Maelezo ya jumla
Ugonjwa wa homa ya matumbo (typhoid fever) ni ugonjwa hatari unaosababishwa na bakteria anayeitwa salmonella typhi.
Ni zipi dalili za ugonjwa wa homa ya matumbo?
Zifuatazo ni dalili za ugonjwa wa homa ya matumbo:
- Maumivu ya tumbo
- Kuwa na hasira/kutotulia
- Kuwa na damu kwenye kinyesi
- Kutetemeka
- Kuchanganyikiwa
- Kushindwa kuwa makini
- Kuanza kuonekana kama hujielewi/kujitambua
- Hisia zinazobadilika badilika
- Kuanza kuona vitu au kusikia sauti ambazo wengine hawazioni
- Kutokwa na damu puani
- Kujisikia mchovu sana
- Mwili kukosa nguvu
Ni nini sababu ya ugonjwa wa homa ya matumbo?
Bakteria anayesababisha ugonjwa wa homa ya matumbo – salmonella typhi – husambaa kutokana na kula chakula, kunywa vinywaji au maji yaliyochafuliwa. Kama ukila au kunywa chochote kilichochafuliwa, bakteria huingia mwilini, na kuingia kwenye utumbo, na baadae kwenye damu, kisha husafiri na kufika kwenye tezi za mwili, mfuko wa nyongo, ini, bandama, na sehemu nyingine za mwili.
Kuna baadhi ya watu wachache wanaweza kubeba bakteria hawa wa salmonella typhi bila kuugua, lakini wanaendelea kutoa bakteria kwenye kinyesi kwa miaka mingi na kusambaza ugonjwa huu. Ugonjwa wa homa ya matumbo umekithiri sana katika nchi zenye uchumi unaokua.
Ni nani yuko kwenye hatari ya kupata ugonjwa wa h0ma ya matumbo?
Mtu yeyote anayekutana na bakteria wa salmonella typhi yuko kwenye hatari.
Ni wakati gani unapaswa kuomba msaada wa kitabibu?
Ongea na daktari kama umekutana na mtu mwenye ugonjwa wa homa ya matumbo au kama una dalili za ugonjwa wa homa ya matumbo. Kama umewahi kuugua na kutibiwa ugonjwa wa homa ya matumbo, wakati mwingine ugonjwa unaweza kujirudia. Ongea na daktari pia kama unapata maumivu makali sana ya tumbo, unapata mkojo kidogo sana au haukojoi kabisa, au kama unaona kuna dalili mpya usizozielewa.
Utambuzi wa ugonjwa wa homa ya matumbo
Unapokuwa umegundulika kuwa una salmonella typhi kwa vipimo vya maabara; stool culture au ELISA daktari ataanzisha matibabu
Uchaguzi wa matibabu ya ugonjwa wa homa ya matumbo
Unaweza kuongezewa maji kupitia kwenye mishipa. Utapatiwa antibiotiki zinazofaa kuua bakteria. Kuna ongezeko kubwa la usugu wa vimelea kwa dawa ulimwenguni, kwa hiyo daktari ataangalia ni aina gani ya dawa inapendekezwa tumika na wizara ya afya.
Baadhi ya dawa zinazopendelewa zaidi ni pamoja na ampicillin, trimethoprim-sulfamethoxazole na ciprofloxacin. Wagonjwa wanapatiwa antibiotiki mara nyingi huanza kujisikia nafuu baada ya siku 2 au 3, ni kwa nadra sana kifo kutokea. Hata hivyo, watu wasiopata matibabu wanaweza kuendelea kupata homa kwa wiki au miezi kadhaa, na karibia 20% hufariki kutokana na matatizo yanayosababishwa na maambukzi haya
Matarajio
Dalili mara nyingi huboreka ndani ya wiki 2 mpaka 4 baada ya matibabu. Matokeo ni mazuri zaidi kama matibabu yatawahi, na yanweza yasiwe mazuri sana kama matatizo yanayosababishwa na maambuzki yatakuwa yameanza kutokea. Dalili zinaweza kujirudia kama mgonjwa hatatumia dawa zote na kupna kabisa maambukizi.
Matatizo yanayoweza kutokea
Yafuatayo ni matatizo yanayoweza kutokea kama ugonjwa wa homa ya matumbo hautatambuliwa na kutibiwa mapema:
- Kuvuja damu kwenye utumbo
- Kutoboka kwa utumbo
- Kushindwa kwa figo kufanya kazi
- Kusambaa kwa maambukizi kwenye tumbo na kusababisha uvimbe wa fumbatio – peritonitis
Kuzuia
Japo zipo chanjo kwa ajili ya kuzuia ugonjwa wa homa ya matumbo, hazifanyi kazi kila wakati, kwa hiyo ni vizuri kunywa maji yaliyochemshwa pekee au maji ya chupa na kula chakula kilichopikwa vyema.
Kuboresha mfumo wa kutibu maji ya bomba, maji taka, na kulinda chakula kisichafuliwe ni moja ya njia za kuilinda jamii dhidi ya homa ya matumbo.
Kama kuna mtu anayebeba ugonjwa huu lakini haugui na anaweza kuwaambukiza wengine “typhoid carriers” wasiruhusiwe kuwa wapishi au kushughulika na chakula.