UGONJWA WA TEZI DUME

UGONJWA WA TEZI DUME

 • October 31, 2020
 • 0 Likes
 • 119 Views
 • 0 Comments

Maelezo ya jumla

Tezi dume (prostate), ni tezi iliyo kwenye kizazi cha mwanaume inayozalisha maji maji yanayobeba manii/shahawa. Inaizunguka urethra, mrija unaotoa mkojo kwenye kibofu kwenda nje. Tezi dume ya kila mwanaume huongezeka ukubwa kadri umri unavyoongezeka. Kadri tezi inapokua na kuongezeka ukubwa,inaweza kukandamiza urethra na kusababisha matatizo ya kibofu na matatizo ya kukojoa. Tezi dume inapoongezeka ukubwa huitwa ”benign prostatic hyperplasia” kwa kifupi ”BPH”. Hii sio saratani, na haiongezi hatari ya kupata saratani ya tezi dume.

Nini dalili za kuongezeka ukubwa wa tezi dume?

Si watu wote wenye tezi kubwa hupata dalili, nusu ya watu wenye tezi kubwa hawapati dalili kabisa na nusu iliyobaki hupata dalili, ambazo ni pamoja na:

 • Mkojo unapokuwa unaishilia , hudondoka kwa matone
 • Mkojo kushindwa kutoka (mgonjwa huhisi mkojo umembana,lakini akijaribu kukojoa hautoki)
 • Mkojo haushi kwenye kibofu hata baada ya kutoka kukojoa ,mgonjwa huhisi kuna mkojo umebaki kwenye kibofu.
 • Mgonjwa hawezi kujizuia kukojoa, anajikojolea
 • Mgonjwa hukojoa mara nyingi zaidi kuliko kawaida, huamka kukojoa mara mbili au tatu wakati wa usiku.
 • Kupata maumivu wakati wa kukojoa au kupata mkojo wenye damu (hii inaweza kuashiria kuwa kuna maambukizi kwenye nia ya mkojo)
 • Kusita kwa mkojo, mgonjwa hulazimika kuusubiria mkojo kwa muda kidogo kabla haujaanza kutoka.
 • Mgonjwa hujikamua sana ndio mkojo utoke
 • Mgonjwa huhisi hamu kubwa ya kukojoa,mkojo ukimbana inabidi akimbilie chooni haraka sana.
 • Mkojo hauna nguvu unapotoka, hauendi mbali,huishia kuangukia miguuni mwa mgonjwa

Ni nini kinachosababisha tezi kuwa kubwa?

Sababu halisi ya tezi dume kuongezeka ukubwa haijulikani. Kuna mambo kadhaa yanayohusishwa na ukuaji wa tezi hii, kama vile kuzeeka na kuwa na korodani. Wanaume ambao korodani zao ziliondolewa wakati wakiwa wadogo (kwa mfano, kama matokeo ya kansa ya korodani/pumbu) hawapati BPH. Vivyo hivyo, Kama korodani zitaondolewa kwa mgonjwa mwenye tezi dume kubwa sana, itaanza kupungua ukubwa. hii inaonesha kuwa, kama una korodani zinazofanya kazi, zinaongeza hatari ya tezi yako dume kukua na kuongezeka ukubwa.

Nani yuko kwenye hatari zaidi?

Kadri umri unavyoongezeka uwezekano wa kukua kwa tezi unaongezeka. Tezi dume inawapata wanaume wengi sana, na inawezekana kuwa kila mwanaume atapata BPH kama akiishi miaka mingi zaidi. Tezi hii huanza kukua kwa wanaume waliofikisha umri wa miaka 40 na kuendelea na zaidi ya 90% ya wanaume  walio na umri zaidi ya miaka 80 wana tezi dume kubwa.  Hakuna sababu nyingine maalumu inayoongeza hatari ya kukua kwa tezi dume tofauti na kuwa na korodani zinazofanya kazi kikamilifu.

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Mwone daktari mara moja kama:

 • Unapata mkojo kidogo kuliko kawaida
 • Una homa au unahisi baridi
 • Una maumivu ya mgongo, upande, au maumivu ya tumbo
 • Una damu au usaha kwenye mkojo

Pia mwone daktari kama:

 • Baada ya kukojoa unahisi mkojo umebaki kwenye kibofu, unajihisi mkojo hauishi kwenye kibofu
 • Unatumia dawa zinazoweza kusababisha matatizo ya mkojo, dawa kama vile diuretics, antihistamines, antidepressants, au USIACHE AU KUREKEBISHA dozi ya dawa bila kuzungumza na daktari
 • Umejaribu kujitunza na kujihudumia mwenyewe kwa muda wa miezi miwili bila nafuu

Utambuzi

Baada ya kuchukua historia kamili, daktari atafanya uchunguzi wa sehemu ya ndani ya njia ya haja kubwa –ataingiza kidole cha pili kwenye njia ya kutolea haja kubwa ili kugusa na kuichunguza tezi dume. Vipimo vifuatavyo pia vinaweza kufanyika:

 • Urine flow rate –Kipimo hiki hupima kiwango cha mtiririko wa mkojo.
 • Post-void residual urine test –Kipimo hiki hupima kiwango cha mkojo kinachobaki kwenye kibofu mara tu baada ya kukojoa.
 • Pressure flow studies– kipimo hiki hupima shinikizo (pressure) ndani ya kibofu wakati wa kukojoa.
 • Urinalysis –kipimo hiki huangalia kama kuna damu au maambukizi kwenye mkojo
 • Urine culture – Kipimo hiki huchunguza maambukizi kwa kupanda mkojo kwenye mazingira maalumu ili kuruhusu wadudu walimo kukua,ili iwe rahisi kuwatambua.
 • Prostate-specific antigen (PSA)– kipimo hiki ni maalumu kwa kutambua saratani ya tezi dume. Wagonjwa wa BPH hufanyiwa kipimo hiki ili kuondoa uwezekano wa kuwepo kansa ya tezi hii.
 • Cystoscopy – Kifaa chenye kamera huingizwa kupitia kwenye ncha ya uume,kupitia kwenye urethra ili kuchunguza kibofu.

Unaweza kuombwa kujaza fomu ya kutathmini ukali wa dalili na matokeo ya ugonjwa katika maisha yako ya kila siku. Matokeo ya tathmini yanaweza kulinganishwa na kumbukumbu za zamani ili kuona kama hali yako inakua mbaya zaidi au la.

Uchaguzi wa matibabu

Uchaguzi wa matibabu unategemea ukali wa dalili zako, ni kwa kiasi gani maisha yako ya kila siku yanaathirika, na kama una tatizo lingine la kiafya.

Chaguzi za matibabu kwa ugonjwa wa tezi dume ni pamoja na “Kusubiri huku daktari akifuatilia hali yako (watchful waiting),” mabadiliko ya mfumo wa maisha, dawa, au upasuaji.

Kama una miaka zaidi ya 60, kuna uwezekano mkubwa utakua umeanza kuona dalili. Lakini wanaume wengi wenye ugonjwa wa tezi dum wana dalili kidogo. Mara nyingi hatua za kawaida tu za kujitunza zinatosha kabisa kukufanya ujihisi vizuri.

Kama una BPH, unapaswa kumwona daktari angalau mara moja kwa mwaka ili kufuatilia maendeleo ya dalili zako na kama dalili zimekuwa kali anaweza kushauri mpango mpya wa matibabu.

MADAWA

Alpha 1-blockers (doxazosin, prazosin, tamsulosin, terazosin, na alfuzosin) ni dawa zilizo kwenye kundi la dawa zinazotumika kutibu shinikizo la juu la damu. Madawa haya hulegeza misuli ya shingo ya kibofu na tezi dume. Hii huruhusu mkojo kutoka kwa urahisi. Watu wengi wanatumia dawa ya Alpha 1-blockers, na husaidia sana kupunguza dalili zao.

Finasteride na dutasteride  ni dawa zinazopunguza kiwango cha homoni zinazotengenezwa na tezi dume,hupunguza ukubwa wa  tezi dume, huongeza kiwango cha mtiririko wa mkojo, na kupunguza dalili za BPH. Inaweza kuchukua miezi 3 hadi 6 kabla ya kuona mabadiliko makubwa katika dalili zako. Kutumia finasteride na dutasteride kunaweza kuleta madhara mabaya kama,kupungua kwa nguvu za kiume na hata kuwa hanithi.

Daktari anaweza kuagiza upewe antibiotics ili kutibu  kuvimba kwa tezi dume (prostatitis), mara nyingi prostatitis huambatana na BPH.

UPASUAJI

Upasuaji wa tezi dume unaweza kupendekezwa  iwapo :

 • Unajikojolea/ unashindwa kuzuia mkojo
 • Unakojoa mkojo wenye damu mara kwa mara
 • Unashindwa kukojoa mkojo wote,(Mkojo unabaki kwenye kibofu hata baada ya kukojoa)
 • Maambukizi ya mara kwa mara kwenye njia ya mkojo
 • Kushindwa kwa figo kufanya kazi
 • Mawe kwenye kibofu

Uchaguzi wa aina maalum ya upasuaji, mara nyingi hutegemea ukali wa dalili ,ukubwa na umbo la tezi dume.

 • Transurethral resection of the prostate (TURP): Hii ni aina ya upasuaji inayopendelewa zaidi kutibu ugonjwa wa tezi dume. TURP hufanyika kwa kuingiza kifaa chenye kamera kupitia kwenye uume na kisha kukata na kuondoa tezi dume kipande baada ya kipande.
 • Transurethral incision of the prostate (TUIP): Upasuaji huu unafanana kidogo na TURP, na hufanyika kwa wanaume walio na tezi dume isiyo kubwa sana. Kwa kawaida upasuaji hufanyika na kisha mgonjwa huruhusiwa kwenda nyumbani (hakuna kulazwa). Kama ilivyo kwa TURP, kifaa chenye kamera huungizwa kupitia kwenye uume mpaka kuifikia tezi dume. Kisha, badala ya  kukatakata na kuiondoa, daktari hufanya mkato mdogo kupanua urethra ili kuruhusu mkojo kupita.
 • Simple Prostatectomy : Mgonjwa hupewa dawa ya nusu kaputi na kisha daktari hupasua tumbo (chini ya kitovu) ili kuifikia tezi dume. Sehemu ya ndani ya tezi dume huondolewa . sehemu ya nje huachwa . Huu ni utaratibu unaochukua muda mrefu, mgonjwa huhitajika kulazwa hospitalini kwa siku 5 hadi 10.

Mtiririko wa mkojo huboreka kwa wanaume wengi baada ya kufanyiwa upasujai.

Nini cha kutarajia?

Chaguzi za matibabu kama zilivyoelezwa hapo juu, hupunguza dalili. Upasuaji mara nyingi hufanikiwa zaidi kuondoa dalili, lakini hatari ya kupata matatizo yatokanayo na upasuaji ni mkubwa zaidi.

Matatizo yanayoweza kutokea

Wanaume ambao wamekuwa na BPH kwa muda mrefu wanaweza:

 • Kushindwa ghafla kukojoa (ghafla mkojo hushindwa kutoka)
 • Kuwa na maambukizi kwenye njia ya mkojo
 • Kuwa na mawe ya mkojo
 • Kuharibika figo
 • Kuwa na damu kwenye mkojo

Hata baada ya upasuaji, Tezi dume inaweza kujirudia baada ya kitambo.

Kuzuia

 • Kwa dalili za kawaida:
  • Kojoa mara tu unapobanwa. Pia, kojoa kila unapopata nafasi hata kama hujabanwa.
  • Epuka kunywa pombe na kafeini, hasa baada ya chakula cha jioni.
  • Usinywe maji mengi kwa mara moja. Kunywa maji kidogo kidogo mchana wote. Epuka kunywa maji masaa 2 kabla
  • Jaribu KUTOTUMIA dawa za mafua zenye decongestants au antihistamines. Dawa hizi zinaweza kuongeza dalili za tezi dume.
  • Epuka baridi na fanya mazoezi mara kwa mara. Hali ya ubaridi na kukosa mazoezi kunaweza kusaabisha dalili kuwa mbaya zai
  • Punguza msongo. Hofu na msongo husababisha kukojoa mara kwa mara.

Vyanzo

http://wikidoc.org/index.php/Benign_prostatic_hyperplasia_(patient_information)

Leave Your Comment