Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Ugonjwa wa homa ya nyani ni nini?
Homa ya nyani (monkeypox) ni ugonjwa unaosababishwa na virusi uliogunduliwa kwa nyani waliokuwa wamelelewa maabara mwaka 1958. Ugonjwa huu unapatikana zaidi katika nchi za magharibi mwa Afrika. Aina nyingi za wanyama ikiwemo na binadamu wanaweza kuambukizwa ugonjwa huu. Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa homa ya nyani vinafanana kwa karibu na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa ndui (smallpox) na ugonjwa wa homa ya ng’ombe (cowpox) kwa wanadamu.
- Jifunze zaidi kuhusu ugonjwa wa ndui hapa
Ni wanyama gani wanaweza kuambukizwa ugonjwa wa homa ya nyan?
Nyani, jamii zote za panya (panya wa nyumbani, panya buku, kichakuro, kindi) na sungura wanaweza kuambukizwa ugonjwa huu. Ukweli ni kuwa, hatujui kwa hakika ni aina gani na gani za wanyama wanaweza kuambukizwa virusi hawa. Yawezekana wapo wanyama wengine wa mwituni au wa kufuga wanaoweza kuambukizwa lakini hatuwajui bado.
Wanyama wanaambukizwaje ugonjwa wa homa ya nyani
Ugonjwa wa homa ya nyani unasambaa kwa kugusana moja kwa moja na mnyama aliyeambukizwa. Hii inaweza kutokea kupitia vidonda kwenye ngozi au majimaji kwenye hewa.
Wanyama wanaathiriwa vipi na ugonjwa wa homa ya nyani
Kwa wanyama wa jamii ya nyani, kwa kawaida ugonjwa wa homa ya nyani unajitokeza kama upele unaodumu kwa siku 4 mpaka wiki 6; malengelenge yaliojaa usaha yataonekana mwili mzima, lakini yatakuwa mengi zaidi kwenye uso, miguu, viganja vya mikono, nyayo za miguu na mikia. Ni nadra sana kifo kutokea, isipokuwa kwa nyani wachanga. Baadhi ya nyani wanaweza kuambukizwa virusi hawa na wasipate dalili zozote.
Wanadamu wanaambukizwaje ugonjwa wa homa ya nyan
Watu wanaweza kuambukizwa ugonjwa wa homa ya nyani kwa kugusana moja kwa moja na damu, majimaji ya mwili na vidonda vya mnyama aliye na uambukizo. Dalili za ugonjwa zinaanza kuonekana kuanzia siku ya 12 baada ya kuambukizwa. Dalili hizi ni pamoja na;
- Homa
- Maumivu ya kichwa
- Kuhisi baridi
- Maumivu ya koo
- Kuvimba kwa tezi (mtoki)
- Uchovu
Baada ya siku 1 mpaka 3 upele mkubwa unaanza kutokea kwenye mikono na miguu na hata usoni au kwenye mwili. Baadae mapele haya yanabadilika na kuwa kama majipu au malengelenge yaliyojaa usaa. Katika hatua za mwisho, yanapasuaka na kukauka na mwisho yanatawanyika. Ugonjwa huu unadumu kwa muda wa wiki 2 mpaka 4 na watu wengi wanapona vizuri tu.
Nifanye nini kama ninashuku kuwa nina ugonjwa wa homa ya nyani?
- Kwa mnyama – ongea/ mpigie mtaalamu wa wanyama haraka
- Kwa mwanadamu – Ongea / mpigie daktari haraka inavyowezekana
Nitawalinda vipi wanyama wangu na ugonjwa wa homa ya nyani
Kuwapatia chanjo ya vaccinia (ni chanjo inayotumika kukinga dhidi ya ugonjwa wa ndui) inaweza kuwakinga wanyama jamii ya nyani na ugonjwa wa homa ya nyani. Kwa wanyama wengine njia nzuri ya kuwakinga ni kuhakikisha hawakutani na wanyama au watu wenye maambukizi.
Nitajilinda vipi na ugonjwa wa homa ya nyani?
Jitahidi usikutane na wanyama au watu walioambukizwa virusi vya ugonjwa wa homa ya nyani. Japo chanjo inayotumika kukinga ugonjwa wa ndui (smallpox) inaonekana inaweza kufanya kazi kukinga watu dhidi ya homa ya nyani. Â Inapendekezwa itumiwe na watu wanaoshiriki moja kwa moja kuuchunguza na kuudhibiti ugonjwa wa homa ya ini, au wanaofanya tafiti na chunguzi mbalimbali za moja kwa moja kuhusu ugonjwa huu. Chanjo inaweza kutolewa mpaka siku 14 baada ya kuambukizwa.
- Jifunze zaidi kuhusu ugonjwa wa ndui hapa
Vyanzo
http://www.cdc. gov/ncidod/monkeypox/
Leave feedback about this