Magonjwa ya ndani ya mwili

USAHAULIFU:Sababu,dalili,matibabu,kuzuia

Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko

Maelezo ya jumla

Usahaulifu au kupoteza kumbukumbu (amnesia) ni hali isiyo ya kawaida ya kusahau sana. Mgonjwa anaweza asiwe na uwezo wa kukumbuka matukio mapya, anaweza asiwe na uwezo wa kukumbuka tukio au matukio ya zamani, au yote mawili.

Sababu ya usahaulifu /kupoteza kumbukumbu ni nini?

Kuna maeneo kadhaa ya ubongo yanayosaidia kuunda, kutunza na kurejesha kumbukumbu unapozihitaji. Uharibifu au hitilafu katika maeneo haya kunaweza kusababisha mgonjwa kupoteza kumbukumbu.
Usahaulifu unaosababishwa na sehemu tofauti za ubongo unaweza kuwa tofauti. Kupoteza kumbukumbu/usahaulifu huu unaweza kuhusisha kumbukumbu za matukio mapya, ya zamani au yote. Usahaulifu unaweza kuwa kwa matukio maalum pekee au kwa matukio yote. Mtu anaweza kushindwa kujifunza habari mpya au kutengeneza kumbukumbu mpya.
Uwezo wa kufikiri huenda ukapotea au ukaendelea kuwepo. Mgonjwa anaweza kujaza mapengo ya kumbukumbu yake kwa matukio ya kubuni au kufikirika (yasiyo ya kweli), na anaweza kukanganya muda na mahali alipo.
Usahaulifu unaweza kuwa wa maneno, mawazo, au uwezo wa kutenda mambo. Mgonjwa anaweza kushindwa kukumbuka aina fulani tu ya matukio au vitu fulani pekee.
Usahaulifu unaweza kuwa wa muda mfupi (transient) au wa muda mrefu.
Sababu za kupoteza kumbukumbu ni pamoja na:

  • Pombe au dawa za kulevya
  • Tukio liwezalo kusababisha upungufu wa oksijeni kwenye ubongo (kushindwa kwa moyo, kushindwa kupumua, matatizo yatokanayo na dawa za nusu kaputi)
  • Uvimbe kwenye ubongo (unaosababishwa na saratani au maambukizi)
  • Maambukizi kwenye ubongo kama vile ugonjwa wa kaswende, au VVU / UKIMWI
  • Upasuaji wa ubongo, kama vile upasuaji unaofanyika kutibu ugonjwa wa kifafa
  • Matibabu ya kansa, kama vile tiba ya mionzi ya ubongo au tibakemikali
  • Aina fulani ya degedege
  • Dementia –Ugonjwa huu husababisha mtu kuwa msahaulifu
  • Kama dalili hazitadhibitiwa vizuri, ugonjwa wa kushuka moyo, ugonjwa unaosabisha kufurahi na kuhuzunika kupita kiasi ”bipolar disorder”, au ugonjwa wa skizofrenia unaweza kusababisha mtu kupoteza kumbukumbu
  • Dissociative disorder- Hili ni tatizo la kutokujitambua ambalo humpata mtu anayetaka kujitenga na ukweli, mtu aliyekutwa na jambo kubwa, la kuumiza, jambo asilopenda kulikumbuka. Upotevu huu wa kumbukumbu unaweza kuwa wa muda mfupi au muda mrefu
  • Kuvimba ubongo kunakosababishwa na maambukizi, kemikali, madawa, sumu au magonjwa mengine
  • Kifafa ambacho hakijadhibitiwa vyema kwa dawa
  • Kuumia au majeraha ya kichwa
  • Magonjwa yanayosababisha kupoteza au kuharibika kwa seli za neva (ugonjwa wa neva), kama vile ugonjwa wa ”parkinson”, ugonjwa wa huntington’, au ugonjwa wa ”multiple sclerosis”
  • Matumizi ya pombe ya muda mrefu
  • Kipandauso
  • Matatizo ya lishe (upungufu wa vitamini, mfano vitamini B12)

kupoteza kumbukumbuNani yuko kwenye hatari zaidi?

Kupoteza kumbukumbu kunaweza kusababishwa na mambo mengi, baadhi ya sababu ni za kudumu na nyingine ni za muda tu. Usahaulifu unaweza kuja polepole au kwa ghafla. Uzee unaweza kusababisha iwe vigumu kujifunza mambo mapya na vigumu kutunza kumbukumbu. Hata hivyo, uzee hausababishi mtu kupoteza kumbukumbu haraka, isipokuwa magonjwa ya uzeeni yanapohusishwa.

Utambuzi wa tatizo la usahaulifu

Daktari atafanya uchunguzi wa kina na kuchukua historia ya mgonjwa. Karibu mara zote, marafiki na wanafamilia wataulizwa maswali. Wanafamilia na marafiki wanapaswa kuja na mgonjwa hospitalini.
Maswali watakayoulizwa yanaweza kujumuisha:

  • Aina
    • Je, Mtu huyu anaweza kukumbuka matukio ya hivi karibuni (je! kumbukumbu ya muda mfupi imeathrika)?
    • Je, Mtu huyu anaweza kukumbuka matukio ya zamani au siku za nyuma (Je, kumbukumbu ya muda mrefu imeathirika)?
    • Je, Mgonjwa amepoteza kumbukumbu kuhusu mambo yaliyotokea kabla ya tukio fulani maalum (anterograde amnesia)?
    • Je, Mgonjwa amepoteza kumbukumbu kuhusu mambo yaliyotokea baada ya tukio fulani maalum (retrograde amnesia)?
    • Je, mgonjwa anasahau sana au kidogo?
    • Je, mgonjwa hujaribu kujaza mapengo katika kumbukumbu yake kwa matukio ya kubuni au kufikirika?
  • Muda
    • Je, hali yake inazidi kuwa mbaya mwaka hadi mwaka?
    • Je, kupoteza kumbukumbu kumeanza ndani ya wiki kadhaa au miezi?
    • Je kupoteza kumbukumbu kunakuwepo wakati wote au kuna vipindi maalumu vya kutokea tatizo hili?
    • Kama kuna vipindi maalum vya kutokea tatizo hili, vinadumu kwa muda gani?
  • Sababu zinazochochea
    • Je, amewahi kuumia au kupata jeraha kichwani siku za hivi karibuni?
    • Je! Amekutwa au kupatwa na tukio la kutisha au kudhoofisha nafsi?
    • Je! Amewahi kufanyiwa upasuaji baada ya kupewa dawa za nusu kaputi?
    • Je, Anatumia pombe? Kiasi gani?
    • Je! unatumia madawa haramu / ya kulevya? Kiasi gani? Aina gani?
  • Dalili nyingine
    • Je, Ana dalili zipi nyingine?
    • Je, mgonjwa amechanganyikiwa au hajitambua?
    • Je! Anaweza kujitegemea wakati wa kula, kuvaa, au kujitunza?
    • Je, Amepata degedege?

Uchunguzi wa mwili utahusisha vipimo vya kina vya uwezo wa kufikiri na kumbukumbu, na uchunguzi wa mfumo wa neva.
Vipimo vinavyoweza kufanyika ni pamoja na:

  • Vipimo vya damu kwa ajili ya magonjwa maalum (kama vile upungufu wa vitamini B12 au ugonjwa wa tezi dundumio(thyroid)
  • Angiography ya ubongo
  • Vipimo vya kupima ufahamu na utambuzi (vipimo vya kisaikolojia)
  • CT Scan au MRI ya kichwa
  • EEG

usahaulifuWakati gani utafute matibabu ya haraka?

Mwone mtoa huduma wa afya kama una tatizo la kusahau-sahau

Uchaguzi wa matibabu

Kwa watu wenye matatizo madogo ya kusahau sahau, tiba ya kurejesha na kuboresha ufahamu wa mgonjwa (cognitive therapy) inayofanywa na mtaalamu wa lugha/kunena na watalaamu wa saikolojia

Huduma nyumbani kwa mtu mwenye tatizo la usahaulifu

Wanafamilia wanapaswa kumtegemeza mgonjwa. Wanapaswa kumkumbusha uhalisia kwa kutumia muziki, vitu, au picha ili kumsaidia aendelee kujitambua na kutambua wakati na mahali alipo. Watu wengine wanaweza kuhitaji msaada ili kujifunza upya mambo waliyoyasahau. Ratiba na kiasi cha dawa anachotakiwa kutumia mgonjwa, kiandikwe ili asitegemee kumbukumbu kufuata ratiba hiyo.

Vyanzo

http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/ency/article/003257.htm

Leave feedback about this

  • Quality
  • Price
  • Service

PROS

+
Add Field

CONS

+
Add Field
Choose Image
Choose Video
X