UGONJWA WA FIZI

UGONJWA WA FIZI

 • December 20, 2020
 • 0 Likes
 • 16 Views
 • 0 Comments

Maelezo ya jumla

Ugonjwa wa fizi (gingivitis) husababisha kuvimba kwa fizi.

Dalili za ugonjwa wa fizi?

 • Kutokwa damu kwenye fizi (unakuta damu kwenye mswaki hata kama ukisugua polepole meno)
 • Kuwa na fizi zenye rangi nyekundu sana au zenye rangi ya zambarau
 • Kuwa na fizi zinazouma ukizigusa, lakini vinginevyo haziumi
 • Vidonda kinywani
 • Fizi zilizovimba
 • Fizi zinazong’aa sana

Ni nini husababisha ugonjwa wa fizi?

Ugonjwa wa fizi ni mojawapo ya magonjwa yanayoathiri tishu zinazotegemeza meno (periodontal disease). Ugonjwa huu huathiri tishu zinazotegemeza meno kama vile fizi, kano, na soketi za meno.

Ugonjwa wa kuvimba fizi hutokana na utando wa uchafu uliojengeka kwa muda mrefu kwenye fizi. Utando huu huundwa kwa bakteria, uteute na mabaki ya chakula yanayobakia mdomoni. Utando huu husababisha sehemu kubwa ya meno yanayooza. Utando hujikusanya kwenye shina la jino na bakteria walio kwenye utando hutoa sumu zinazosababisha fizi kuvimba na kuuma.

Majeraha kwenye fizi yanayosababishwa na kitu chochote, kama vile kusugua meno kwa nguvu, yanaweza kusababisha ugonjwa wa fizi.

Yafuatayo huongeza hatari ya kupata ugonjwa wa fizi:

 • Usafi duni wa meno
 • Ujauzito (mabadiliko ya homoni hufanya fizi kuwa sensitive)
 • Kisuari kisichodhibitiwa vyema
 • Magonjwa mengine

Meno ambayo hayajapangika vizuri, meno yaliyozibwa na yenye vifaa vinavyotumika kukaza meno, yanaweza kusababisha ugonjwa wa fizi.

Madawa kama vile phenytoin na dawa za kupanga uzazi na metali nzito kama vile lead na bismuth husababisha ugonjwa wa fizi.

Nani yuko kwenye hatari zaidi?

Watu wengi wana ugonjwa wa kuvimba fizi kwa viwango tofauti tofauti. Mara nyingi huanza utotoni au kipindi cha balehe kwa sababu ya mabadiliko ya homoni na unaweza kuendelea au kujirudiarudia mara kwa mara.

Utambuzi

Daktari wa meno atachunguza kinywa na meno na kuangalia kama una fizo laini, zilizovimba, na nyekundu au zambarau. Utando unaweza kuwepo kwenye shina la meno. Fizi huwa haziumi, ila unaweza kupata maumivu akizigusa.

Mara nyingi hakuna vipimo zaidi vinavyohitajika , lakini eksirei ya meno inaweza kuhitajika kuchunguza kama uvimbe umesambaa .

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Mwone daktari wa meno kama una dalili za ugonjwa wa fizi, hasa kama haujasafishwa au kufanyiwa uchunguzi wa meno kwa zaidi ya miezi 6.

Uchaguzi wa matibabu

Lengo la matibabu ni kupunguza uvimbe. Meno husafishwa vyema na daktari wa meno kwa kutumia vifaa mbalimbali kuondoa uchafu kwenye meno.

Usafi wa kinywa ni muhimu baada ya kusafishwa meno na mtaalamu. Daktari wa meno atakufundisha jinsi ya kusafisha meno yako. Inapendekezwa kuwa usafishwe meno na daktari wa meno kwa angalau mara mbili kwa mwaka au mara kwa mara kwa watu wenye ugonjwa mkali wa fizi. Unaweza kutumia dawa za kusafisha meno pia.

Nini cha kutarajia?

Unaweza kujisikia vibaya wakati wa kuondoa utando kwenye meno. Kuvuja damu na maumivu yatapungua ndani ya wiki 1 au 2 baada ya kusafishwa meno. Kusukutua kwa maji ya uvuguvugu yenye chumvi au dawa ya kusukutua hupunguza uvimbe zaidi. Dawa za maumivu zinaweza kutumika kama maumivu ni makali.

fizi zenye afya zina rangi ya waridi na imara. Usafi wa kinywa unapaswa kuzingatiwa milele, la sivyo ugonjwa wa fizi utajirudia.

Matatizo yanayoweza kutokea

 • Kujirudia kwa ugonjwa wa fizi
 • Kuvimba kwa tishu zingine zinazoshikilia jino-periodontis
 • Maambukizi au jipu kwenye fizi au taya
 • Kunuka mdomo

Kuzuia

Njia bora zaidi ya kuzuia ugonjwa huu, ni kufanya vyema usafi wa kinywa. Unapaswa kupiga mswaki kwa angalau mara mbili kwa siku na kutumia nyuzi za hariri kuondoa uchafu kwenye meno (flossing) kwa angalau mara moja kwa siku. Kwa watu walio katika hatari kubwa zaidi wanaweza kushauriwa kupiga mswaki na kuondoa uchafu kwenye meno baada ya kila mlo. Daktari wa meno anaweza kukupatia maelekezo jinsi ya kusafisha meno kwa kutumia nyuzi na kupiga mswaki.

Kwa watu wenye mahitaji maalumu au walio katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa fizi, daktari wa meno anaweza kupendekeza vifaa maalumu. Vifaa hivi ni pamoja na miswaki maalumu, vijiti vya kusafisha meno (toothpick) na vifaa vingine.

Dawa za kusafisha meno na za kusukutua zinaweza kupendekezwa na daktari wa meno.

Kusafishwa meno mara kwa mara na mtaalamu wa meno ni muhimu ili kuondoa utando -mabaki unaotengenezeka hata kama unapiga mswaki vizuri. Madaktari wa meno wanashauri usafishwe meno angalau mara moja  kila baada ya miezi 6.

Vyanzo

http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/article/001056.htm

 • Share:

Leave Your Comment