Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maelezo ya jumla
Unyanyasaji wa kingono kwa watoto (sexual abuse) ni hali ya kuwaingiza kwa makusudi watoto wadogo kwenye shughuli za kingono. Hii inamaanisha, mtoto hulazimishwa au kushawishiwa kufanya ngono au shughuli za kingono na mtu mwingine.
Unyanyasaji wa kingono wa watoto hujumuisha:
- Ngono ya kinywa
- Picha za ngono
- Ngono
- Kugusa au kutomasa tomasa
Utamtambuaje unyanyasaji wa kingono kwa watoto?
Dalili za kutendewa vibaya kingono kwa watoto zinafanana na za mtoto mwenye Sonona ,wasiwasi au hofu. Zinaweza kujumuisha:
- Matatizo ya tumbo, kama vile kujinyea, hasa anapokuwa na wasiwasi mwingi
- Matatizo wakati wa kula, kama vile kupungua/kupoteza hamu ya kula kabisa
- Dalili kwenye via vya uzazi au njia ya haja kubwa, kama vile, maumivu wakati kunya au kukojoa, Kuwashwa au kutokwa uchafu ukeni
- Maumivu ya kichwa ya mara kwa mara
- Mtoto hukosa usingizi/ hushindwa kulala au hushtukashtuka toka usingizini
- Matatizo ya tumbo (malalamiko yao yanaweza yasiwe wazi sana)
Watoto wanaotendewa vibaya kingono wanaweza:
- Kuanza tabia mbaya za kutokujali na uharibifu kama vile kutumia pombe na madawa ya kulevya au kushiriki ngono hatarishi bila kujali
- Kufanya vibaya shuleni
- Kuwa na hofu nyingi sana
- Kujitenga na wengine au shughuli za kawaida zinazofanywa na wengine
Ni nini husababisha unyanyasaji wa kingono kwa watoto?
Jamii ilisita kukabiliana na unyanyasaji wa kingono kwa watoto miongo michache iliyopita. Lakini siku hizi jamii imegutuka na inalichukulia hatua kubwa suala hili.
Ni vigumu kutambua ukubwa wa tatizo hili. Hii ni kwa sababu, swala hili hufanyika kwa siri sana kuliko unyanyasaji wa kimwili. Watoto mara nyingi huogopa kumwambia mtu yeyote kuhusu unyanyasaji huu. Matukio mengi ya unyanyasaji wa aina hii hayaripotiwi.
Wanyanyasaji kwa kawaida ni wanaume. Huwa ni watu wanaofahamiana au walio karibu na mtu anayenyanyaswa. Jambo hili linaumiza moyo sana, kwa sababu mara nyingi tendo hili hufanywa na mtu anayeaminiwa na kutegemewa na mhanga.
Kutendewa vibaya kingono kwa watoto hutokea katika jamii zote bila kujali tofauti za kiuchumi au kijamii.
Mambo yanayoongeza hatari ya kutendewa vibaya kingono watoto hufanana sana na yale yanayoongeza hatari ya unyanyasaji wa kimwili wa watoto, ikiwa ni pamoja na:
- Ulevi wa pombe na madawa ya kulevya
- Matatizo ya familia
- Umaskini
Kwa mara nyingi, watu wanaowatendea vibaya watoto huwa na historia ya kutendwa vibaya kingono au kimwili walipokuwa wadogo.
Baadhi ya watu wanaorudia rudia tabia ya kuwatenda vibaya watoto huwa na ugonjwa wa akili unaojulikana kama pedophilia. Mtu mwenye ugonjwa huu huwatamani watoto wadogo kingono.
Wakati gani utafute matibabu ya haraka?
Kama unashuku mtoto anatendwa vibaya kingono, tafadhali mpeleke hospitalini haraka. Kama hauwezi kumpeleka hospitalini kwa sababu yoyote, toa taarifa polisi mapema.
