Magonjwa ya ndani ya mwili

SONONA:Sababu,dalili,matibabu,kuzuia

kuomboleza

Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko

Maelezo ya jumla

Sonona (Depression) ni hali ya kuhisi huzuni, kushuka moyo na kukosa furaha. Wengi wetu hujihisi hivi kwa wakati mmoja au mwingine kwa muda mfupi. Ugonjwa wa sonona ni tatizo la kihisia, mgonjwa huhisi huzuni mwingi na hasira. Mafadhaiko wa aina hii huvuruga mfumo wa maisha ya kila siku wa mgonjwa.

Je! Nini dalili za sonona?

 • Dalili ni pamoja na:
  • Hali ya msononeko au hasira wakati wote
  • Kupoteza hamu ya kufanya shughuli au mambo aliyokuwa akiyafurahia.
  • Hapati usingizi au analala sana
  • Mabadiliko makubwa ya hamu ya chakula, mara nyingi mgonjwa hupungua au kuongezeka uzito
  • Uchovu na kukosa nguvu
  • Mgonjwa hujihisi kutokuwa na thamani yoyote, hujichukia, na hujihisi mwenye hatia
  • Hupata ugumu kuzingatia mambo
  • Huwa mnyonge au mwenye papara
  • Hapendi kufanya lolote na huepuka kufanya shughuli za kawaida
  • Hujihisi kukata tamaa na bila msaada
  • Hupata mawazo ya kifo au kujiua mara kwa mara
  • Kutokujiamini ni swala la kawaida kwa mgonjwa wa sonona. Anaweza pia kuwa na hasira za ghafla na hukosa raha hata anapofanya mambo yanayopasa kumfurahisha mtu, hii ni pamoja na ngono.
  • Watoto wenye sonona huenda wasiwe na dalili sawa na watu wazima. Angalia mabadiliko kwenye kazi za shule, usingizi, na tabia. Kama unashuku mwanao ana ugonjwa huu, ni muhimu kuongea na mtoa huduma wa afya.

sononaAina za sonona

 • Aina kuu ni pamoja na:
  • Sonona yenye dalili nyingi (major depression): Ili kutambuliwa na aina hii, ni lazima uwe na dalili tano au zaidi ya zilizotajwa hapo juu kwa angalau wiki 2. Aina hii kuu inaweza kuendelea kwa muda wa miezi 6 au zaidi kama haitatibiwa.
  • Sonona yenye dalili chache (minor depression) – Mgonjwa huwa na dalili zisizozidi tano kwa angalau wiki mbili. Aina hii haitofautiani sana na yenye dalili nyingi, isipokuwa kwa idadi ya dalili (huwa na dalili mbili mpaka nne).
  • Sonona yenye dalili zisizo kawaida (atypical depression): Aina hii huwapata zaidi ya theluthi moja ya wagonjwa walio na sonona. Dalili hujumuisha kula na kulala sana isivyo kawaida. Unaweza kujihisi kama umebebeshwa mzigo mzito.
 • Aina nyingine ni:
  • Sonona inayotokea baada ya kujifungua (postpartum depression): Wanawake wengi hujihisi wenye huzuni baada ya kujifungua, lakini mtu mwanamke mwenye sonona ya kweli huwa na dalili kali na hujumuisha dalili za sonona yenye dalili nyingi.
  • Sonona inayotokea kabla ya hedhi (premenstrual dysphoric disorder ): Dalili huanza wiki 1 kabla ya hedhi na kutoweka baada ya kupata hedhi.
  • Kwa baadhi ya wagonjwa dalili za sonona hupokezana na zile za wazimu, hii hujulikana kama ”manic depression” au ”bipolar disorder”.
  • Sonona huwapata zaidi wanawake kuliko wanaume. Hii inaweza kuwa kwa sababu wanawake hutafuta msaada zaidi kuliko wanaume.
  • Pia, sonona huwapata zaidi vijana walio kwenye balehe.

Sonona husababishwa na?

 • Baadhi ya watu hurithi jeni zinazoongeza hatari ya kuwa na ugonjwa huu. Tabia unazojifunza nyumbani pia zinaweza kuchangia watu wa familia fulani kuwa na sonona. Watu wanaozaliwa na jeni hizi huanza kuwa na ugonjwa huubaada ya tukio la kuhuzunisha linaloongeza msongo wa mawazo.
 • Mambo/sababu nyingi zinaweza kusababisha ugonjwa huu, ikiwa ni pamoja na:
 • Hali za kitabibu, magonjwa au matibabu kama vile:
  • Aina fulani za kansa
  • Maumivu ya muda mrefu
  • Kukosa usingizi
  • Kutumia dawa aina ya ”steroid”
  • Kama tezi dundumio haifanyi kazi vyema
 • Matukio yanayoongeza msongo kwenye maisha, kama vile:
  • Unyanyaswaji au kutelekezwa
  • Kuvunjika kwa mahusiano ya kimapenzi
  • Aina fulani za kansa
  • Kifo cha jamaa au rafiki
  • Talaka, hii ni pamoja na talaka kwa mzazi
  • Kufeli mitihani au kurudia darasa
  • Kuugua kwa mwanafamilia
  • Kupoteza kazi
  • Maumivu ya muda mrefu
  • Kutengwa na jamii (hasa kwa wazee)

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

 • Ukihisi au ukiwa na mawazo ya kujiua, mwambie mtu uliyekaribu yako au nenda katika kituo cha afya kilicho karibu yako.
 • Mwone daktari kama:
  • Unasikia sauti ambazo hazipo au watu wengine hawazisikii
  • Unalia lia kila mara bila sababu yoyote
  • Sonona imeathiri uwezo wako wa kufanya kazi, kusoma shule, au kuishi vyema na familia kwa zaidi ya wiki 2
  • Una dalili tatu au zaidi za sonona
  • Kama unadhani moja ya dawa unazotumia zinakusababishia sonona. USIBADILI au USIACHE kutumia dawa yoyote bila kuzungumza na daktari
  • Unafikiri unapaswa kupunguza kunywa pombe, mwanafamilia au rafiki amekuomba kupunguza unywaji wa pombe, unahisi hatia kuhusu kiasi cha pombe unachokunywa, au unakunywa pombe asubuhi sana

Utambuzi

 • Mhudumu wa afya atagundua ukali wa ugonjwa wako (sonona inaweza kuwa kadri, wastani, au kali) na kutafuta sababu kwa:
  • Historia ya kiafya
  • Mahojiano ili kutambua afya ya akili
  • Uchunguzi wa kimwili
  • Kama kuna hatari ya wewe kujiua, utapaswa kubaki hospitalini kwa ajili ya matibabu
 • Utaongea na mtoa huduma ya afya kuhusu masuala au matukio yanayoweza kukusababishia shida hii. Daktari anaweza kukuuliza kuhusu:
  • Hali (Mood) yako na dalili nyingine (usingizi, hamu ya chakula, umakini, nguvu)
  • Mambo yanayoongeza msongo maishani na watu wanaokutegemeza
  • Kama umeshawahi kuwa na mawazo ya kukatisha maisha yako
  • Matumizi mabaya ya madawa ya kulevya, pombe, na madawa mengine unayotumia

Uchaguzi wa matibabu

Uchaguzi wa matibabu hutegemea na dalili ulizo nazo , kwa sonona ya kadri, ushauri na kujitunza mwenyewe kunatosha. Lakini kwa watu wenye Sonona ya wastani au kali, tiba yenye ufanisi zaidi ni mchanganyiko wa matumizi ya madawa ya kudhibiti sonona na tiba maongezi ”talk therapy”. Daktari anaweza kuamua kukupeleka kwa mtaalamu wa magonjwa ya akili kama sonona yako ni wastani au kali, au kama matibabu anayokupatia hayasaidii.

Mambo unayoweza kufanya mwenyewe kudhibiti sonona

Kuna baadhi ya mabadiliko kwenye mfumo wa maisha unayoweza kufanya ili kukusaidia unapopitia wakati wa kushuka moyo. Mabadiliko haya yata-support tiba ambayo daktari wakoatakuwa anatoa

