SHINIKIZO KUBWA LA DAMU: Mlo/Chakula/Ulaji unaofaa

Shinikizo la juu la damu

Sababu hasa za shinikizo la juu la damu/ presha/ shinikizo kubwa la damu kwa sehemu kubwa hazijulikani. Hata hivyo shinikizo la damu hubadilika mara kwa mara kutegemeana na shughuli mtu anayofanya, hali ya joto, chakula alichokula, hali ya msongo wa mawazo, ukiwa umelala au kusimama na hata matumizi ya baadhi ya dawa.

Shinikizo kubwa la damu linapotokea mwilini

shinikizo kubwa la damu

Shinikizo kubwa la damu hutokea pale panapokuwa na ongezeko la nguvu ya msukumo wa damu katika mishipa inayochukua damu kutoka kwenye moyo kwenda kwenye viungo na tishu mwilini. Ukubwa wa shinikizo hilo la damu unategemea wingi na nguvu ya msukumo wa damu kutoka kwenye moyo na ukubwa wa mishipa inayopeleka damu mwilini.

Kiwango kinachoashiria tatizo la shinikizo la damu

Blood pressure machine (sphignomanometer) hutumika kupima shinikizo la damu na kipimo kinachochukuliwa kuwa ni kawaida ni 120/80 mmHg au chini yake. Kiwango kinapokuwa 140/90mmHg au zaidi hali hiyo huwa ni shinikizo kubwa la damu. Ikumbukwe panaweza kuwepo tofauti kati ya mtu na mtu.

Viashiria hatarishi vya shinikizo la juu la damu

Watu wenye umri wa miaka 45 au zaidi wako kwenye hatari zaidi ya kupata shinikizo kubwa la damu kutokana na mabadiliko yanayotokea katika mishipa yao ya damu. Pia mafuta, lehemu au madini ya chokaa yakizidi mwilini huwa na tabia ya kujikusanya katika kuta za ndani za mishipa ya damu kidogo kidogo na kusababisha kuwa na upana mdogo na hivyo kupunguza uwezo wake wa kutanuka. Hali hii huchangia kwa kiasi kikubwa mtu kupata shinikizo kubwa la damu Mambo yanayoashiria uwezekano wa kupata shinikizo kubwa la damu ni pamoja na:

 • Historia ya shinikizo kubwa la damu katika familia; ­
 • Umri wa zaidi ya miaka 40; ­
 • Jinsi ya kiume (huwapata wanaume zaidi kuliko wanawake); ­
 • Uzito uliozidi kiasi; ­
 • Msongo wa mawazo;
 • Matatizo mengine ya kiafya mwilini, kama magonjwa ya figo, matatizo ya mishipa ya damu, magonjwa ya moyo, matatizo ya vichocheo mwilini, kisukari au saratani; ­
 • Matumizi ya baadhi ya dawa; na ­
 • Kutokufuata mtindo bora wa maisha.

Tatizo la shinikizo kubwa la damu pia linaweza kujitokeza wakati wa ujauzito.

Dalili za shinikizo kubwa la damupresha

Kwa kawaida hakuna dalili za wazi zinazojitokeza pale ambapo mtu ana shinikizo kubwa la damu. Kipimo maalum ndiyo huweza kuonesha tatizo hili. Mara nyingi shinikizo kubwa la damu hutambulika mtu anapokuwa na tatizo jingine la kiafya. Kwa bahati mbaya watu wengi huishi na tatizo hili kwa muda mrefu bila kufahamu kwani hakuna dalili zilizo bayana. Hali hii humuweka mtu katika hatari ya kupata ugonjwa wa moyo hivyo ni muhimu kuwa na tabia ya kupima shinikizo la damu mara kwa mara.

Shinikizo la damu likiwa katika kiwango cha juu sana dalili zifuatazo huweza kujitokeza:

Ulaji unaoshauriwa kwa mtu mwenye shinikizo kubwa la damu

Pamoja na ulaji unaoshauriwa ni muhimu sana mgonjwa kutumia dawa kama atakavyoelekezwa na daktari. Mara nyingi wagonjwa wa shinikizo kubwa la damu huacha kutumia dawa wanapohisi nafuu. Hii si sahihi kwani huongeza uwezekano wa kupata madhara. Inashauriwa:

 • Kuepuka vyakula vyenye chumvi nyingi, ikiwa ni pamoja na vile vilivyosindikwa kwa chumvi; ­
 • Kutumia viungo mbalimbali kuongeza ladha ya chakula (tangawizi, vitunguu saumu, madalasini); ­
 • Kuepuka vyakula vyenye mafuta na sukari nyingi; ­
 • Kula mlo kamili angalau mara tatu kwa siku ukizingatia kula vyakula vya aina mbalimbali; ­
 • Kula matunda na mbogamboga kiasi cha kutosha katika kila mlo; na ­
 • Kutumia nafaka zisizokobolewa na vyakula vya jamii ya kunde kwa wingi.

Ni muhimu kuwa na uzito unaoshauriwa kulingana na urefu na kama uzito umezidi hakikisha anapungua. Fanya mazoezi angalau nusu saa kila siku na fuata ulaji unaofaa.

Mbinu za kupunguza uwezekano wa kupata shinikizo kubwa la damu

shinikizo la juu la damu

Ili kupunguza uwezekano wa kupata shinikizo kubwa la damu ni muhimu kufuata mtindo bora wa maisha ukizingatia:

 • Kuepuka vyakula vyenye mafuta mengi;
 • sukari na chumvi nyingi; ­
 • Kuepuka mafuta yenye asili ya wanyama; ­
 • Kuepuka vyakula vyenye lehemu kwa kiasi kikubwa; ­
 • Kupunguza kiasi cha nyama unachokula hasa nyama nyekundu; ­
 • Kuepuka kuwa na uzito uliozidi; ­
 • Kuepuka matumizi ya pombe, sigara na tumbaku; ­
 • Kudhibiti msongo wa mawazo; na ­
 • Kufanya mazoezi kila siku.

Shinikizo kubwa la damu wakati wa ujauzito

Mjamzito mwenye shinikizo kubwa la damu ni muhimu kuhudhuria kliniki mara kwa mara kufuatilia hali yake; kutumia dawa za kupunguza shinikizo la damu kama atakavyoelekezwa na mtaalam wa afya; kufuatilia kwa makini ongezeko la uzito wa mwili na kuepuka utumiaji wa pombe na sigara. Mjamzito afuate ulaji unaoshauriwa kwa watu wenye shinikizo kubwa la damu, bila kusahau ongezeko la mahitaji ya virutubishi kutokana na hali ya kuwa mjamzito

Vyanzo

https://www.tfnc.go.tz/publications/9

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi