Watoto

TATIZO LA KUHARISHA KWA WATOTO

Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko

Maelezo ya jumla

Yawezekana mwanao amewahi kusumbuka au umewahi kusikia rafiki au ndugu akilalamika kuwa mtoto wake anaharisha na haelewi ni kitu gani anaweza kufanya. Makala hii inalenga kuwa msaada unapokutana na changamoto ya kuharisha kwa watoto.

Kuharisha kwa watoto ni tatizo linasababisha vifo miongoni mwa watoto chini ya miaka mitano. Inakadiriwa kwamba kwa kila watoto 5 wanaofariki , 1 hufa kwa sababu ya kuharisha.

Kuharisha husababisha upotevu wa maji na madini muhimu kutoka katika mwili wa binadamu kupitia kinyesi na kupelekea upungufu wa maji mwilini.

Nini sababu inayopelekea kuharisha???

Kuharisha kunaweza kusababishwa na aina mbalimbali za vimelea, ingawa pia kunaweza kusitokane na maambukizi ya vimelea. Vimelea vinavyosababisha kuharisha ni:

 • Virusi: Virusi vinaongoza katika kusababisha tatizo la kuharisha kwa watoto katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea.
 • Bakteria: Wanasababisha kuharishakuharisha kwa asilimia chache. Kuharisha kunakosababishwa na bakteria husababisha upotevu mdogo wa maji ukilinganishwa na virusi. Mfano wa bakteria wanaoweza kusababisha tatizo hili ni “Campylobacter”, “Salmonella”, “Shigella”, na “Escherichia coli”
 • Parasiti pia husababisha kuhara, lakini kwa ujumla, aina ya kuhara huwa ni sugu na mara nyingi haiambatani na homa, kutapika, na upungufu wa maji mwilini. “Giardia lamblia” na “Cryptosporidium parvum” ni moja ya aina hii za parasiti wanaosababisha kuhara.

Sababu ambazo hazihusiani na maambukizi ya vimelea ni pamoja na:

 • Kula chakula kilichochanganywa na sumu au kumeza sumu
 • Matatizo katika sehemu ya utumbo mwembamba na mnene, na
 • Matatizo ya usagaji, umeng’enyaji au ufyonzwaji wa chakula

Kwa vile sababu kuu ya kuharisha ni kutokana na virusi, tutazungumzia aina kuu ya virusi wanaosababisha kuhara.
Kuna aina takribani 4 wanaojulikana ambao ni “Rotavirus”, “Adenovirus”, “astrovirus” na “norovirus”. Kati ya hawa jamii ya virusi vya Rota ndio huongoza duniani kote katika kueneza na kusababisha kuharisha kwa watoto wachanga na wadogo.
Katika nchi zinazoendelea, “Rotavirus” ndio chanzo kikuu cha vifo vinavyotokana na kuhara miongoni mwa watoto chini ya umri wa miaka 5. “Rotavirus” huathiri wavulana na wasichana kwa uwiano sawa.
Jamii hii ya virusi huenea kwa urahisi sana kutoka kwa mtoto mmoja kwenda kwa mwingine kwa sababu ya usafi duni wa mzazi au mtoto. Ni rahisi mtoto kupata uambukizi wa “rotavirus” iwapo atakula chembechembe za kinyesi zenye vimelea hivi.
Mtu mwenye vimelea hivi anaweza kuambukiza mtu mwingine hata kabla ya dalili kuanza kujionesha au hata siku kadhaa baada ya dalili kujionesha.
Mtu aliyeambukizwa anaweza kutoa idadi kubwa ya vimelea hivi kiasi cha virion 1-10 kwa kila mililita ya kinyesi. Ili kuambukizwa kinahitajika kiasi kidogo tu cha hawa vimelea, takribani miligramu 0.000001. Hivyo ni rahisi kuambukizwa kwa kugusana au kwa kushika au kutumia vifaa vyenye maambukizi ya “rotavirus” .

Dalili na Mwonekano wa mgonjwa baada ya kuharisha

Watoto wanaohara kwa sababu ya virusi vya rota huwa na dalili kuu tatu ambazo ni homa, kutapika na kuharisha. Kwa kawaida kinyesi huwa cha majimaji sana. Tafiti zinaonesha kuwa asilimia kubwa ya watoto wanaolazwa hospitalini kwa tatizo hili, huonesha dalili zote tatu na asilimia chache wanaonesha dalili mbili.
Wakati mwingine kuharisha kunaweza kujitokeza baadaye baada ya kutapika au homa. Joto la mtoto huwa si kali sana ingawa baadhi ya watoto wanaweza kuwa na joto kali linalozidi nyuzi joto 39 za sentigredi.
Kutapika kunaweza kusiwe zaidi ya masaa 24. Vilevile wanaweza kuwa na kuchefuchefu, maumivu ya tumbo, kulia pasipo kutulia akibembelezwa na uchovu.
Vifo husababishwa na upungufu wa maji mwilini. Upungufu wa maji waweza kuambatana na upungufu na kukosekana uwiano wa madini mwilini. Aidha kunaweza kusababisha madhara katika figo na katika mfumo wa neva na kusababisha na mtoto kupoteza fahamu. Inashauriwa kuchunguza kiasi cha maji kilichopotea.

Je, Nini dalili zinazoweza kuonekana kwa mtoto aliyepoteza maji na madini mwilini kutokana na kuharisha?

Dalili za kupoteza maji na madini muhimu kutoka mwilini mwa mtoto kwa sababu ya kuharisha, ni tatu na matibabu yake yanatofautiana kutokana na dalili anazoonesha.

 • Dalili za upungufu / upotevu mkubwa sana wa maji kutoka mwilini
  • Kupoteza fahamu
  • Kushindwa kula na kunywa.
  • Kuwa na macho yaliyolegea na kuingia ndani sana
  • Mushindwa kutoa mkojo kabisa
  • Kushindwa kutoa machozi na mdomo kuwa mkavu sana.
  • Ngozi ukiivuta inarudi taratibu sana
 • Dalili za upungufu / upotevu wa wastani wa maji kutoka mwilini 
  • Macho ya mtoto huingia ndani.
  • Ngozi kurudi taratibu pindi inapovutwa
  • Uchovu au kulia lia tu
  • Kiu kikali na kunywa maji kwa haraka na kuomba maji mara nyingi
  • Mtoto kutoa machozi kidogo sana pindi anapolia
  • Midomo kuwa mikavu na
  • Kupumua kwa haraka kuliko kawaida
 • Dalili kama hakuna upungufu wa maji / upotevu wa kawaida wa maji kutoka mwilini
  • Kuhisi kiu kawaida ya maji
  • Ngozi inayorudi vizuri kwa haraka ikivutwa
  • Uchovu

Unapoona dalili hizi wakati mtoto anaharisha unapaswa kumpeleka haraka kituo cha afya ili kupata ushauri wa wataalamu wa afya.

Uchunguzi

Daktari anaweza kuagiza vipimo vifuatavyo:

 • Kipimo cha choo: hujumuisha pia uchunguzi wa vimelea.
 • Kipimo cha antigeni cha virusi vya rota : ingawa 50% ya majibu yanaweza kuwa si sahihi (false-negative) hasa pale panapokuwa na damu kwenye choo.
 • Kupima kiwango cha sukari mwilini: ili kuhakikisha kuwa sukari haijapungua mwilini kwa sababu baadhi ya dalili zake zinafanana na za upungufu wa maji mwilini
 • Kupima kiwango cha chembechembe nyeupe za damu: Ili kutambua kama kuna maambukizi ya bakteria.
 • Kipimo cha kazi ya figo: ili kuangalia kama figo zinafanya kazi ipasavyo
 • Vipimo vingine: Kutegemea na hali ya mgonjwa, daktari anaweza kuagiza vipimo vingine pia

