KUOTA VINYAMA /MASUNDOSUNDO SEHEMU ZA SIRI

Maelezo ya jumla

Ugonjwa wa kuota vinyama sehemu za siri/Masundosundo/vigwaru au “Genital warts”, ni tatizo la kuota vinyama vidogo laini kwenye ngozi au utando laini unaozunguka maeneo ya siri. Vinaweza kutokea kwenye uume, uke, mrija wa mkojo “urethra”, vulva, shingo ya kizazi , au maeneo ya kuzunguka njia ya haja kubwa au ndani yake. Huu ni ugonjwa unaoenezwa kwa njia ya kujamiiana

Sababu za kuota vinyama sehemu za siri/masundosundo

Ugonjwa wa masundosundo husababishwa na jamii ya virusi wanaoitwa ”Human papilloma virus” kwa kifupi HPV. Kuna zaidi ya aina 70 tofauti za virusi wa HPV ingawa si wote wanaosababisha masundosundo kwenyesehemu za siri ”genital warts”. Baadhi ya aina nyingine za virusi vya HPV husababisha masundosundo kwenye ngozi inayozunguka sehemu nyingine za mwili kama vile kwenye mikono au miguu.
Tafiti kadhaa zimeonesha kuwa baadhi ya aina za virusi wa HPV pia husababisha saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake au saratani ya njia ya haja kubwa kwa jinsia zote mbili. Aina hii ya virusi hujulikana kama high-risk HPV. Pamoja na kwamba ugonjwa wa masundosundo kwenye maeneo ya siri umejitokeza kwa kasi kubwa hasa baada ya kuwepo kwa janga la UKIMWI, watu wengi waliopatwa na ugonjwa huu huwa hawaoneshi dalili zozote zile. Kwa mfano, kwa wanawake, virusi wa HPV wana uwezo wa kusambaa mpaka kwenye maeneo ya ndani kabisa ya kuta za uke au shingo ya kizazi bila kuonekana wala kuhisiwa kwa urahisi.

masundosundo
Masundosundo/Vigwaru /Genital warts

Kama tulivyotangulia kueleza hapo awali, maambukizi ya HPV husambaa kutoka kwa mtu mmoja mpaka mwingine kwa njia ya kujamiiana kunakohusisha njia ya haja kubwa, uke au ngono ya mdomoni. Mara baada ya kuambukizwa, inaweza kuchukua mpaka muda wa wiki sita hadi miezi 6 kwa masundosundo kuwa dhahiri, ingawa baadhi ya wagonjwa wanaweza kukaa hata miaka kadhaa bila kuwa na dalili yeyote ile. Aidha imeonekana pia kuwa si kila mtu anayejamiina na aliye na maambukizi ya HPV au mwenye masundosundo anaweza naye kupata ugonjwa huu.

Makundi yaliyo kwenye hatari zaidi kupata masundosundo

Masundosundo huonekana kama vioteo laini vinavyojitokeza juu ya ngozi ingawa wakati mwingine vinaweza kuwa vidogo mno kiasi cha kutoweza kuonekana vizuri kwa macho ya kawaida. Kwa wanaume, vioteo hivi hutokea zaidi kwenye uume, ngozi ya pumbu, eneo la mitoki, mapajani pamoja na maeneo ya kuzunguka nje ya njia ya haja kubwa au ndani yake; wakati kwa wanawake hutokea ndani ya uke au njia ya haja kubwa, nje ya uke au ngozi ya nje kuzunguka njia ya haja kubwa, au ndani ya uke kuzunguka eneo la shingo ya kizazi.
Kwa wale wanaopenda kufanya ngono ya mdomoni, wanaweza kupatwa na masundosundo kwenye maeneo ya kuzunguka mdomo, midomo, kwenye ulimi na hata kwenye utando unaozunguka koo. Dalili nyingine ni kama vile mgonjwa kujihisi kukosekana kwa hisia /kufa ganzi maeneo yaliyozungukwa na masundosundo, kwa wanawake kuongezeka kwa utoko/ uchafu sehemu za siri, kuwashwa sana maeneo ya siri na wakati mwingine kutokwa na damu ukeni mara baada ya tendo la ngono. Hata hivyo dalili hizi hutokea mara chache sana.
Wanawake wengi vijana wanaojihusisha na vitendo vya ngono huambukizwa sana ugonjwa huu lakini wengi wao hupona bila hata kuhitaji matibabu, wakati wanaume wanaoambukizwa, wengi wao huwa hawaoneshi dalili zozote za ugonjwa ingawa wanaweza kuwaambukiza wenzi wao bila ya wao kujua.

Uchunguzi na vipimo

Kwa wanawake, uchunguzi wa ugonjwa wa masundosundo sehemu za siri hujumuisha uchunguzi wa maeneo ya nyonga ambapo daktari huchunguza eneo hilo kwa kutumia vifaa maalum vinavyomuwezesha kuona uwepo wa masundosundo na wapi vilipo.

Wakati fulani, kunyunyizia dawa yenye tindikali ya “acetic acid” husaidia kufanya masundosundo kuonekana kwa urahisi zaidi. Wakati mwingine daktari anaweza pia kufanya kipimo cha “pap smear” kwa ajili ya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi (kwa vile kama tulivyoona hapo awali, zipo aina fulani fulani za HPV ambazo husababisha saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake).
Kwa wanaume, uchunguzi wa maeneo ya siri ni muhimu sana ili kufahamu kama kuna masundosundo au la.

Uchaguzi wa matibabu

Ni vema masundosundo yaliyo sehemu za siri yatibiwe hospitalini na daktari; haishauriwi kutumia dawa za kununua kujitibu mwenyewe kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa kuchanganya aina ya dawa zinazotumika maalum kutibu aina nyingine za vigwaru/masundosundo kwa ajili ya kujitibu masundosundo ya sehemu za siri “genital warts. Matibabu ya vigwaru ya sehemu za siri yanafanyika hospitalini na daktari kwa kuondoa vioteo juu ya ngozi iliyoathirika au kwa kutumia dawa utakazoandikiwa na daktari na kuelekezwa namna ya kuzitumia mwenyewe nyumbani kwa siku kadhaa mpaka majuma kadhaa. Dawa zinazotumika ni pamoja:

  • Podophyllin na podofilox
  • Trichloroacetic acid (TCA) au
  • Imiquimod .

Ukiachilia mbali matumizi ya dawa, masundosundo yanaweza pia kutibiwa kwa njia ya upasuaji mdogo kama vile kwa kuvikata, au kuvimaliza kwa kutumia njia ya baridi/barafu “cryosurgery laser therapy”. Kama yalivyo matibabu ya magonjwa mengine yanayosambaa kwa njia ya ngono, ni lazima yahusishe pia tiba kwa mwenza wa mgonjwa. Wakati mwingine hata kama utajihisi huna dalili za waziwazi, ni vema kumuona daktari ili uchunguzwe na kutibiwa kuepusha kusambaza ugonjwa kwa watu wengine au kuachia ugonjwa mpaka ukakuletea madhara zaidi.
Aidha matibabu yanaweza kuhitaji kurudiwa rudiwa mara kadhaa mpaka masundosundo yatakapokuwa yametoweka kabisa.
Kwa wanawake ambao wametibiwa “genital warts” na kupona au wale ambao wamewahi kuwa na wenza waliowahi kuugua ugonjwa huu, wanashauriwa sana kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa shingo za kizazi “pap smear”, ni vema kufanya kipimo cha “pap smear” walau kila baada ya miezi 3 mpaka 6 tangu kupata matibabu ya awali ya masundosundo sehemu za siri. Na kwa wale watakaonekana kuwa na dalili za awali za saratani ya shingo ya kizazi, hawana budi kufanyiwa uchunguzi na tiba zaidi li kuepusha uwezekano wa kupata saratani kamili ya shingo ya kizazi.

Vyanzo

https://medlineplus.gov/ency/article/000886.htm

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi