TAUNI

TAUNI

 • November 22, 2020
 • 0 pendwa
 • 11 Wameona
 • 0 Maoni

Maelezo ya jumla

Tauni (plague) ni ugonjwa wa kuambukiza unaowapata  panya, wanyama fulani na binadamu. Ugonjwa huu husababishwa na bakteria wanaoitwa Yersinia pestis. Bakteria hawa hupatikana katika maeneo mengi duniani. Kuna aina tatu za tauni, tauni inayosababisha mtoki (bubonic), tauni inayosababisha nyumonia (pneumonic) na tauni inayosambaa kwenye damu (septicemic). Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na: homa, maumivu ya kichwa, kuhisi baridi, maumivu ya misuli, kichefuchefu na kutapika. Tauni inayosababisha mtoki husababisha tezi za limfu kuvimba; Tauni inayosababisha nyumonia husababisha matatizo kwenye mapafu; Tauni inayosambaa kwenye damu husababisha kuvuja damu na kuoza kwa tishu za mwili. Watu wanaoishi maeneo ya kijijini, wanaokutana na panya, wako katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa ugonjwa huu. Tauni hutambuliwa kwa ishara, dalili na vipimo vya maabara. Matatizo yanayoweza kutokea ni pamoja na; nyumonia, mshtuko na kifo. Wagonjwa 8-10% hufa hata baada ya matibabu kwa kutumia antibiotiki.

 Je, nini dalili za tauni?

Dalili za tauni hutegemea mgonjwa ameambukizwaje bakteria wanaosababisha tauni. Tauni inaweza kuchukua sura tofauti tofauti.

Tauni inayosababisha mtoki

Dalili huonekana ghafla, siku 2 – 5 baada ya kuambukizwa bakteria, na hujumuisha:

 • Homa ya ghafla
 • Uchovu
 • Maumivu ya kichwa
 • Kuhisi baridi
 • Kukosa nguvu
 • Maumivu ya misuli
 • Degedege
 • Kuuma na kuvimba kwa tezi za limfu (mtoki)
 • Tezi za limfu za kwenye kinena, makwapani shingoni huvimba na kusababisha mtoki kwenye kwapa, kinena au shingoni.
 • Maumivu yanaweza kutokea katika eneo lililoumwa kabla uvimbe haujaonekana

Tauni inayosababisha nyumonia

Dalili huanza ghafla siku 2 – 3 baada ya kuambukizwa, na hujumuisha:

 • Homa
 • Maumivu ya kichwa
 • Kukosa nguvu
 • Nyumonia, yenye dalili kama:
 • Kupata shida kupumua
 • Maumivu ya kifua
 • Kukohoa

Tauni inayosambaa kwenye damu

Aina hii inaweza kusababisha kifo hata kabla ya dalili zake kuonekana. Dalili hujumuisha:

 • Homa
 • Kuhisi baridi
 • Kichefuchefu
 • Kutapika
 • Kukosa nguvu kabisa
 • Maumivu ya tumbo
 • Kuvuja damu kweny ngozi na viungo vingine (kwa sababu ya damu kushidwa kuganda)
 • Kuhara
 • Kuoza kwa tishu, kama vile vidole vya mikono, vidole vya miguu na pua

Je, Tauni husababishwa na nini?

Tauni husababishwa na bakteria wanaoitwa Yersinia pestis. Mnyama mgugunaji, kama panya, hubeba ugonjwa huu na huenezwa na viroboto wao.

Wanadamu huambukiwa tauni kwa njia zifuatazo:

 • Kuumwa na viroboto
 • Mara nyingi watu huambukizwa tauni baada ya kuumwa na kiroboto aliyeambukizwa.
 • Wakati wa mlipuko wa tauni, wanyama wagugunaji kama panya hufa kwa wingi, na viroboto wao hutoka na kutafuta vyanzo vingine vya damu.
 • Watu na wanyama wanaotembelea maeneo ambapo panya wamekufa kwa tauni huwa katika hatari ya kuumwa na viroboto wa panya hao na kuambukizwa.
 • Mbwa na paka pia wanaweza kubeba viroboto walioambukizwa na kuwaleta nyumbani.
 • Baada ya kuumwa na kiroboto unaweza kupata tauni inayosababisha mtoki au tauni inayosambaa kwenye damu.
 • Kugusa majimaji au tishu zenye maambukizi
 • Wanadamu wanaweza kuambukizwa baada ya kugusa tishu au majimaji ya mwili wa mnyama aliyeambukizwa tauni.
 • Matone yenye uambukizo
 • Mtu mwenye tauni inayosababisha nyumonia, akikohoa hurusha matone ya mate kwenye hewa yenye maambukizi. Mtu mwingine akivuta hewa yenye matone haya hupata tauni inayosababisha nyumonia.
 • Mtu aliyekaribu na mgonjwa wa tauni inayosababisha nyumonia ni rahisi kuambukizwa.
 • Matone kwenye hewa baada ya kukohoa au kupiga chafya ndio njia pekee ya mwanadamu kumwambukiza mwingine tauni.
 • Paka yuko katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa tauni, hii ni kwa sbabu anaweza kula mizoga ya panya na kuambukizwa tauni kisha kuwaambukiza wanadamu.

Aina tatu za tauni ni:

 • Tauni inayosababisha mtoki (bubonic)- maambukizi ya tezi za limfu
 • Tauni inayosababisha nyumonia (pneumonic) – maambukizi ya mapafu
 • Tauni inayosambaa kwenye damu (septicemic) – Maambukizi kwenye damu

Dalili huanza kuonekana siku 2 hadi 7, lakini zinaweza kuanza mapema zaidi kwa tauni inayosababisha nyumonia.

Nani yuko katika hatari zaidi?

Tauni hutokea kwenye maeneo yenye wanyama wagugunaji kama panya. Hatari ni kubwa zaidi kwa watu wanaoishi vijijini, hasa wanaoishi katika maeneo yenye vicheche, panya n.k.

Watu wanaweza kupata tauni kwa kuumwa na viroboto wa wanyama wagugunaji (rodents) wanaobeba bakteria wa tauni. Watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa ni pamoja na:

 • Watu wanaoshughulika na wanyama walioambukizwa
 • Watu huwa katika hatari zaidi, muda mfupi baada ya mlipuko wa tauni.
 • Watu wanaotembelea maeneo yenye panya waliokufa kutokana na tauni.
 • Watu wenye paka walioambukizwa tauni

Wakati gani utafute Matibabu ya haraka?

Watu wanaopaswa kutafuta huduma ya matibabu haraka ni pamoja na:

 • Mtu yeyote ambaye ameanza kuona dalili za tauni baada ya kuumwa na viroboto, hasa baada ya kutembelea eneo lenye mlipuko wa tauni.

Watu walio karibu au wanaoishi na wagonjwa wa tauni ya mapafu, wanapaswa kuchunguzwa , na ikiwezekana kuwekwa chini ya unagalizi. Dawa za antibiotiki zinaweza kutolewa pia kama kinga.

Utambuzi

Hatua ya kwanza ya kutambua ugonjwa wa tauni ni kuchunguzwa na daktari. Ishara ya tauni inayosababisha mtoki ni kuvimba na maumivu ya tezi za limfu. Kuwepo kwa mtoki na historia ya kuumwa na viroboto humsaidia daktari kutambua tauni.

Mara nyingi mgonjwa wa tauni inayosambaa kwenye damu na tauni inayosababisha nyumonia hana dalili zilizo wazi ambazo huonesha kuwa ana tauni. Utambuzi hufanyika kwa kuchukua sampuli kutoka kwa mgonjwa, hasa damu au sehemu ya tezi ya limfu iliyovimba, na kuipima maabara.

Mara baada ya maabara kupokea sampuli, matokeo ya awali ya vipimo yanaweza kuwa tayari ndani ya masaa mawili. Ili kudhibitisha matokeo haya inaweza kuchukua masaa 24 hadi 48.

Mara nyingi, kama mgonjwa anahisiwa kuwa na tauni,  matibabu ya awali kwa kutumia antibiotiki huanzishwa kabla matokeo ya vipimo.

Uchaguzi wa matibabu

Tauni ni ugonjwa mbaya sana, lakini hutibiwa vyema kwa antibiotiki za kawaida. Mgonjwa anapaswa kutibiwa mapema ili kupunguza uwezekano wa kupata matatizo yanayotokana na tauni.

Watu walio karibu na wagonjwa wa tauni inayosababisha nyumonia wanaweza kufanyiwa tathmini na hata kuwekwa chini ya uangalizi. Wanaweza pia kupewa antibiotiki ili kuzuia kutokea kwa dalili kama wameambukizwa.

Wagonjwa wa tauni wanapaswa kupewa matibabu mapema sana. Kama mgonjwa hatapata matibabu ndani ya masaa 24 baada ya dalili za awali kuanza, anaweza kufa. Dawa za antibiotiki zinazoweza kutibu tauni ni pamoja na:

 • Streptomycin
 • Gentamicin
 • Doxycycline
 • Ciprofloxacin

Mgonjwa anaweza kuhitaji kuongezewa maji, oksijeni, au hata msaada kupumua.

Wagonjwa wenye tauni inayosababisha nyumonia wanapaswa kutengwa na wagonjwa wengine. Wahudumu wa afya wanapaswa kujikinga vyema ili wasiambukizwe. Watu waliokuwa karibu na wagonjwa wa tauni ya mapafu wanapaswa kuwekwa chini ya uangalizi na kupewa antibiotiki ili kudhibiti maambukizi mapema.

Nini cha kutarajia?

Bila matibabu, 50% ya watu walio na tauni inayosababisha mtoki hufa. Karibu watu wote wenye tauni inayosababisha nyumonia hufa kama hawatatibiwa. Matibabu hupunguza vifo kwa 8-10%.

Matatizo yanayoweza kutokea

Matatizo yanayoweza kutokea ni pamoja na:

 • Nyumonia
 • Kuenea kwa maambukizi mwili mzima
 • Kifo kama hutatibiwa

Kuzuia

Hatua muhimu za kuzuia maambukizi ya tauni ni pamoja na:

 • Kupunguza panya wanaoishi karibu na nyumba, sehemu kazi au maeneo ya michezo. Ondoa vichaka, miamba, uchafu, kuni zilizotapakaa, na chochote kinachoweza kuwa chakula cha panya.
 • Vaa glavu kama unamshughulikia mnyama mwenye viroboto ili kupunguza uwezekano wa kuambukizwa tauni.
 • Jipake dawa ya kufukuza viroboto (repellant) kama unaenda katika maeneo hatarishi, mfano kuweka kambi mwituni, kupanda mlima au kufanya kazi msituni.
 • Hakikisha hakuna viroboto kwa wanyama wako wa kufugwaa. Wasafishe kwa dawa mara kwa mara. Usiwaache wanyama wako kuzururazurura wanaweza kubeba viroboto na kuwaleta nyumbani.
 • Kama mnyama wako wa kufugwa akiugua mpeleke kwa daktari wa mifugo mapema iwezekanavyo.

Vyanzo

 • Shirika la Afya Duniani (WHO)
 • Shirikisha:

Leave Your Comment