. Maambukizi ya virusi vya HPV ndio sababu ya karibu kesi zote za kansa ya mlango wa kizazi. Virusi hivi huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja mpaka mwingine kwa njia ya ngono
    • Watu wazima wengi huambukizwa virusi vya HPV kwa wakati fulani katika maisha yao, lakini maambukizi mengi hupona tu yenyewe bila matibabu. Aina fulani za virusi vya HPV zinaweza kusababisha mabadiliko katika seli za mlango wa kizazi. Kama mabadiliko haya yakigundulika mapema, saratani ya kizazi inaweza kuzuiwa kwa kuondoa au kuua seli zilizobadilika kabla hazijawa seli za saratani.
    • Chanjo kwa wanawake wenye umri wa miaka 9 hadi 26 inayotolewa huwalinda dhidi ya aina mbili za maambukizi ya HPV yanayosababisha saratani ya kizazi.
  • Wanawake wasiofanya mara kwa mara kipimo cha Pap test:
    • Saratani ya kizazi huwapata kwa wingi zaidi wanawake wasiofanya kipimo cha pap test mara kwa mara. Kipimo cha pap test huwasaidia madaktari kuzigundua mapema seli zilizobadilika kabla hazijawa seli za saratani. Kwa kuua au kuondoa seli hizi zilizobadilika husaidia kuzuia saratani ya shingo ya kizazi.
  • Kuvuta sigara:
    • Kwa wanawake wenye maambukizi ya virusi vya HPV, uvutaji wa sigara huongeza hatari ya kupata saratani ya kizazi angalau kwa kidogo.
  • Kudhoofika kwa mfumo wa Kinga mwili:
    • Maambukizi ya VVU (virusi vinaosababisha UKIMWI) au kutumia madawa yanayosababisha kudhoofika kwa mfumo wa kinga ya mwili huongeza hatari ya kupata saratani ya mlango wa kizazi.
  • Historia ya ngono:
    • Wanawake waliowahi kushiriki ngono na wapenzi wengi tofauti tofauti wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata saratani ya mlango wa kizazi. Vivyo hivyo pia, kwa mwanamke aliyefanya ngono na mwanamume aliyewahi kufanya ngono na wanawake wengi. Katika kesi zote mbili, hatari ya kupata saratani ya kizazi ni kubwa kwa sababu, wanawake hawa wote wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa virusi vya HPV.
  • Kutumia vidonge vya kupanga uzazi kwa muda mrefu:
    • Kutumia dawa za kupanga uzazi kwa muda mrefu (miaka 5 au zaidi) kunaweza kuongeza hatari ya kupata kansa ya kizazi kwa wanawake walio na maambukizi ya virusi vya HPV. Hata hivyo, hatari hupungua haraka wanawake hao wanapoacha kutumia dawa za uzazi wa mpango.
  • Kuzaa watoto wengi:
    • Tafiti zinaonesha kuwa kuzaa watoto wengi (5 au zaidi) kunaweza kuongeza hatari ya kupata kansa ya kizazi kwa wanawake walio na maambukizi ya virusi vya HPV.

saratani ya shingo ya mlango wa kizaziWakati gani utafute matibabu ya haraka?

  • Unapaswa kuanza kufanya kipimo cha Pap test mara kwa mara unapofikia umri wa miaka 21, au ndani ya miaka mitatu mara baada ya kuanza kufanya ngono.
  • Vipimo vya Pap ni mojawapo ya vipimo vya uchunguzi vya saratani vinavyoaminika na vinavyopatikana kwa urahisi, pia vinaweza kusaidia kutambua hali nyingine ambazo zinahitaji matibabu, kama vile maambukizi au uvimbe.
  • Mbali na kipimo cha Pap; Kipimo kikuu cha saratani ya mlango wa kizazi, ni cha kupima virusi vya HPV, Kinachoweza kutumika kwa utambuzi kwa wanawake wenye umri wa miaka 30 na zaidi, au wanawake wa umri wowote wenye matokeo yasiyoeleweka ya Pap test.
  • Kama una miaka 30 au zaidi, na matokeo ya vipimo vyako ni ya kawaida, uwezekano wako wa kupata saratani ya mlango wa kizazi kwa miaka michache ijayo ni mdogo sana. Kwa sababu hiyo, daktari anaweza kukuambia kwamba hauhitaji kufanya kipimo kingine cha pap kwa angalau miaka mitatu ijayo.
  • Ni muhimu pia kuendelea kufanya kipimo cha Pap mara kwa mara, hata kama unadhani umekua mzee sana na hauna mpango/ hauwezi kupata mtoto, au haufanyi ngono tena.

Utambuzi wa saratani ya shingo ya mlango wa kizazi

Madaktari wanashauri wanawake kufanya kipimo cha pap test mara kwa mara ili kupunguza hatari ya kupata saratani ya mlango wa kizazi. Kipimo cha Pap test (ambacho kwa wakati mwingine huitwa Pap smear au cervical smear) ni kipimo rahisi kinachotumika kuchunguza seli za kizazi. Vipimo vya Pap vinaweza kutambua saratani ya kizazi au seli zisizo za kawaida ambazo zinaweza kusababisha saratani ya kizazi.
Kutambua na kutibu seli zisizo za kawaida kwenye mlango wa uzazi kunaweza kuzuia kansa nyingi za kizazi. Kipimo cha Pap kinaweza kusaidia kutambua kansa mapema, wakati ambao tiba huwa na ufanisi zaidi. Kwa wanawake wengi, kipimo cha Pap hakisababishi maumivu. Kipimo hiki kinafanyika kwenye ofisi ya daktari au kwenye kliniki.
Daktari au nesi hukwangua sampuli kutoka sehemu ya ndani ya mlango wa uzazi. Maabara huchunguza sampuli hiyo na kuangalia kama kuna mabadiliko. Mara nyingi, seli zenye mabadiliko zinazopatikana wakati wa pap test hazisababishi kansa. Sampuli hiyo hiyo inaweza kupimwa kuangalia kama kuna virusi vya HPV.
Ikiwa umepata majibu ya Pap test au majibu ya HPV yasisiyo ya kawaida, daktari anaweza kupendekeza ufanye vipimo vingine:

Colposcopy: Daktari hutumia colposcope kuangalia kizazi. Colposcope ni kifaa maalumu

kinachotumia mwanga mkali na lenzi ya kukuzia vitu (magnifying lens) ili kuona tishu kwa urahisi. Kifaa hiki hakiingizwi ukeni. Colposcopy kawaida hufanyika ofisini kwa daktari au kliniki.

  • Biopsy: Daktari hutia ganzi kwenye mlango wa kizazi na kisha kukata nyama ndogo (sampuli) kwa ajili ya vipimo. Mwanapatholojia huchunguza tishu hizi kwa darubini ili kuangalia kama kuna mabadiliko kwenye seli za mlango wa kizazi.
  • Kuchukua tishu kutoka kwenye kizazi kunaweza kusababisha kutokwa na damu au majimaji mengine. Eneo lenyewe hupona haraka. Wanawake wengine huhisi maumivu kama wanayopata wakati wa hedhi. Daktari anaweza kupendekeza dawa kadhaa za kukupunguzia maumivu.

Uchaguzi wa matibabu

  • Wanawake walio na saratani ya kizazi wana machaguo kadhaa ya matibabu. Machaguo hayo ni pamoja na upasuaji, tiba ya mionzi, tibakemikali (chemotherapy), au mchanganyiko.
  • Uchaguzi wa matibabu hutegemea hasa ukubwa wa uvimbe na kama saratani imeenea.
  • Uchaguzi wa matibabu pia unaweza kutegemea kama mwanamke ungependa kuwa mjamzito hapo baadae. Daktari anaweza kukueleza kuhusu kila chaguo la matibabu, matokeo ya kila mmoja, na madhara yanayoweza kuletwa na kila chaguo. Wewe na daktari mnaweza kuzungumza na kukubaliana mpango wa matibabu utakao kufaa wewe binafsi.
  • Daktari anaweza kukupa rufaa uonane na daktari bingwa au unaweza kuomba uonane na daktari bingwa anayehusika na kutibu saratani za wanawake. Wataalamu hao ni pamoja na gynecologists, gynecologic oncologist, medical oncologists, surgeons na radiation oncologists.
  • Kabla ya matibabu kuanza, waulize madaktari kuhusu madhara yanayoweza kuletwa na dawa na ni kwa kiasi gani matibabu yatavuruga utaratibu wako wa maisha ya kila siku. Kwa sababu matibabu ya kansa huharibu seli za mwili, madhara yatokanayo na madawa ni ya kawaida. Madhara yatokanayo na madawa yanatofautiana kwa kila mgonjwa na yanaweza kubadilika badilika kwa kila kipindi cha matibabu.

Nini cha kutarajia?

  • Ni muhimu kujitunza vyema kwa kula na kufanya mazoezi kwa kadri unavyoweza, hasa katika kipindi kigumu cha matibabu. Unahitaji kula vyema ili kuwa na nguvu mwilini.
  • Kula vizuri kunaweza kukusaidia kujisikia vizuri na kuwa na nguvu zaidi. Hata hivyo, huenda usihisi hamu ya kula wakati wa matibabu au baada ya matibabu. Unaweza kujihisi vibaya na kuwa mchovu. Unaweza kuhisi kuwa chakula sio kitamu kama kilivyokuwa hapo mwanzo. Aidha, madhara yatokanayo na matibabu (kama vile kukosa hamu ya kula, kichefuchefu, kutapika, au vidonda vya mdomo) yanaweza kusababisha kula vizuri kuwa mtihani. Daktari anaweza kupendekeza njia kadhaa za kukabiliana na matatizo ya namna hii.
  • Tafiti zinaonesha kuwa, watu wenye saratani hujihisi vizuri wakiendelea kufanya kazi zao za kila siku. Wakitembea, wakijihusisha na yoga, kuogelea na shughuli zingine hupata nguvu mwilini. Mazoezi yanaweza kupunguza kichefuchefu, maumivu na taabu za matibabu kwa kiasi. Husaidia pia kupunguza msongo. Ongea na daktari kabla haujaanza kufanya aina yoyote ya mazoezi utakayochagua.
  • Utahitaji kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara baada ya matibabu ya saratani ya shingo ya kizazi. Uchunguzi wa mara kwa mara utahakikisha kuwa mabadiliko yoyote yatakayotokea kwenye afya yako yanagunduliwa mapema na kushughulikiwa. Kama kuna tatizo lolote kwenye uchunguzi wowote ongea na daktari wako. Daktari atachunguza kama saratani inarejea tena hata kama ulipona kabisa. Wakati mwingine ugonjwa hurudi tena baada ya seli za saratani kubakia mahala fulani mwilini baada ya matibabu. Uchunguzi wa mara kwa mara hujumuisha uchunguzi wa mwili, pap tests na ekisirei ya kifua.

Matatizo yanayoweza kutokea

  • Aina fulani za saratani ya kizazi haziitikii vyema matibabu tuliyonayo kwa sasa.
  • Kansa inaweza kurudi baada ya matibabu.
  • Wanawake ambao huchagua aina nyingine za matibabu badala ya kuondolewa kizazi kama walivyopendekeza madaktari ili waweze kupata watoto baadae, huwa na uwezekano mkubwa wa kansa kujirudia tena baada ya matibabu.
  • Upasuaji na mionzi inaweza kusababisha matatizo ya tumbo, kibofu na hata wakati mwingine matatizo wakati wa ngono.

Kuzuia

  • Epuka kuambukizwa virusi vya HPV
    • Epuka kuanza ngono katika umri mdogo
    • Epuka kuwa na washirika wengi wa ngono
    • Epuka kuwa na mpenzi ambaye amekuwa na washirika wengi wa ngono
    • Epuka kufanya ngono na wanaume wasiotahiriwa
  • Kuacha ngono: Kusubiri na kuanza kufanya ngono baadae unapokuwa mtu mzima kunasaidia kupunguza uwezekano wa kuambukizwa virusi vya HPV.
  • Tumia kondomu: Kondomu hukulinda na maambukizi ya virusi vya HPV.
  • Epuka kuvuta sigara: Tafiti zinaonesha kuacha kuvuta sigara hupunguza hatari ya kupata saratani ya shingo ya kizazi.
  • Kupata chanjo: Chanjo zinaweza kuwalinda wanawake kutokana na maambukizi ya HPV.
  • Uchunguzi wa mara kwa mara wa kizazi
    • Kipimo cha Pap
    • Matibabu ya seli zenye mabadiliko kabla hazijawa saratani

Vyanzo

Leave feedback about this

  • Quality
  • Price
  • Service

PROS

+
Add Field

CONS

+
Add Field
Choose Image
Choose Video
X