SHINIKIZO LA JUU LA DAMU :Dalili na Matibabu

Maelezo ya jumla

Shinikizo la juu la damu, ni hali ya muda mrefu ambapo shinikizo la damu katika mishipa huwa juu saana. Presha (Shinikizo la damu) ni nguvu ya damu inaposukumwa/kukandamizwa dhidi ya kuta za mishipa wakati wa kutiririka. Kila wakati moyo unapopiga, unasukuma damu ndani ya mishipa.

Shinikizo la damu ni kubwa wakati moyo unapiga na kusukuma damu, hii inaitwa shinikizo la sistoli. Wakati moyo unapopumzika, kati ya mapigo ya moyo, wakati moyo anapokua hausukumi damu, shinikizo la damu hushuka. Hii inaitwa shinikizo la diastoli.

Mtu anachukuliwa kuwa na shinikizo la juu la damu anapokuwa na shinikizo la damu ≥ 140/90 mmHg. Shinikizo la damu kati ya 120/80 mmHg hadi 139/89 mmHg ni “shinikizo la awali. Shinikizo la awali sio ugonjwa; ila watu hawa wenye shinikizo la awali wana hatari zaidi ya kupata shinikizo la juu la damu. Shinikizo la damu la kawaida ni sawa au chini ya 120/80mmHg.

Kwa wagonjwa wa kisukari au ugonjwa wa figo, utafiti umeonesha kwamba shinikizo ≥130/80 mmHg linapaswa kuchukuliwa kuwa la juu na linahitaji matibabu zaidi.

Nini dalili za shinikizo la juu la damu?

Mara nyingi, hakuna dalili. Kwa wagonjwa wengi, ongezeko la shinikizo hugunduliwa wakati wa uchunguzi wa mwili wanapotembelea kituo cha afya wakiwa na tatizo lingine kabisa.

Kwa sababu hakuna dalili, watu wanaweza kupata magonjwa ya moyo na matatizo ya figo yatokanayo na shinikizo bila kujua kuwa wana ugonjwa huu.
Ikiwa una maumivu makali ya kichwa, kichefuchefu au kutapika, kuchanganyikiwa, matatizo ya macho, au kutokwa damu puani unaweza kuwa una aina kali na hatari ya shinikizo la juu la damu.

Nini husababisha shinikizo la damu?

Shinikizo la juu la damu limeganyika katika makundi mawili:

 • Lisilo na chanzo mahususi kinachofahamika ”Essential hypertension”
 • Lenye chanzo kinachofahamika ”Secondary hypertension

Shinikizo la juu la damu lisilo na chanzo mahususi kinachofahamika.

Kupanda kwa presha kusiko na chanzo mahususi kinachofahamika, huathiri 90-95% ya wagonjwa wa shinikizo la damu. Ingawa hakuna chanzo cha moja kwa moja kinachosababisha shinikizo la aina hii, kuna sababu kadhaa zinazochukuliwa kuwa muhimu ili kutokea kwake.

 • Mtindo mbaya wa maisha
 • Uzito mkubwa na kitambi husababisha 80-85% ya ongezeko la presha isilo na chanzo maalumu.
 • Ulaji wa chumvi nyingi
 • Unywaji wa pombe uliopitiliza
 • Upungufu wa Vitamini D
 • Kuwepo kwa historia ya shinikizo la damu katika
 • Magonjwa ya kimaumbile
 • Matatizo ya kimetaboliki – mwili huwa na usugu kwa insulini kwa sababu ya uzito mkubwa/ kitambi na huwa na ongezeko la shinikizo la damu, kisukari, na kiwango kikubwa cha mafuta kwenye damu.                                                                

Shinikizo la juu la damu lenye chanzo kinachofahamik

Presha ya juu yenye chanzo kinachofahamika hutibiwa kwa kutibu sababu/chanzo kinachosababisha kupanda kwake. Kupanda kwa shinikizo la damu husababishwa na kutokuwepo kwa usawa thabiti wa mfumo wa homoni, ambao hudhibiti kiasi cha maji katika damu na kazi moyo unayoakiwa kufanya. Kuna hali nyingi zinazosababisha shinikizo la damu kuongezeka, kama vile:

 • Kuongezeka kwa shinikizo kunakosababishwa na matatizo ya figo: Mishipa ya damu inayoingiza na kutoa damu katika figo huwa myembamba kwa sababu mbalimbali na kusababisha shinikizo mwilini kuongezeka. Makovu baada ya jeraha au saratani kwenye figo yanaweza kusababisha presha kuongezeka kwa sababu moyo hutumia nguvu nyingi zaidi kusukuma damu kupitia mishipa hiyo.
 • Pheochromocytoma: Ni tatizo linalotokana na uvimbe katika tezi ya ndongo inayoitwa ”adrenal”. Uvimbe katika tezi hii husababisha kuzalishwa kwa wingi homoni za ”norepinephrine” na ”epinephrine” ambazo kwa kawaida husababisha kipeny cha mishipa ya damu kupungua. Kwa sababu ya kipenyo cha mishipa kupungua, moyo hutumia nguvu nyingi zaidi kusukuma damu na kupelekea kupanda kwa la presha.
 • Hyperaldosteronism: Ni hali inayotokea baada ya tezi za ”adrenal” kutengeneza kwa wingi kupita kiasi homoni ya aldosterone, homoni hii inapokuwa nyingi mwilini hubakiza kiasi kikubwa cha chumvichumvi katika damu kwa kupunguza kiasi kinachotolewa katika mkojo. Kwa sababu ya chumvichumvi nyingi kubaki katika damu, mwili hubakiza maji mengi mwilini pia ili kuisawazisha. Hali hii husababisha kuongezeka kwa ujazo wa damu na shinikizo.
 • Cushing’s syndrome: Hii ni hali inayosababishwa na tezi za ”adrenal” za mwili kutengeneza homoni aina ya ”cortisol” kwa wingi kupita kiasi. ”Cortisol” ni homoni inayosaidia kuleta uwiano wa shinikizo la damu, inapokuwepo kwa wingi katika damu inasababisha shinikizo la damu kuongezeka.
 • Hyperparathyroidism: Hii ni hali inayotokana na kutolewa kwa wingi homoni ya ”parathyroid” (homoni hii hutengenezwa na tezi nne zilizopo shingoni zinazoitwa ”parathyroid”) huongeza shinikizo la damu.
 • Hyperthyroidism: Ni hali inayotokana na kutengenezwa kwa wingi kupita kiasi homoni ya ”thyroid”, inayotengenezwa na tezi dundumio iliyopo shingoni na huongeza shinikizo la damu.
 • Ugonjwa sugu wa figo: Ugonjwa sugu wa figo huharibu tishu za figo, na unaweza kuharibu mtiririko wa damu katika figo na kusababisha ongezeko la presha.
 • Dawa: Kuna dawa baadhi ukizitumia zinaweza kuongeza shinikizo la damu, kwa mfano, dawa za kupanga uzazi, steroids, NSAIDs,n.k.
 • Mimba: Sababu ya kuongezeka shinikizo kipindi cha ujauzito haifahamiki vyema.
 • White coat hypertension: hili ni shinikizo la juu damu linalotokea katika mazingira ya kituo cha afya pekee, labda kutokana na wasiwasi ambao watu wengine hupata wakati wa kutembelea kliniki ya afya.
 • Perioperative hypertension: Shinikizo la juu la damu linalotokea muda mchache kabla ya kuingia katika chumba cha upasuaji

Nani yuko kwenye hatari zaidi?

Sababu/Mambo yafuatayo huongeza hatari ya kupata shinikizo la juu la damu lisilo na chanzo mahususi kinachofahamika

Kuna mjadala kuwa, shinikizo la juu la damu huwapata zaidi watu weusi ikilinganishwa na wazungu. Kulingana na tafiti kadhaa ,hili linaonekana kuwa kweli japo sababu haifahamiki vyema bado. Kwa sasa wataalamu wa afya wanadhani sababu zifuatazo zinachangia sana watu weusi kupata shinikizo la damu.;

 • Ulaji wa mlo wenye chumvi na mafuta mengi.
 • Hali ya chini ya kiuchumi na kijamii

Utambuzi kuwa una shinikizo la juu la damu

Mtoa huduma wako wa afya atakupima shinikizo la damu mara kadhaa kabla ya kugundua kama presha imepanda. Ni kawaida kwa shinikizo la damu kuwa tofauti kulingana na wakati wa siku. Kwa watu wazima wengi, tunasema kuwa wana shinikizo la juu la damu kama presha iko ≥ 130/80 au 140/90 mmHg.

