UFA KWENYE NJIA YA HAJA KUBWA

Maelezo ya jumla

Ufa kwenye njia ya haja kubwa (anal fissure) ni hali inayotokana na kuchanika au kupasuka kwa utando utelezi unaoifunika sehemu ya chini ya rektamu

Je! Nini dalili za ufa kwenye njia ya haja kubwa?

Nyufa kwenye njia ya haja kubwa zinaweza kusababisha maumivu wakati wa kwenda haja kubwa na hata kusababisha kutokwa damu. Kinyesi kinaweza kuwa na michirizi ya damu kwa nje au kwenye tishu za chooni baada ya kutawaza.
Dalili nyingine zinaweza kujumuisha:

 • Ufa unaonekana hasa kama eneo hilo likipanuliwa kidogo (mara nyingi ufa huwa katikati)
 • Kufunga choo

Je,Nini husababisha ufa kwenye njia ya haja kubwa?

UNi kawaida sana watoto wadogo kupata nyufa kwenye njia ya haja kubwa,lakini nyufa zinaweza kutokea katika umri wowote. Tafiti zinaonesha kuwa asilimia 80 ya watoto wachanga watapata ufa kwenye njia ya haja kubwa kabla hawajamaliza mwaka wa kwanza. Kiwango cha nyufa zinazotokea hupungua kadri umri unapoongezeka. Watoto wenye umri wa kwenda shule hupata nyufa mara chache sana ukilinganisha na watoto wachanga.

Kwa watu wazima, nyufa zinaweza kusababishwa na kufunga choo, Kupata kinyesi kikubwa,kigumu au kuhara kwa muda mrefu. Kwa watu wazima, ufa kwenye njia ya haja kubwa unaweza kusababishwa pia na kupungua kwa mtiririko wa damu kwenye eneo hilo.
Ni kawaida kwa wanawake waliojifungua hivi karibuni kuwa na nyufa kwenye njia ya haja kubwa

Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata ufa kwenye njia ya haja kubwa?

Watu ambao wako katika hatari zaidi ya kupata ufa kwenye njia ya haja kubwa ni pamoja na:

 • Watoto
 • Wazee
 • Wanawake ambao wamejifungua hivi karibuni
 • Watu wenye ugonjwa wa crohn – ugonjwa huu husababisha kuvimba kwa matumbo
 • Watu ambao wana shida ya kufunga choo au kuhara sugu

Utambuzi wa ufa kwenye njia ya haja kubwa

Mtoa huduma ya afya atafanya uchunguzi wa rektamu na kuangalia tishu ili kutambua kama una ufa.

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Mwone mtoa huduma wa afya kama una dalili za ufa kwenye njia ya haja kubwa, au kama ufa hauponi hata baada ya matibabu.

Uchaguzi wa matibabu ukiwa na ufa kwenye njia ya haja kubwa

Nyufa nyingi hupona zenyewe bila kuhitaji matibabu, kwa watoto usafi wa nepi unahitajika.
Hata hivyo, baadhi ya nyufa zinaweza kuhitaji matibabu. Mbinu zifuatazo zinaweza kutumika nyumbani ili kuponya ufa.

 • Kusafisha taratibu
 • Mabadiliko ya mlo – kula mlo mzito,unaoweza kunyonya maji tumboni
 • Kupaka mafuta ya kulegeza misuli kwenye ngozi
 • Kutumia cream inayopunguza maumivu,hasa wakati wa kwenda haja kubwa
 • Kupaka mafuta ya kawaida (petroleum jelly)
 • Kukalia maji – mgonjwa ataweka maji ya uvuguvugu kwenye chombo na kuyakalia kwa muda,hii hupunguza maumivu
 • Kutumia dawa za kulainisha choo

Kama nyufa kwenye njia ya haja kubwa hazitapona kwa matibabu ya nyumbani,matibabu yafuatayo yanaweza kupendekezwa:

 • Kuchomwa sindano ya botox kwenye misuli ya njia ya haja kubwa, sindano hii hulegeza misuli kwenye njia ya haja kubwa
 • Upasuaji mdogo ili kulegeza misuli ya njia ya haja kubwa

ufa kwenye njia ya haja kubwaNini cha kutarajia ukiwa na ufa kwenye njia ya haja kubwa?

Nyufa kwenye njia ya haja kubwa mara nyingi hupona bila matatizo yoyote. Hata hivyo, watu ambao wamepata ufa kwenye njia ya haja kubwa wana uwezekano mkubwa wa kupata ufa mwingine hapo baadae.

Matatizo yanayoweza kutokea ukiwa na ufa kwenye njia ya haja kubwa

Kwa mara chache, Ufa unaweza kuwa sugu na hauponi. Nyufa sugu zinaweza kuhitaji upasuaji mdogo ili kulegeza misuli inayozunguka mkundu.

Kuzuia nyufa kwenye njia ya haja kubwa

Ili kuzuia nyufa kwenye njia ya haja kubwa, nepi za watoto wachanga zinatakiwa kubadishwa mara kwa mara.
Ili kuzuia nyufa wakati wote:

 • Hakikisha eneo la haja kubwa ni kavu
 • Jifute au tawadha kwa kutumia kitambaa laini au nguo iliyolowekwa au pamba
 • Tibu mapema magonjwa ya kuhara au kufunga choo
 • Epuka kukera au kusumbua au kuchokonoa rektamu

Vyanzo

http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/article/001130.htm

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi