Macho

UASTIGMATI:Sababu,dalili,matibabu,kuzuia

Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko

Maelezo ya jumla

Uastigmati (Astigmatism) ni dosari katika jicho/lenzi unaozuia fokasi sahihi ya mwanga kwenye retina (refrative error). Retina ni sehemu  inayopokea nuru ndani ya jicho. Mtu mwenye uastigmati haoni vizuri.

Je, nini dalili za uastigmati?

Hali hii inaweza kusababisha dalili kama vile:

  • Kuona ukungu
  • Makengeza
  • Kuhisi mkazo au kuchoka macho
  • Uchovu
  • Kichwa kuuma
  • Ugumu kuendesha gari usiku

Unaweza kuwa na uastigmati usio mkali na usijue. Hasa kwa watoto wadogo ambao hawajui kawaida ni ipi. Baadhi ya watu wazima wanaweza kuwa na uastigmati usio mkali na usio na dalili yoyote. Ni muhimu kufanya vipimo vya macho ili kuhakikisha unaona vizuri.

Ni nini husababisha uastigmati?

Sababu ya tatizo hili haijulikani. Kwa kawaida mtu huzaliwa na tatizo hili, na mara nyingi hupata ugumu /shida kuona mbali au karibu. Kama hali ya uastigmati haina dalili kali, inachukuliwa kuwa kawaida na haihitaji kurekebishwa.
Mara nyingine uastigmati hutokea baada ya upasuaji au jeraha la jicho. Kwa mara chache, uastigmati wenye dalili kali unaweza kusababishwa na hali fulani isiyo ya kawaida inayoitwa ”keratoconus”. Hali hii huharibu muundo wa konea (sehemu ya mbele ya jicho (iliyo ngumu) inayowezesha miali ya mwanga kupenya na kuingia jichoni).

Nani yuko kwenye hatari zaidi kupata uastigmati   ?

Ugonjwa huu unaweza kuwathiri watoto na watu wazima. Kulingana na utafiti wa nchini Marekani uliochapishwa na ”Archives of Ophthalmology”, karibu watoto 3 kati ya 10 walio kati ya umri wa miaka 5 na 17 wana uastigmati. Kulingana na utafiti uliofanyika nchini Bangladesh, mtu mzima 1 kati ya 3 (32.4%) walio na umri zaidi ya miaka 30 walikuwa na tatizo hili. Tafiti kadhaa zimegundua kuwa kiwango cha uastigmati huongezeka kadri umri unavyoongezeka.
Baadhi ya wagonjwa wenye uastigmati usio na dalili kali wanaweza wasione mabadiliko makubwa. Ni muhimu kufanya vipimo mara kwa mara ili kutambua tatizo hili kwa watoto.

Utambuzi wa uastigmati

Uastigmati unaweza kutambuliwa kwa urahisi baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kina wa jicho. Vipimo maalum mara nyingi havihitajika. Vipimo vinavyoweza kufanyika wakati wa uchunguzi ni pamoja na:

  • Visual acuity: Kipimo hiki huangalia ukali wa picha anayoona mgonjwa, hasa anapoangalia picha za maumbo. Kama mgonjwa anaona maumbo vyema bila kufifia inamaanisha kuwa retina na ubongo vinafanya kazi vyema.
  • Keratometry: Keratometer ni kifaa cha uchunguzi kinachopima mpindo na muundo wa konea, kifaa hiki hupima ukali wa uastigmati.
  • Uwezo wa kupindisha mwanga (refraction): Lenzi kadhaa huwekwa mbele ya macho ya mgonjwa ili kutambua ni miwani ipi inayoweza kuongeza udhahiri na ukali maono.
  • Retinoscopy: Watoto na watu wengine wasioweza kujibu maswali, wanaweza kupimwa kiwango cha tatizo la macho kwa kupima kiasi cha mwanga kinachoakisiwa.

Uastigmati

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Mwone mtoa huduma ya afya au daktari wa macho kama uwezo wako wa kuona unapungua au miwani haisaidii.

Uchaguzi wa matibabu

Uastigmati unaweza kusahihishwa na miwani ya macho, lenzi ya kuweka ndani ya kope za jicho ”contact lenses”, au upasuaji. Uchaguzi wa aina ya matibabu yanayokufaa hutegemea ni aina gani inakufaa kwa mfumo wako wa maisha.
Miwani ya macho ndiyo njia rahisi na salama zaidi kusahihisha uastigmati. Mtaalamu wa macho atakuchagulia aina ya lenzi inayofaa kukusaidia kuona vyema kadri iwezekanavyo.
Contact lenses hufanya kazi kwa kupindisha mwanga unaoingia kwenye jicho na kuboresha fokasi kwenye retina.  Kwa kesi nyingi, lenzi ya kuweka ndani ya jicho huboresha uwezo wa kuona na kuleta unafuu mkubwa. Ni chaguo salama na lenye ufanisi kama zikiwekwa na kutumiwa vizuri. Ni muhimu kunawa mikono na kusafisha lenzi zako kama ulivyoelezwa ili kupunguza hatari ya maambukizi.
Haupaswi kutumia contact lense kama una matatizo fulani ya macho. Ongea na mtaalamu wa macho kupata maelekezo zaidi.
Upasuaji hulenga kurekebisha muundo wa konea. Mabadiliko haya ya muundo husaidia konea ku-fokasi mwanga vyema kwenye retina.

Kuzuia

Hauwezi kuzuia uastigmati, lakini unaweza kuzuia dalili zisiwe mbaya zaidi kwa kufuata maelekezo na njia sahihi ya matibabu. Hivyo, ni muhimu kuchunguzwa vyema macho.

Nini cha kutarajia?

Kwa ujumla, matarajio ya kupona uastigmati ni mazuri sana kama matibabu yatazingatiwa. Uwezo wa kuona hurejea na kuwa kawaida kwa kutumia miwani au lenzi

Vyanzo

Leave feedback about this

  • Quality
  • Price
  • Service

PROS

+
Add Field

CONS

+
Add Field
Choose Image
Choose Video
X