Utambuzi wa unyanyasaji wa kingono kwa watoto;
Kama unashuku mtoto anatendewa vibaya kingono, mtoto huyo anapaswa kuchunguzwa haraka iwezekanavyo na mtaalamu wa huduma ya afya. Madaktari wengi wamepewa mafunzo maalumu ya kuchunguza kesi zinazohusu unyanyasaji wa kingono.
Usicheleweshe uchunguzi wa daktari kwa sababu yoyote. Ishara nyingi za kuumizwa zinazosababishwa na kutendwa vibaya kingono ni za muda mfupi. Uchunguzi unapaswa kufanyika ndani ya masaa 72 ya tukio au ugunduzi.
Uchunguzi wa mwili mzima ni lazima ufanyike, ili kuangalia kama kuna alama au ishara zozote za kunyanyaswa kimwili na kingono. Aina hizi mbili za unyanyasaji zinaweza kuwepo kwa pamoja.
Maeneo yanayoweza kuathiriwa ni pamoja na kinywa, koo, uume, njia ya haja kubwa, na uke.
Daktari anaweza kupima vipimo vya damu ili kuangalia magonjwa ya zinaa, kama vile kaswende na VVU, na mimba kwa wanawake. Vipimo hivi vinaweza kusaidia kuamua matibabu.
Picha za majeraha zinaweza kusaidia kutunza kumbukumbu ya kilichotokea. Ni muhimu sana kuandika dalili zote zinazotokana na aina yoyote ya unyanyasaji wa watoto.
Ikitolewa taarifa polisi kuhusu kutendwa vibaya kingono, mtoto atapaswa kupimwa na kuchunguzwa na mtaalamu mwenye mafunzo maalumu.
Uchaguzi wa matibabu baada ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto
Matibabu ya kimwili ya majeraha ni sawa na majeraha mengine ya kawaida. Mgonjwa anaweza kuhitaji madawa ili kuzuia au kutibu magonjwa ya zinaa. Watoto wakubwa wanaweza kupata madawa ili kuzuia mimba.
Watoto wote waliotendwa au kunyanyaswa kingono, wanapaswa kupata ushauri kutoka kwa mtaaamu wa afya ya akili.
Kama unashuku mtoto anatendwa vibaya kingono ni jukumu lako kutoa taarifa polisi. Madaktari, waalimu na walezi wa watoto wanatakiwa na sheria kuripoti kama watashuku unyanyasaji.
Baada ya taarifa kutolewa , polisi watapaswa kufanya uchunguzi. Matokeo ya uchunguzi yakionesha ni kweli mtoto anatendwa vibaya, anapaswa kulindwa asinyanyaswe tena. Mtoto anaweza kuhamishwa na kuishi na mzazi asiyekuwa mnyanyasaji au jamaa mwingine.
Nini cha kutarajia baada ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto?
Suala kubwa ni afya ya akili ya mtoto.
Matokeo hutegemea:
- Msaada na ukaribu wa familia na jamii kwa ujumla
- Hulka ya mtoto
- Ni kwa muda gani mtoto alinyanyaswa na aina ya unyanyasaji aliyoipata
- Tiba
Matatizo yanayoweza kutokea
- Matatizo ya wasiwasi
- Sonona/kushuka moyo
- Matatizo ya kula -anaweza kupoteza hamu ya kula
- Matatizo ya usingizi
- Kujihusisha na ngono zisizo salama
- Watoto walionyanyaswa kingono wana hatari kubwa ya kuwa wanyanyasaji watakapokuwa wakubwa
Kuzuia
Tunapaswa kuwafundisha watoto wasikae kimya wanaponyanyaswa
- Tunapaswa kuwafundisha watoto tofauti kati ya mguso “mzuri” na “mbaya” . Wazazi wanapaswa kuanza kazi hii nyumbani.
- Shule zinapaswa kuweka mpango wa kufundisha watoto wa shule kuhusu unyanyasaji wa kingono na jinsi ya kuuzuia.
- Vijana wa umri wa balehe pia wanapaswa kufundishwa jinsi ya kuepuka ubakaji.
Ufuatiliaji na uangalifu wa watu wazima ni muhimu ili kuzuia aina zote za unyanyasaji wa watoto.
Leave feedback about this