Matibabu

Ingawa yawezekana mtoto kupona bila hata matibabu, lakini ni jambo muhimu kuchunguza madhara yanayoweza kusababishwa na upungufu wa maji mwilini. Ieleweke kuwa watoto wapo katika hatari kubwa zaidi ya kupungukiwa na maji mwilini kutokana na kuharisha, hivyo basi msingi wa matibabu ni kurudisha kiasi cha maji kilichopotea.
Hali kadhalika, kumpatia mtoto nyongeza ya madini ya zinc yamehusishwa na kupungua kwa makali ya ugonjwa na kupunguza muda wa kuharisha.
“Oral rehydration salt (ORS)” ambayo ni mchanganyiko wenye uwiano mzuri wa chumvi na sukari, ni aina ya tiba inayopendekezwa na Shirika la Afya Duniani kwa ajili ya matibabu. Uwiano uliopo katika ORS huwezesha utumbo wa mtoto kufyonza vizuri maji na madini mengine.
Matibabu ya kuharisha kwa watoto yanaweza kugawanywa katika awamu kuu mbili

 • Kurudisha maji yaliyopotea
 • Kuendelea kuupa mwili maji kwa ajili ya mahitaji ya kila siku

Mlezi au mzazi hushauriwa namna ya kutengeneza mchanganyiko huu wa ORS kulingana na hali ya mtoto. Kwa mama anayenyonyesha, anashauriwa kuendelea kumnyonyesha mtoto mgonjwa huku akimpa mlo wa kawaida wa kila siku.
Ikiwezekana, ni vema pia kuendelea kumpa mtoto maji ya ziada. Kama mtoto akitapika, mzazi/mlezi anashauriwa kusubiri kwa angalau dakika 5-10 kabla ya kuendelea tena kumnywesha kidogo kidogo (kwa mfano, kijiko kila baada ya dakika 2-3).
Watoto walio na hali mbaya na wale waliopoteza zaidi maji hawana budi kupewa maji kwa njia ya mishipa ya damu yaani kuwekewa dripu ya maji.
Kwa vile chanzo kikuu cha kuhara kwa watoto ni maambukizi ya virusi, haishauriwi kutumia antibioyiki kama sehemu ya matibabu. Hata hivyo antibiotiki zinaweza kutumika tu pale ambapo itathibitika kuwa kuharisha kumesababishwa na bakteria.
Dawa za kuzuia kuharisha kama vile “Loperamide” hazishauriwi kwa sababu athari zake ni mbaya zaidi kwa mtoto kuliko faida.

Nawezaje kuzuia mtoto wangu asiharishe???

Unaweza kufanya mambo yafuatayo ili kumkinga mwanao

 • Zingatia usafi wa chakula (wakati wa kupika, kula na kuhifadhi chakula).
 • Nawa mikono kila baada ya kutoka chooni, kabla ya kushika chakula na wakati wa kula.
 • Kuwa makini na watoto wanaoharisha ikiwezekana kuwatenga na wenzao
 • Kuwapatia watoto chanjo. Hii chanjo ya kuzuia kuharisha kwa watoto inatolewa Tanzania mtoto akiwa amefikisha wiki Sita (Mwezi mmoja na nusu) baada ya kuzaliwa na anapewa Tena anapofika wiki kumi toka amezaliwa (miezi miwili na nusu)

Angalia pia: Ratiba ya chanjo za watoto nchini Tanzania

Kumbuka

Unapoona mtoto anaharisha ni vema kuwahi kituo cha afya kwa matibabu sahihi.
Karibu Sana na endelea kufuatilia makala zetu zinahusu afya katika tovuti yetu hii, pia ukiwa na swali au unaitaji msaada wa ushauri waweza pia kuacha comment ay ujumbe wako nasi tupo kukusaidia.

Imeandaliwa na DR.GEKURA MATARO

Vyanzo

https://medlineplus.gov/ency/patientinstructions/000693.htm


  • 2 years ago (Edit)

  Uko sahihi kabisa, endelea kutuokoa ndugu

   • 2 years ago

   Amina, karibu sana

Leave feedback about this

 • Quality
 • Price
 • Service

PROS

+
Add Field

CONS

+
Add Field
Choose Image
Choose Video
X