 • Unapokuwa umeshuka moyo, hata shughuli ndogo tu zinaonekana ngumu. JARIBU KUWEKA LENGO DOGO, unaloweza kulikamilisha kwa siku kila siku. Kama vile kutembea kuzunguka mtaa wako au kula chakula kizuri asubuhi. Fanya hivyo pia unapojihisi kuwa una matatizo mengi ambayo unashindwa kuyakamilisha. Jaribu kushughulikia tatizo moja baada ya jingine, moja baada ya jingine, kama inawezekana ivuje hiyo shughuli katika vipande vidogo vidogo unavyoweza kuvikamisha kimoja baada ya kingine
 • Kama kwa mara cha unapata mawazo ya kujidhuru au kujihisi huzuni sana, JARIBU KUJIWEKA BUSY na jambo jingine kama vile kusikiliza radio au kuangalia TV, vitu ambavyo havihitaji kuwa makini sana ‘’concentration’’.
 • Jaribu KUEPUKA MAMBO YATAKAYOKUONGEZEA MSONGO. Kama ikiwezekana ahirisha au mpatie mtu mwingine kazi ya kufanya hayo maamuzi magumu. Angalia shughuli unazotaka kufanya, fanya kile ambacho unakiona ni muhimu zaidi na kile ambacho sio muhimu kiweke kwanza
 • USIWEKE MAMBO MOYONI. Utajisikia kufunguliwa kama utamwambia mtu kuhusu hisia zako, hasa rafiki wa karibu au mwanafamilia. Kuzungumza kuhusu tatizo lako haimaanishi kuwa wewe ni mnyonge au haujiwezi, ni jambo la kawaida kuomba msaada.
 • JARIBU KULA mara kwa mara, hata kama haujisikii. Chagua vyakula ambavyo unavifurahia, lakini kumbuka kuchanganya mbogamboga, matunda, mkate, wali, na viazi. Kula kidogo kidogo kama haujisikii kula mlo mkubwa.
 • KUFANYA MAZOEZIyatakusaidia kujisikia poa ‘’relax’’, kupata usingizi mzuri na kupunguza sonona kwa kusababisha ubongo kutoa kemikali ambazo zitasababisha hali yako ‘’mood’’ kuwa nzuri. Kutembea tu au kufanya kazi kwenye bustani kuna faida kubwa. Kila mtu anapaswa kufanya mazoezi, lakini kama unaumwa (mfano kama una maumivu ya viungo au matatizo ya moyo) ni vizuri kumwona daktari wako kabla hujaanza mazoezi.
 • PUNGUZA AU ACHA KUNYWA POMBE, japo kunywa pombe kunaweza kukufanya ukajihisi vizuri kwa muda, lakini ukweli ni kwamba pombe inachangia kwa kiwango kikubwa kuleta sonona na matatizo mengine ya kiafya
 • ACHA KUTUMIA MADAWA YA KULEVYA kama vile bangi au ecstasy; zina madhara ya muda mrefu ambayo yanasababisha sonona
 • Kama unapata shida kusinzia na unashindwa kulala, punguza kiwango cha kahawa unayokunywa na epuka kulala mchana
 • Kama unajihisi misuli yako imekaza na inashindwa kulegea ‘’relax’’, FANYA MAZOEZI YA KUPUMUA NA KULEGEZA MISULI.
 • Kama unaweza, JARIBU KUTAMBUA NINI SABABU YA SONONA yako. Kutambua sababu ya tatizo lako inaweza kukusaidia ukaacha kujisikia mwenye hatia na baada ya muda unaweza kuanza kushughulika na hilo tatizo sababishi

Kuzuia

 • Mfumo wa maisha ulio bora unaweza kusaidia kuzuia ugonjwa huu, na kupunguza uwezekno wa kujirudia. Maongezi tiba na madawa vitakuweshweza usipate sonona tena.
 • Maongezi tiba yanaweza kukusaidia wakati wa huzuni, dhiki, na majonzi.
 • Kuwa karibu na watu wengine ni muhimu ili kuzuia tatizo hili.

Vyanzo

http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/ency/article/003213.htm

  • 1 year ago (Edit)

  Nipo katika hali hiyo najihis kuumbiwa matatizo😭😭

   • 1 year ago

   pole sana. pole sana. ongea na mtu unayemwamini. wakati mwingine kuzungumza na mtu anayekujali kuhusu matatizo yako njia inaanza kuonekana. kila mwandamu anakutana na masaibu yake. ONGEA NA MTU unayemwamini, kiongozi wa dini, baba, mama, rafiki n.k

  • 1 year ago (Edit)

  Napitia changamoto hizo na Sina msaada nifanye nini

Leave feedback about this

 • Quality
 • Price
 • Service

PROS

+
Add Field

CONS

+
Add Field
Choose Image
Choose Video
X