Watoto

UGONJWA WA SELIMUNDU (SIKOSELI) – mtoto akiwa na sikoseli

ugonjwa wa selimundu

Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko

Ugonjwa wa selimundu (sikoseli) ni nini?

Ugonjwa wa selimundu (sikoseli) ni aina ya ugonjwa wa damu unaorithiwa na Watoto kutoka kwa wazazi wao. Unasababisha seli nyekundu za damu kutengeneza protin ya hemoglobin iliyoharibika. Protini ya hemoglobin ni sehemu muhimu ya damu inayosaidia kubeba hewa ya oksijeni na kuipeleka mwili mzima.

Hewa ya oksijeni inasafirishwa ndani ya chembechembe nyekundu za damu ikijishikiza kwenye protini inayoitwa hemoglobini. Pamoja na kushikilia oksijeni, hemoglobini inachangia umbo la chembechembe hizi ambalo kwa kawaida ni bapa na mviringo kama vile sahani. Selimundu ni ugonjwa wa kurithi unaosababisha umbo la chembechembe nyekundu za damu kuwa refu na uliochongoka kama mundu au mwezi mchanga unavyoonekana.

Chembechembe za namna hii zinaishi kwa muda mfupi kuliko chembechembe za kawaida, zinapita kwa shida kwenye mishipa midogo ya damu na wakati mwingine kusababisha kuziba kwa mishipa hiyo na hivyo sehemu husika kukosa damu, hewa na virutubishi.Ili kutambua kama mwanao ana ugonjwa huu wa selimundu, daktari atafanya vipimo kadhaa.

.Ugonjwa wa seli mundu

Urithi wa ugonjwa wa selimundu (sikoseli)

Tabia ya selimundu (AS) haijidhihirishi kama ugonjwa. Umuhimu wake mkubwa ni kwamba mtu anakuwa na uwezo wa kuipitisha tabia hiyo kwa watoto wake. Endapo mwenzi wake pia ana tabia ya selimundu, basi kuna uwezekano wa moja kati ya nne kwa kila ujauzito kuwa jeni ya selimundu itarithiwa kutoka kwa wazazi wote wawili na mtoto atakuwa na ugonjwa wa selimundu (SS).Uwezekano wa kuwa na mtoto wa kawaida (AA) pia ni moja kati ya nne, na kuna uwezekano wa 2 kati ya 4 kuwa mtoto atarithi tabia ya selimundu (AS). Ni jambo la muhimu kwa wazazi kupima, ili kufahamu ikiwa mtoto wao ataweza kuathirika

Urithi wa jeni ya Mundu

Kila mtoto hupokea jeni moja ya hemoglobini kutoka kwa kila mzazi. Jeni hizi mbili huamua aina ya hemoglobini. Jeni inayopelekea kuwa na haemoglobini ya kwaida hujulikana kama (A). Jeni inayopelekea uwepo wa ugonjwa wa selimundu hujulikana kama (S). Endapo utarithi jeni mbili za mundu, utakuwa na ugonjwa wa selimundu (SS).

Endapo utarithi jeni moja ya mundu utakuwa na tabia ya selimundu (AS). Kama hutakuwa na jeni yo yote ya mundu, basi utakuwa na hemoglobini ya kawaida (AA). Asilimia 13% – 15% ya watu nchini Tanzania wana tabia ya selimundu (AS) na inakadiriwa kuwa watoto 8,000 – 15,000 wanazaliwa kila mwaka wakiwa na ugonjwa wa selimundu.

Umuhimu wa jeni ya selimundu

Watu wenye haemoglobini ya kawaida (AA) wako katika hatari ya kufariki kutokana na malaria. Watu wenye ugonjwa wa selimundu (SS) wako katika hatari kubwa zaidi ya kufariki kutokana na ugonjwa wa malaria na wa selimundu. Watu wenye tabia ya selimundu (AS) hukingiwa dhidi ya kupata malaria kali na hatimaye kifo.

Dalili za Ugonjwa wa Selimundu

Watu wenye tabia ya selimundu (AS) na baadhi ya wale wenye ugonjwa wa selimundu (SS) hawana dalili yoyote. Kwa upande mwingine, baadhi ya watu wenye ugonjwa (SS) huathiriwa kwa kiasi kikubwa na huwa na dalili wakati wa utoto wao. Njia pekee ya kuwa na uhakika kuhusu hali yako ya umundu wa hemoglobini ni kufanya kipimo cha damu.

Dalili zinatokana na chembechembe nyekundu za damu kuziba mishipa ya damu na chembechembe hizi kuwa na uhai mfupi kuliko kawaida:

 • Anaemia (upungufu wa damu)
 • Watoto wadogo wanaweza kupata maumivu na kuvimba kwa vidole vya mikono na miguu
 • Maumivu makali kwenye mifupa, karibu na viungio na fumbatio
 • Vipindi vya homa vya mara kwa mara kutokana na malaria na maambukizi ya bakteria
 • Maumivu ya kifua na kukosa pumzi
 • Uvimbe sehemu za tumbo kutokana na kupanuka kwa bandama
 • Vidonda sugu kuzunguka vifundo na muundi
 • Homa ya manjano inayosababishwa na kuharibika kwa kasi kwa seli nyekundu za damu (sehemu nyeupe ya jicho kuwa ya manjano)
 • Kudinda kwa uume kunakouma na kusikokoma
 • Kuziba kwa mtiririko wa damu: husababisha uharibufu wa tishu na tatizo hutegemea sehemu ya mwili iliyoathirika, kwa mfano, udhaifu wa ghafla au kupoteza hisia, maumivu ya kichwa au kubadilika ghafla kwa uwezo wa kuona
 • Kuchelewa kukua na kuendelea kimwili.

Ugonjwa wa selimundu (sikoseli) unaweza kusababisha matatizo gani?

Watu wenye ugonjwa wa selimundu wako katika hatari ya kufariki mapema kutokana na matatizo mbalimbali ya kiafya yakiwemo malaria, maambukizi ya bakteria na kiharusi. Zaidi ya hapo, wanaweza kuhitaji kuongezewa damu mara kwa mara kwa sababu ya upungufu wa damu (hatua ambayo inaongeza uwezekano wa kupata virusi vya UKIMWI na ini) na kupata huduma za afya mara kwa mara hospitali.

Unapaswa kufanya nini kama mwanao ana ugonjwa wa selimundu?

Kama mtoto ana maumivu ya mkono, mguu, au mgongo mpigie daktari umweleze kama unaweza, kama haiwezekani kamwone  daktari.

Kama mwanao ana maumivu au kama ameanza kuvimba ghafla eneo la tumboni, inamaanisha kuwa kunaweza kuwepo na tatizo kwenye ini au bandama. Mpeleke mtoto kwa daktari haraka sana.ugonjwa wa selimundu

Ninawezaje kupunguza uwezekano wa mtoto wangu mwenye ugonjwa wa selimundu kupata maambukizi makali

Watoto wote wenye ugonjwa wa selimundu wanapaswa kupewa chanjo zote wanazopaswa kupewa. Muulize daktari kama mtoto anahitaji chanjo nyingine za ziada.

Baadhi ya vimelea wanaweza kusababisha matatizo makubwa kwa afya ya mtoto. Daktari anaweza kumwanzishia mapema mwanao dawa za antibiotiki atakazoendelea kutumia – hata kabla miezi miwili haijaisha. Mwanao anaweza kuendelea kutumia dawa hizi mpaka atakapofikisha miaka mitano. Kama mwanao ana homa zaid ya 380C au 1010F, mpeleke akaonane na daktari.

Upungufu mkubwa wa damu nini na unatibiwaje?

Kama mtoto ana upungufu mkubwa wa damu rangi ya mwanao itafifia sana (midomo, ulimi au kope za macho zinafifia rangi kuwa nyeupe) au kama anachoka sana, anaweza kuwa na upungufu mkubwa wa damu. Upungufu mkubwa wa damu ni dharura na unaweza kutibiwa kwa kumwongezea mtoto damu.

Mwanao anaweza pia kuhitaji kuongezewa damu kabla ya kufanyiwa upasuaji. Hii itapunguza uwezekano wa kupata matatizo wakati wa upasuaji.sikoseli

Kiharusi ni nini na kinatibiwaje?

Kiharusi ni hali inayotokea kunapokuwepo na kizingiti kinachozuia damu isifike vizuri kwenye ubongo. Hii inaweza kusababisha seli za ubongo kufa. Kiharusi kinampata mtoto mmoja kati ya 10 wenye ugonjwa seli mundu (sikoseli).

Daktari anaweza kufanya vipimo ili kuangalia kama mwao yuko kwenye hatari ya kupata kiharusi. Kama mwanao ana miaka miwili au zaidi, muulize daktari kama vipimo hivyo vinahitajika. Kama vipimo vinaonesha uwezekano mkubwa wa kupatwa na kiharusi, dakataria atazungumza nawe kuhusu kuongezewa damu mara kwa mara.

Kama mkono wa mwanao au mguu umelegea au unakosa nguvu, anashindwa kuongea vizuri, anakataa kutembea, au anaonekana kuchanganyikiwa; inaweza kuwa dalili za kiharusi; mpeleke haraka kwa daktari.

Ninawezaje kuitunza afya ya mwanangu mwenye ugonjwa wa selimundu

Mwanao anapaswa kuonana na daktari mwenye uzoefu na ugonjwa wa selimundu. Kadri siku zinavyokwenda utajifunza kutambua mwanao anapopata tatizo kubwa. Daktari atakufundisha pia kuhusu matibabu. Hata wakati ambao watoto wana afya njema, daktari anapaswa kuwaona, kuwafanyia uchunguzi na vipimo kila baada ya miezi mitatu mpaka wafikishe miaka miwili. Baada ya hapo, daktari anapaswa kuwaona kila baada ya miezi sita. Hii itamsaidia daktari kutambua namna mwili wa mwanao unavyofanya kazi na kama matibabu maalumu yanahitajika.

Namna ya kuepuka ugonjwa wa Selimundu

Ugonjwa wa selimundu hauambukizi na hauna tiba ya moja kwa moja. Mpeleke mtoto aliye na dalili zilizotajwa hapo juu kwenye kituo cha afya kutibiwa na kushauriwa namna ya kuishi na ugonjwa huo. Muhimu zaidi ni kuepuka kupata ugonjwa huu. Ikiwa una selimundu au vinasaba vyake, basi amua usizae na mtu mwenye selimundu au vinasaba vyake ili msizae mtoto mwenye selimundu au vinasaba vyake. Watu wanaotoka kwenye familia zenye vinasaba hivi ni vizuri kupima damu ili kujua kama una vinasaba. Ukijua una vinasaba ni vyema kutafuta mwenzi asiye na vinasaba.

Vyanzo

https://medlineplus.gov/sicklecelldisease.html

Leave feedback about this

 • Quality
 • Price
 • Service

PROS

+
Add Field

CONS

+
Add Field
Choose Image
Choose Video
X