UGONJWA WA DEMENTIA (UGONJWA WA KUSAHAU)

Ugonjwa wa dementia (Ugonjwa wa kusahau) ni nini?

Ugonjwa wa dementia (Ugonjwa wa kusahau) ni ugonjwa unaosababisha mgonjwa kupoteza kumbukumbu, kupungua kwa uwezo wa kufikiria, kuongea na mabadiliko katika hisia na tabia. Ugonjwa wa dementia unasababishwa na uharibifu kwenye ubongo unaosababisha seli za ubongo kushindwa kuwasiliana vizuri. Kama mgonjwa akisaidiwa vizuri, anaweza kuishi vyema akiwa na ugonjwa huu.

Nani hupata Ugonjwa wa dementia (Ugonjwa wa kusahau)?

Ugonjwa wa kusahau unaweza kumpata mtu wa tamaduni, rangi, dini, jinsi au nchi yoyote. 2.4% ya watu wenye umri zaidi ya miaka 50 barani afrika wanakadiriwa kuwa na ugonjwa wa dementia (2010). Hii ni sawa na watu milioni 2.7.

Watu takribani 850,000 huishi na ugonjwa dementia nchini Uingereza, ambapo 28,000 wanatoka jamii za watu weusi, waasia na makabila madogo madogo. Idadi hii inatarajiwa kuongezeka mara mbili kufikia mwaka wa 2026.

Watu wa jamii ya waasia na wakaribea weusi wanapatwa zaidi na Ugonjwa wa kusahau kwa sababu pia wako kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa shinikizo la juu la damu, kisukari, kiharusi na ugonjwa wa moyo ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa Ugonjwa wa dementia (Ugonjwa wa kusahau). Jamii zikifanya mabadiliko ya mfumo wa maisha kama vile; kufanya mazoezi na kula chakula bora zitapunguza uwezekano wa kupata ugonjwa huu.

Dalili za Ugonjwa wa dementia (Ugonjwa wa kusahau)

Ugonjwa wa dementia unamwathiri kila mgonjwa kwa namna yake, wagonjwa hawafanani. Mtu mwenye ugonjwa dementia anaweza kuwa na matatizo yafutatayo:

 • Kupoteza kumbukumbu za kila siku – Kusahau alichokuwa anakifanya, hata kama ni muda mfupi tu baada ya kukifanya, kurudia swali lile lile tena na tena bila kujitambua.
 • Kupungua kwa uwezo wa kufikiri, kupanga na kuandaa mambo – Mgonjwa anaweza kuanza kupata ugumu kufanya maamuzi, ugumu kutatua matatizo au kutekeleza majukumu yake (kwa mfano: kushindwa au kusahau kupika chakula).
 • Matatizo wakati wa kuzungumza – Mgonjwa anaweza kushindwa au kusahau maneno sahihi yanayohitajika katika mazungumzo na inaweza kuwa ngumu kufuatilia mazungumzo.
 • Kushindwa kuamua umbali na kina cha vitu – kwa mfano; inaweza kuwa ngumu kupanda ngazi
 • Kusahau muda na eneo alilopo – mgonjwa anaweza kusahau siku, muda, tarehe, au anaweza kupotea na asikumbuke amefikaje alipo.

Sambamba na matatizo haya ya kumbukumbu na uwezo wa kufikiria, mtu aliye na Ugonjwa wa dementia (Ugonjwa wa kusahau) anaweza pia kuwa mwenye mihemko, wasiwasi, hasira, kutotaka kuzungumza au mwenye huzuni mwingi.

Ugonjwa wa kusahau huzidi kuwa mbaya kadri siku zinavyokwenda. Dalili za mgonjwa wa dementia zinaendelea kuongezea na kuwa mbaya zaidi kadri muda unavyosonga. Kwa baadhi ya aina za Ugonjwa wa dementia, mtu anaweza kuona au kusikia sauti ambazo watu wengine hawazisikia au anaweza kuendelea kuamini vitu ambavyo si vya kweli. Mgonjwa anaweza kujikuta akichanganya mambo anayoyafanya sasa na kumbukumbu za zamani.

Kadri siku zinavyokwenda, ugonjwa wa demetia huendelea kuharibu ubongo wa mgonjwa siku hadi siku. Dalili huanza zikiwa kidogo, lakini kadri muda unavyoongezeka ndivyo zinapokuwa mbaya zaidi.

Hata baada ya dalili kudhihirika na daktari kufanya utambuzi kuwa ni Ugonjwa wa kusahau, wagonjwa wengi huendeea kuishi kwa uhuru kwa miaka kadhaa.

Aina za Ugonjwa wa dementia (Ugonjwa wa kusahau)

Dementia sio ugonjwa mmoja, ni neno mwamvuli linalowakilisha magonjwa mengi yanayotokana na uharibifu wa seli za ubongo; kama ilivyo kwa neno ugonjwa moyo, Ugonjwa wa dementia  ni neno mwamvuli linalowakilisha matatizo yanayosababisha matatizo ya kupoteza kumbukumbu na kupungua kwa uwezo wa kufikiri mpaka kuathiri mfumo wa maisha ya kila siku.

Kuna aina nyngi ya magonjwa yaliyo katika mwamvuli huu, yafuatayo ni baadhi:

 • Ugonjwa wa Alzheimer’s: Karibia 60 -80% ya visa vyote vya Ugonjwa wa dementia (Ugonjwa wa kusahau) vinasababishwa na ugonjwa wa Alzheimer. Ugonjwa wa Alzheimer ni aina ya Ugonjwa wa kusahau inayosababishwa na kusinyaa, kupukutika au kufa kwa seli za ubongo. Kwa sababu ya uharibifu wa seli za ubongo, mgonjwa huanza kupoteza kumbukumbu, kupungua kwa uwezo wa kufikiri na hata kusababisha mabadiliko ya tabia na hisia. Dalili huzidi kuwa mbaya zaidi kadri umri unayoongezeka.
 • Ugonjwa wa dementia unaotokana na matatizo ya mishipa ya ubongo (vascular dementia): Karibia 5 -10% ya visa vyote vya Ugonjwa wa dementia (Ugonjwa wa kusahau) vinasababishwa na kupasuka au kuziba kwa mishipa midogo midogo inayopeleka damu kwenye sehemu mbalibali za ubongo. Kwa baadhi ya wagonjwa, aina hii ya Ugonjwa wa kusahau hutokea baada ya kupata tukio la kiharusi.
 • Ugonjwa wa kusahau unaosababishwa na lewy body (Lewi body dementia): Kariba 5 -10% ya visa vyote vya Ugonjwa wa dementia  hutokana na kuwepo kwa protini ngeni inayojengeka kwenye seli za neva za ubongo inayoitwa lewi bodies. Kwa sababu ya uwepo wa protini hii ya lewi bodies, inaathiri uwezo wa mgonjwa kufikiria, kumbukumbu na kutembea/ kujongea. Dalili za mapema ni pamoja na; Kushindwa kutambua kama ni usiku, mchana au asubuhi; kupata ugumu kukadiria umbali na kina na kusababisha iwe ngumu kupanda ngazi, kuona maluweluwe na matatizo mengine ya mwendo.
 • Ugonjwa wa dementia  unaosababisha matatizo kwenye sehemu ya mbele na upande ya ubongo ‘Fronto temporal dementia’’: Aina hii ya Ugonjwa wa kusahau inasababisha madhara kwenye sehemu ya mbele na/au pande za ubongo. Kwa kawaida Ugonjwa wa dementia huwapata watu wenye umri zaidi ya 65, lakini fronto temporal dementia hutokea mapema (miaka 45-65). Dalili za huanza na kuendelea kuwa mbaya zaidi kadri muda unavyokwenda: Mabadiliko ya tabia, hisia, kuwa na wasiwasi mwingi na hata kupoteza stadi za lugha.
 •  Ugonjwa wa kusahau unaosababishwa na sababu mchanganyiko (mixed dementia): Aina hii ya Ugonjwa wa dementia hutokana na sababu zaidi ya moja na mara nyingi mgonjwa huwa na dalili mchanganyiko pia.
 • Magonjwa mengini: Yapo magonjwa mengine pia yanasababisha Ugonjwa wa dementia; ugonjwa wa Parkinson’s, Ugonjwa wa huntington’s, ukosefu wa aina fulani za vitamin, matatizo ya tezi dundumio (thyroid gland), N.k.

Kwa nini ni muhimu ufanyiwe utambuzi?

Mtu yeyote ambaye ana wasiwasi kuhusu kumbukumbu zake anapaswa kuzungumza na daktari. Daktari atashauri na kutathimini ili kutambua kama una ugonjwa wa ubongo. Hakuna kipimo kimoja cha moja kwa moja kinachotumika kutambua Ugonjwa wa kusahau. Madaktari hufanya utambuzi wa aina mbali mbali za Ugonjwa wa kusahau kwa kuongea na mgonjwa, kuchukua historia ya kimatibabu, uchunguzi wa mwili, vipimo vya maabara na kuangalia mabadiliko ya uwezo wa kufikiria, tabia, kumbukumbu na mfumo wa maisha ya kila siku.

Ni muhimu kufanyiwa tathmini na uchunguzi unaofaa kwa sababu:

 • Itasaidia kutambua na kuondoa uwezekano wa kama tatizo limesababishwa na shida nyingine na sio Ugonjwa wa dementia (kwa mfano: maambukizi ya ubongo, sonona au msongo wa mawazo)
 • Itasaida kumpa mgonjwa ufafanuzi kuhusu ugonjwa wake, dalili na matarajio ya yanayokuja ili kupanga vyema atakavyoishi
 • Itamsaidia mgonjwa kupata tiba, ushauri, maelezo na msaada anaohitaji ili kuishi vizuri
 • Tathmini itamruhusu mtu aliye na Ugonjwa wa kusahau kupanga na kufanya mipango ya siku za usoni

Matibabu na msaada

Hakuna tiba inayoweza kuponya kabisa Ugonjwa wa dementia. Lakini kuna mengi yanayoweza kufanywa ili kumsaidia mtu mwenye ugonjwa huu aishi vyema akiwa na hali hiyo. Kwa baadhi ya aina za Ugonjwa wa kusahau, kama vile ugonjwa wa Alzheimer`s, matibabu yanapatikana. Matibabu yaliyopo yanasaidia kudhibiti dalili na kupunguza kasi ya uharibifu wa ubongo, angalau kwa muda.

Aina mbalimbali za matibabu, uangalizi na michezo mbalimbali zinaweza kumsaidia mtu kuishi vyema akiwa na Ugonjwa wa dementia . Kuna mengi tunayoweza kufanya kumsaidia mtu aliye na ugonjwa dementia na familia yake kuishi vyema. Mtu aliye na Ugonjwa wa kusahau anapaswa kuhimizwa kuendelea kushiriki katika shughuli za kijamii, kushughulisha akil na mwili pia. Ni muhimu kuendelea kufanya vitu unavyofurahia, hata kama itamaanisha kubadii namna ya kuvifanya ili uendelee kuvifanya kwa njia tofauti kidogo.

Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata Ugonjwa wa kusahau?

Zipo sababu zinazoweza kubadilishwa na zile zisizoweza kubadilishwa. Ni muhimu kufahamu sababu hizi kwa sababu nyingi zinaweza kubadilishwa.

 • Umri ni sababu kubwa ya kutokea kwa Ugonjwa wa dementia : Ni Watu wachache sana walio na umri chini ya miaka 65 wanaopata ugonjwa dementia, lakini baada ya miaka 65, wagonjwa wanaongezeka zaidi. Ugonjwa wa kusahau unaathri mtu 1 kati ya 6 ya watu wenye mika zaidi ya 80.
 • Kuwa na mzazi au ndugu aliye na ugonjwa wa Alzheimer’s huongeza uwezekano binafsi wa kupata Alzheimer’s.
 • Hali nyingi za kitabibu huongeza hatari ya Ugonjwa wa dementia; ikiwemo shinikizo la juu la damu, ongezeko la mafuta mwini (kolesteroli), matatizo ya moyo, unene wa kupindukia, kiharusi na msongo wa mawazo.
 • Mtindo wa maisha usiofaa – Wenye mazoezi kidogo sana, kuvuta sigara, na kunywa pombe kupita kiasi na lishe yenye mafuta na chumvi nyingi sana – unahusishwa na ongezeko la hatari ya Ugonjwa wa kusahau.

Kupunguza hatari ya kupata Ugonjwa wa dementia (Ugonjwa wa kusahau)

Kuna mengi ambayo mtu anaweza kufanya ili kupunguza uwezekano wake wa kupata ugonjwa wa kupoteza fahamu:

 • Fanya mazoezi ya mwili kila mara – angalau dakika 30 kwa siku, mara tano kwa wiki.
 • Wahi kumwona daktari unapohisi kuwa unaumwa. Fanya uchunguzi wa mwili kila mara na tumia dawa kama ulivyoelekezwa na mtaalamu iwapo unaumwa.
 • Ikiwa unavuta sigara, jaribu kuacha. Punguza kiasi cha pombe unachokunywa (acha kabisa ikiwezekana) – mwombe daktari ushauri kuhusu haya atakusaida.
 • Kula mlo unaofaa – punguza sukari, chumvi na mafuta mengi. Kula samaki, matunda na mboga nyingi za majani.
 • Dumisha uzito unaofaa kiafya – kupitia lishe na mazoezi.
 • Jaribu kuendelea kutumika katika shughuli za kijamii kadri unavyoweza

Kwa kufuata haya, utapunguza hatari ya kupata magonjwa mengine (mfano, ugonjwa wa moyo, shinikizo la juu la damu n.k), ambayo pia huongeza hatari ya kupata Ugonjwa wa kusahau.

Jumbe 5 muhimu

 • Ugonjwa wa dementia (Ugonjwa wa kusahau) si kosa la mtu – yeyote anaweza kuupata.
 • Ugonjwa wa dementia (Ugonjwa wa kusahau) husababishwa na magonjwa ya ubongo na kuna aina nyingi tofauti tofauti.
 • Watu 5 kati ya 6 wa umri zaidi ya miaka 80 hawapati dementia – Sio kila anayezeeka atapata ugonjwa huu
 • Inawezekana kuishi vyema ukiwa na Ugonjwa wa dementia. Unaweza kuendelea kuchangia katika ustawi wa jamii kadri unavyoweza.
 • Mtu aliye na Ugonjwa wa dementia (Ugonjwa wa kusahau) bado ni mtu aliye na hisia, mihemko na maisha kamili.

Vyanzo

https://medlineplus.gov/dementia.html

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi