Magonjwa ya wanawake

UGUMBA:Sababu,matibabu,kuzuia

ugumba

Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko

Maelezo ya jumla

Ugumba (Infertility) ni hali ya kutoweza kupata ujauzito katika kipindi cha mwaka mmoja au zaidi kwa wenzi ambao wamekuwa wakifanya mapenzi bila kutumia njia zozote za uzazi wa mpango. Hali hii inaweza kutokea kutokana na tatizo kwa mwanaume au mwanamke.

 • Ugumba umegawanywa katika makundi mawili:
  • Wanandoa ambao wanafanya ngono bila kinga kwa angalau mwaka mzima na hawajawahi kupata ujauzito huwa na ugumba wa awali – primary infertility
  • Wanandoa waliowahi kupata ujauzito angalau mara moja lakini hajapata mwingine tena baada ya muda mrefu japo wanafanya juhudi za kupata, wana ugumba unaotokea baadae – secondary infertility

Nini dalili za ugumba?

 • Dalili kuu ya ugumba ni kushindwa kushika mimba. Dalili maalum hutegemea kile kinachosababisha utasa/ugumba.
 • Ugumba unaweza kusababisha hisia kali za machungu na kujilaumu kwa mshirika mmoja au wote wawili.

Nini sababu ya ugumba?ugumba

 • Mambo mbalimbali ya kimwili na kihisia yanaweza kusababisha ugumba. Ugumba unaweza kutokana na matatizo kwa mwanamke, mwanaume, au wote wawili.

UGUMBA KWA WANAWAKE:

 • Ugumba kwa wanawake unaweza kutokea kama:
  • Ovari zinashindwa kuzalisha mayai
  • Mayai yanashindwa kusafiri kutoka kwenye ovari hadi kwenye mji wa mimba
  • Yai lililorutubishwa linashindwa kupandikizwa kwenye ukuta wa mji wa mimba
  • Kiinitete au yai lililorutubishwa linashindwa kuendelea kukua baada ya kupandikizwa kwenye ukuta wa mji wa mimba
 • Ugumba kwa wanawake husababishwa na:
  • Matatizo ya mfumo wa kinga ya mwili, kama vile antiphospholipid syndrome
  • Saratani au kansa au uvimbe
  • Kisukari
  • Uvimbe kwenye mji wa mimba
  • Matatizo ya via vya uzazi ya kuzaliwa nayo yanayoathiri uzazi
  • Kufanya mazoezi kupita kiasi
  • Matatizo ya ulaji au lishe duni
  • Matumizi ya madawa fulani, hii ni pamoja na tibakemikali
  • Kunywa pombe sana
  • Kitambi
  • Uzee
  • Uvimbe kwenye ovari uliojaa maji
  • Maambukizi ya fupanyonga au magonjwa yanayoathiri fupanyonga (Pelvic inflammatory disease)
  • Makovu yanayosababishwa na maambukizi ya magonjwa ya zinaa
  • Magonjwa ya tezi dundumio
  • Homoni kidogo au nyingi sana mwilini

UGUMBA KWA WANAUME:

 • Ugumba kwa wanaume unaweza kutokana na:
  • Kupungua kwa wingi wa manii
  • Kushindwa kutoa nje manii
  • Manii yasiyofanya kazi vizuri
 • Ugumba kwa wanaume unaweza kusababishwa na:
  • Uchafuzi wa mazingira
  • Kukaa katika eneo lenye joto kali kwa muda mrefu
  • Kuzaliwa na matatizo ya uzazi
  • Matumizi mabaya ya pombe, bangi au kokeini
  • Homoni kidogo au nyingi sana mwilini
  • Hanithi (impotence)
  • Maambukizi
  • Uzee
  • Matibabu ya kansa, hii ni pamoja na tibakemikali na mionzi
  • Makovu yanayotokana na magonjwa ya zinaa, kuumia, au upasuaji
  • Manii yanayomwagika ndani, maanii badala ya kumwagwa nje yanarudi ndani–retrograde ejaculation
  • Uvutaji wa sigara
  • Matumizi ya madawa fulani, kama vile cimetidine, spironolactone, na nitrofurantoin
  • Kwa wanandoa walio chini ya umri wa miaka 30 wenye afya njema wanaofanya ngono mara kwa mara, kuna asilimia 25 – 30% kwa mwezi ya kupata ujauzito.
  • Mwanamke hufikia kilele cha rutuba ya kuzaa mwanzoni mwa miaka 20. Baada ya umri wa miaka 35 (na hasa 40), nafasi ya mwanamke kupata mimba hupungua sana.

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Mwone mtoa huduma wa afya kama umejaribu kupata mimba kwa zaidi ya mwaka bila mafanikio.

Utambuzi

 • Wakati unaopaswa kutafuta matibabu ya ugumba hutegemea umri. Inashauriwa kuwa wanawake walio chini ya umri wa miaka 30 wanapaswa kujaribu kupata mimba wenyewe kwa mwaka mmoja kabla ya kufanya vipimo.
 • Vipimo vya ugumba huhusisha historia ya kimatibabu na uchunguzi wa kimwili kwa washirika wote wawili.
 • Vipimo vya damu na picha vitafanyika.
 • Kwa wanawake, hii inajumuisha:
  • Vipimo vya damu kuangalia viwango vya homoni, ikiwa ni pamoja na progesterone na homoni za kuchochea mayai kukua na kutolewa (Follicle stimulating hormone)
  • Kuchunguza hali ya joto ya mwili asubuhi ili kuangalia kama ovari zinatoa mayai
  • Kuingiza kamera ndogo kwenye mji wa mimba na mirija ya uzazi ili kuichunguza (Hysterosalpingography)
  • Ultrasound ya fupanyonga
  • Kuchunguza mkojo kama una homoni inayoitwa lutenizining hormone (hii hutabiri kama yai limetolewa tayari kwa ajili ya kurutubishwa)
  • Vipimo kupima jinsi tezi dundumio inavyofanya kazi- thyroid stimuting hormone
 • Vipimo kwa wanaume vinaweza kujumuisha:
  • Kupima manii
  • Kuchukua kinyama kidogo cha korodani (biopsy) na kukipima katika maabara (hili hufanyika mara chache sana)

Uchaguzi wa matibabuugumba

 • Matibabu hutegemea sababu ya ugumba.
 • Yanaweza kujumuisha:
  • Elimu na ushauri
  • Matibabu ya kutungisha mimba kama vile intrauterine insemination na in-vitro fertilization
  • Madawa kutibu maambukizi na matatizo ya kuganda kwa damu
  • Madawa yanayomsaidia mwanamke kukuza na kutoa mayai kutoka kwenye ovari kwa ajili ya kurutubishwa
  • Ni muhimu kutambua na kujadili athari za kihisia kwako na mwenzi wako zinazotokana na ugumba, na kutafuta ushauri wa kimatibabu.
  • Unaweza kuongeza uwezekano wa kupata ujauzito kila mwezi kwa kufanya ngono kila baada ya siku 3 kabla na baada ya yai kutoka(ovulation). Ni muhimu zaidi kufanya hivi masaa 72 kabla ya yai kutoka (ovulation).
  • Yai hutoka (ovulation) wiki 2 kabla ya mzunguko wa hedhi kuanza (MP). Kama mwanamke anapata hedhi yake kila baada ya siku 28, wanandoa wanapaswa kufanya ngono angalau kila baada ya siku 3 kati ya siku ya 10 na 18 baada ya kipindi hedhi kuanza.

Nini cha kutarajia?

 • Kati ya wanandoa 5 wanaotambuliwa kuwa na ugumba, 1 hupata mimba bila matibabu yoyote
 • Zaidi ya nusu ya wanandoa wenye ugumba hupata ujauzito baada ya matibabu, hii ni bila kujumuisha mbinu zinazohitaji teknolojia kubwa kama vile invitro fertiliziation (IVF).

Matatizo yanayoweza kutokea

 • Ugumba unaweza kuleta athari kubwa ya kihisia kwa wanandoa/wenzi
 • Sonona, wasiwasi, na matatizo ya ndoa yanaweza kutokea.

Kuzuia

 • Kuzuia maambukizi ya magonjwa ya zinaa, kama vile gono na chlamydia, kunaweza kupunguza hatari ya kuwa mgumba.
 • Kudumisha lishe bora, uzito, na mfumo wa maisha ulio bora unaweza kuongeza uwezekano wa kupata ujauzito.
 • Tumia dawa za folati na vitamini kabla na baada ya kupata ujauzito. Hii hupunguza hatari ya mimba kutoka na matatizo ukuaji wa mtoto.

Vyanzo

http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/ency/article/001191.htm

Leave feedback about this

 • Quality
 • Price
 • Service

PROS

+
Add Field

CONS

+
Add Field
Choose Image
Choose Video
X