Vipimo vya shinikizo la damu vilivyochukuliwa nyumbani vinaweza kuwa bora kuliko vile vinavyochukuliwa katika ofisi ya daktari. kwa hiyo hakikisha unapata kifaa bora na  kinachostahili kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Mwambie mtoa huduma wa afya akufundishe namna ya kupima shinikizo la damu kwa usahihi ukiwa nyumbani. Daktari pia atakufanyia uchunguzi wa mwili ili kuangalia ishara zinazoashiria kama umepata ugonjwa wa moyo,kuharibika macho na mabadiliko mengine mwilini.

Ni wakati gani utafute huduma ya matibabu  haraka?

Mtu anapaswa kupimwa shinikizo la damu angalau mara moja kila baada ya miaka miwili ikiwa shinikizo la damu ni ≤ 120/80 na kila mwaka ikiwa shinikizo la damu linaanzia 120/80 -139 /89mmHg.

Ikiwa shinikizo la damu ni juu ya 120/80mmHg na una maumivu makali ya kichwa, unapata shida kuona, kizunguzungu, upotevu wa ufahamu, maumivu ya kifua, udhaifu wa mguu au mkono, kichefuchefu, kutapika na uchovu, unapaswa kutafuta huduma ya matibabu haraka.
Ongezeko la shinikizo huhusishwa na aina mbalimbali za dalili lakini kwa ujumla husababisha matatizo ya moyo, ubongo, macho / kuona, figo, mishipa na udhaifu wa mkono / mguu.

Uchaguzi wa matibabu

Shinikizo la juu la damu ni ugonjwa ambao hauwezi kuponywa kabisa lakini unaweza kudhibitiwa. Hii inamaanisha shinikizo linaweza kudhibitiwa na kubaki ndani ya mipaka fulani inayokubalika. Mgonjwa anapaswa kutumia dawa siku zote na kufuata maelekezo ya daktari ili kudhibiti shinikizo. Mgonjwa atakapoacha kufuata maelekezo ya daktari shinikizo la damu huongezeka tena na linaweza kuleta madhara.
Shinikizo la damu linaweza kudhibitiwa kwa njia zifuatazo;

 • Kubadili mfumo wa maisha.
 • Kutumia dawa.

Kubadili mfumo wa maisha.                                                                                                                                                                     

Miongozo kadhaa imependekezwa kuhusu mfumo bora wa maisha unaoweza kudhibiti au kukukinga dhidi ya shinikizo la juu la damu.hatua zifuatazo zinafaa:

 • Zingatia kupima mara kwa mara shinikizo la damu. Japo kuna vifaa mbalimbali vya kupima shinikizo la damu, ni bora zaidi ukipimwa shinikizo la damu na daktari au mtoa huduma wa afya mwenye uzoefu.
 • Kudumisha mlo wenye chumvi kidogo kadri iwezekanavyo (Punguza sodiamu katika mlo hadi chini ya 1,500 mg kwa siku). Watu wazima wanapaswa kujaribu kupunguza ulaji wa chumvi na isizidi 2,300 mg kwa siku ambayo ni sawa na kijiko kimoja cha chumvi.
 • Epuka mafuta mengi kwenye chakula na jaribu kuepuka vyakula vya kukaanga.
 • Ongeza matunda na mboga mboga katika mlo.
 • Mazoezi ya mara kwa mara kama ilivyopendekezwa na daktari.
 • Epuka mlo wenye mafuta mengi.
 • Kunywa kwa kiasi kahawa au chai. Kunywa kiasi kikubwa kinaweza kuongeza shinikizo.
 • Kula vyakula ambavyo havijakobolewa na vyenye nyuzinyuzi kwa wingi.
 • Punguza unywaji wa pombe.

Kutumia dawa

Zifuatazo ni dawa zinazotolewa kwa ajili ya kudhibiti shinikizo la juu la damu:

 • Diuretics: Hizi ni dawa za kupunguza maji kwenye damu, dawa hizi husaidia kupunguza ujazo wa damu na hivyo kupunguza shinikizo.
 • Beta blockers: Dawa hizi hupunguza kiwango cha mapigo ya moyo pamoja na shinikizo la damu.
 • ACE inhibitors: Hizi hupunguza kiwango cha homoni ya ”angiotensin” inayofanya kazi pamoja na Renin kuongeza shinikizo la damu.
 • Calcium Channel Blockers: Hizi huzuia kalsiamu kuingia kwenye mishipa ya moyo na kuizuia mishipa ya moyo kunywea, hivyo kupunguza shinikizo la damu.
 • Angiotensin II blockers: Dawa hizi hufanya kazi moja kwa moja ya kupunguza viwango vya ”Angiotensin” mwilini (”Angiotensin” husababisha kunywea kwa mishipa). Homoni hii inapopungua mwilini mishipa hupanuka na kupunguza shinikizo
 • Alpha Blockers: Dawa hizi hufanya kazi ya kupunguza kunywea kwa mishipa ya damu kunakosababisha kuongezeka kwa shinikizo la damu.
 • Vasodilators -Hizi hupanua mishipa moja kwa moja ili kupunguza shinikizo na hutumiwa zaidi katika hali maalum kama mimba.

Madawa ya kuepuka ukiwa na presha.

Wagonjwa wanaogundulika kuwa na ongezeko la shinikizo la juu, wanapaswa kuepuka kutumia dawa zifuatazo:

 • Abciximab
 • Alteplase
 • Reteplase
 • Tenecteplase
 • Urokinase

Ikiwa imegundulika  kuwa una ongezeko la shinikizo la damu, wasiliana na daktari kabla ya kuanza au kuacha dawa yoyote.
Wagonjwa wanaogundulika kuwa wana shinikizo la juu la damu ambalo halijadhibitiwa vyema wanapaswa kuepuka kutumia dawa zifuatazo:

 • Almotriptan
 • Epoetin alfa
 • Eptifibatide
 • Methoxy polyethilini glycol-epoetin beta
 • Phentermine
 • Phenylephrine
 • Rizatriptan
 • Zolmitriptan

Ikiwa umegundulika kuwa una shinikizo la juu la damu ambalo halijadhibitiwa vyema, wasiliana na daktari kabla ya kuanza au kuacha kutumia dawa yoyote.

Nitarajie nini nikigundua kuwa nina shinikizo la juu la damu?.

Shinikizo la juu haliwezi kuponywa kabisa ila linaweza kudhibitiwa na kuwa katika viwango vya kawaida. Kama mgonjwa atafuata maelekezo ya kitabibu aliyopewa na mtindo bora wa maisha kama vile; kufanya mazoezi, kula mlo ulio bora na wenye afya, kuepuka kula mlo wenye chumvi na mafuta mengi, kuacha uvutaji wa sigara, kupunguza/kuacha kabisa unywaji wa pombe na kupunguza msongo wa mawazo.
Shinikizo la damu lisipodhibitiwa vyema linaweza kusababisha matatizo mbalimbali kama ilivyoelezwa hapo chini. kwa hiyo ni muhimu mgonjwa kuzingatia matibabu kama yalivyoainishwa na daktari.

Matatizo yatokanayo na shinikizo la juu la damu!

Shinikizo la juu la damu linaweza kusababisha matatizo kadhaa ya viungo.-

 • Matatizo kwenye moyo: Shinikizo la juu lisilodhibitiwa vyema linaweza kusababisha Mshituko wa moyo au Moyo kushindwa kufanya kazi kabisa.
 • Matatizo kwenye Ubongo– Mgonjwa mwenye shinikizo lisilodhibitiwa vyema, yupo kwenye hatari kubwa ya kupata Kiharusi na matatizo mengine ya ubongo. Matatizo haya huwa na dalili kama kuchanganyikiwa, degedege na kichwa kuuma. Kuvuja damu kwenye ubongo husababisha kichefuchefu, kutapika, mwanga wa kawaida kuumiza macho na kupoteza fahamu.
 • Matatizo ya macho: Presha inaweza kuharibu macho, uharibifu huu wa macho hupunguza uwezo wa kuona na hatimaye kusababisha upofu.
 • Matatizo ya figo: Shinikizo la damu huharibu figo na kusababisha ugonjwa wa figo na hata kupelekea figo kushindwa kufanya kazi kabisa. Mgonjwa huanza kukojoa sana wakati wa usiku, mkojo unaweza kuwa na damu, kuwa na mkojo wenye povu kutokana na kuwepo kwa protini inayopotea kwenye mkojo na viwango visivyo vya kawaida vya sodiamu, kalsiamu na potasiamu.

vyanzo

http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/ency/article/000468.htm

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi