Magonjwa ya ndani ya mwili

UGONJWA WA MALALE: Sababu, dalili, matiti

Ugonjwa wa malale

Last Updated on October 12, 2023 by Dr Mniko

Maelezo ya jumla

Ugonjwa wa malale (trypanosomiasis /sleeping sickness) ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea wanaoitwa trypanosoma brucei wanaoenezwa na mbung’o. Ugonjwa huu unapatika katika maeneo kadhaa chini ya jangwa la sahara afrika. Watu milioni 60 wanaoishi katika nchi 36 wanaoishi kwenye maeneo yenye hatari ya kuambukizwa ugonjwa huu. Inakadiriwa kuwa watu 50,000 mpaka 70,000 wanaambukizwa ugonjwa huu kila mwaka, japo idadi hii inaonekana kupungua kwa miaka ya hivi karibuni. Karibu watu 48,000 walikufa mwaka 2008 kwa sababu ya ugonjwa huu. Ugonjwa wa malale unasababishwa na aina mbili za vimelea, trypanosoma brucei rhodesiense na Trypanosoma brucei gambiense. Aina kali zaidi ya ugonjwa inasababishwa na rhodesiense.

Ni zipi dalili za ugonjwa wa malale?

Dalili za ugonjwa wa malale zinatokea kwa hatua mbili.

Dalili za hatua ya kwanza hutokea kwa sababu vimelea wamevamia mfumo wa damu na mfumo wa limfu- homa, maumivu ya kichwa na maumivu ya viungo na kuwashwa mwili.

Kuvamiwa kwa mfumo wa damu na mfumo wa limfu na vimelea husababisha kuvimba kwa tezi mwilini na kusababisha mtoki sehemu mbalimbali za mwili.

Ugonjwa wa malale
Mgonjwa analala sana

Kama ugonjwa hautatibiwa katika hatua hii, vimelea huanza kuvamia mwili na kusababisha matatizo makubwa, dalili kama vile upungufu wa damu, uharibifu wa mfumo wa kutengeneza na kudhibiti homoni mwilini, uharibifu wa moyo na figo.

Hatua ya pili ya ugonjwa, huanza kutokea vimelea wanapoanza kuvamia mfumo wa fahamu wa mgonjwa. Vimelea wanapovamia na kuanza kuharibu mfumo wa fahamu, hii ni pamoja na ubongo na mishipa ya fahamu, mgonjwa anapata dalili kama vile kuchanganyikiwa, kushindwa kuratibu mambo, kujihisi mchovu wakati wote, kuota ndoto mbaya na za kuogofya wakati wa mchana na kulala karibia wakati wote wakati wa mchana na kukosa usingizi wakati wa usiku.

Kama mgonjwa asipopata matibabu katika hatua hii, anaweza kufa, uwezo wa akili unaendelea kudhoofika mpaka kuingia kwenye koma na hatimaye kifo. Uharibifu unaosababishwa na vimelea kwenye mfumo wa fahamu hauwezi kutibiwa na kurudi kama ulivyokuwa.

Dalili za jumla ni pamoja na;

 • Kujihisi woga na wasiwasi mwingi
 • Anaonekna mwenye usingizi muda wote
 • Homa
 • Maumivu ya kichwa
 • Analala karibu muda wote
 • Anashindwa kupata usingizi usiku
 • Hisia zake zinabadilika badilika
 • Anatokwa jasho
 • Kuvimba kwa tezi za mwili na kusababisha mtoki
 • Sehemu ulipoumwa na mbung’o pakauwa pamevimba, panauma na pekundu – panatengeneza kinundu kinachouma
 • Anashidwa kujizuia kusinzia – analala lala

Ni nini husababisha ugonjwa wa malale?

trypanosomes
Trypanosoma brucei

Mbung’o ndio husambaza ugonjwa wa malale. Mbung’o aliye na maambukizi anapokuuma, uvimbe mwekundu, unaouma unatokea sehemu alipokuuma. Maambukizi yanasambaa kwenye damu na kusababisha homa, maumivu ya kichwa, kutokwa jasho na kuvimba kwa mtoki mwilini.

Maambukizi yanaposambaa kwenda kwenye mfumo wa fahamu yanasababisha dalili mahususi za ugonjwa wa malale, kama vile kulala sana. Maambukizi yanapofika kwenye ubongo yanasababisha tabia kubadilika, mgonjwa anakuwa mwoga na hisia zake zinabadilikabadilika, baadae anapata maumivu ya kichwa, homa na uchovu. Uvimbe wa misuli ya moyo unaweza kutokea.

Pamoja na kuumwa na mbung’o, ugonjwa wa malale, unaweza pia kuenezwa kwa njia zifuatazo:

 • Kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto – vimelea wa ugonjwa wa malale wanaweza kuvuka kutoka kwa mama na kumwambukiza mtoto akiwa tumboni
 • Maabara – Kuambukizwa kwa bahati mbaya, kwa mfano, wakati wa kushughulikia damu ya mtu mwenye maambukizi ya ugonjwa wa malale au kuwekewa kiungo cha mtu mwenye ugonjwa wa malale – hii ni nadra sana
 • Kuongezewa damu yenye maambukizi ya ugonjwa wa malale
 • Kupitia njia ya kujamiiana (inawezekana, japo ni kwa nadra sana)

Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa wa malale?

Watu wanaishi maeneo ya Afrika yenye mbung’o wengi wako kwenye hatari. Watu wanaosafiri kwenda kwenye maeneo yenye ugonjwa wa malale wako kwenye hatari pia.

Utambuzi wa ugonjwa wa malale

Njia ya uhakika ya kutambua ugonjwa wa malale ni kwa kupima damu ya mgonjwa kuangalia vimelea vya ugonjwa wa malale kwa kutumia darubini. Sampuli ya majimaji inaweza kuchukuliwa kwa sindano kwenye sehemu iliyovimba baada ya kuumwa na mbung’o, kwenye mtoki uliovimba, damu, uboho wa mifupa na kwenye uti wa mgongo ili kupima.

Vipo vipimo vya haraka – trypanosome specific antibodies tests – lakini hivi vinaweza kukosa kutambua ugonjwa kwa baadhi ya visa kama ugonjwa haujasogea sana – ni muhimu kuhakikisha kwa kutumia darubini.

 Wakati gani unapaswa kuomba msaada wa kitabibu haraka?ugonjwa wa malale

Ongea na daktari haraka kama una dalili za ugonjwa huu na unaishi au umetembelea eneo lenye mlipuko au linalojulikana kuwa na ugonjwa wa malale. Ni muhimu kuanza matibabu haraka iwezekanavyo.

Uchaguzi wa matibabu ya ugonjwa wa malale

Dawa zinazotumika kutibu hatua zote mbili za ugonjwa wa malale ni pamoja na:

 • Eflornithine
 • Melarsoprol
 • Pentamidine
 • Suramin

Kuzuia ugonjwa wa malale

Sindano za dawa aina ya PENTAMIDINE zinaweza kukukinga na maambukizi ya vimelea aina ya gambiense, lakini sio rhodesiense.

Kudhibiti na kujikinga na kuumwa na wadudu kutapunguza uwezekano wa kuugua ugonjwa wa malale

 • Kutumia dawa za kufukuza wadudu (repellants)
 • kulala chini ya chandarua.
 • Vaa nguo za mikono mirefu, suruari ndefu, na kofia ili kujikinga unapokuwa maeneo yenye kupe, mbung’o, vaa viatu vinavyofunika

Matarajio

Kama mgonjwa hatapata matibabu, kifo kitatokea ndani ya miezi 6 baada ya moyo kushidwa kufanya kazi au kwa sababu ya vimelea wa malale aina ya rhodesiense.

Ugonjwa wa malale unaotokana na kimelea aina ya gambiense unaasababisha dalili kali kwa sababu vimelea huingia na kuvamia mfumo wa fahamu na kusababisha mgonjwa kusinziasinzia. kwa wagonjwa wa aina hii, ugonjwa huendelea kwa kasi sana na mgonjwa hufa ndani ya wiki kadhaa.

Kwa visa vyote viwili, mgonjwa anapaswa kutibiwa haraka sana.

MAELEZO ZAIDI KUHUSU UGONJWA WA MALALE KWA UFUPI

Maelezo ya jumla

Ni ugonjwa unaosababishwa na protozoa unaosababisha homa, uchovu wa mwili na matatizo ya ubongo yanayoweza kusababisha kifo.

Sababu

Vimelea wanaosababisha kwa kiwango kikubwa ni:

 • Brucei rhodesiense
 • Brucei gambiense

Aina ya vimelea wengine wanaosababisha kwa nadra ni:

 • Cruzi, anayesababisha ugonjwa wa malale wa bara amerika – American Trypanosoniasis

Epidemiolojia

Ugonjwa wa malale unaosababisha ugonjwa wa malale unaosababisha kusinzia sana unapatikana Afrika pekee. Visa vipya 20,000 vinaripotiwa kila mwaka. Vimelea vya T brucei gambiense vinapatikana zaidi katika misitu ya kati na magharibi mwa Afrika.  T.B. rhodesiense anapatikana zaidi maeneo ya savanna na nyika za kati na mashariki mwa Afrika hasa kwa swala.

Uambukizi

Kwa kuumwa na Mbung’o wakati akinyonya damu. Maambukizi yanaweza kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto akiwa tumboni. Ajali katika maabara zinaweza kusababisha maambukizi pia.

Muda kabla dalili kuanza

 1. Brucei rhodensiense: wiki 3 mpaka wiki kadhaa.
 2. T. brucei gambiense: miezi kadhaa mpaka mwaka1

Muda wa uambukizi

Ugonjwa unaweza kuambukizwa muda wote ambapo vimelea watakuwa kwenye damu ya mgonjwa au mnyama au mbung’o

Nani yuko kwenye hatari

Watu wote wanaweza kuambukizwa ugonjwa huu

Muundo wa uambukizo

 1. Mabuu (trypamastigotes) wanaingizwa na mbung’o kwenye ngozi anaponyonya damu
 2. Mabuu wanaongezeka kwenye damu, kwenye mfumo wa limfu na baadae kwenye mfumo wa fahamu.
 3. Mbung’o ananyonya mabuu anapokuja kunyonya damu
 4. Mabuu wanaongezeka kwenye tumbo la mbung’o na kuhamia kwenye mdomo tayari kwa kuambukiza

Dalili

Hatua ya kwanza – kusambaa kwa mabuu kwenye damu

 1. Uvimbe/kidonda kinachouma – sehemu mbung’o alipouma
 2. Homa
 3. Kuvimba mtoki – tezi hazina maumivu
 4. Uchovu
 5. Maumivu ya kichwa
 6. Kupungua uzito
 7. Kuvvimba kwa ini
 8. Mapigo ya moyo kwenda mbio

Hatua ya pili – matatizo kwenye majimaji ya uti wa mgongo (CSF)

 1. Kusinzia sana wakati wa mchana
 2. Kutetemeka
 3. Kukaza kwa misuli
 4. Kushindwa kwa moyo kufanya kazi
 5. Matatizo ya mfumo wa fahamu
 6. Koma na kifo

Utambuzi

 • Kuchunguza kwenye darubini – wet blood smear, thick blood smear
 • Vipimo vya serolojia
 • Kuchunguza uboho wa mfupa

Matibabu

 1. Pentamidine AU
 2. Suramin
 3. Etlornithine AU
 4. Helarsupron AU
 5. Trypansamide

Kuzuia

 1. Elimu kuhusu kujikinga na mbung’o
 2. Kupambana na wadudu wasambazao
 3. Kutibu wagonjwa
 4. Epuka kwenda maeneo yenye kiwango kikubwa cha maambukizi
 5. Vaa nguo zinazokukinga au tumia dawa za kufukuza wadudu
 6. Punguza idadi ya mbung’o kwa;
  • Tambua na fanya uchunguzi kuhusu mazalia ya mbung’o ili kuwadhibiti
  • Kata na fyeka vichaka na nyasi zinazozunguka game reserves, visima vya maji, daraja na pemebezoni mwa mito
  • Pulizia dawa magari yanayotoka katika maeneo yenye mbung’o wengi

Vyanzo

https://medlineplus.gov/ency/article/001362.htm

Leave feedback about this

 • Quality
 • Price
 • Service

PROS

+
Add Field

CONS

+
Add Field
Choose Image
Choose Video
X