UTAPIAMLO: Ukondefu, udumavu, kiribatumbo

Utapiamlo

Hali ya kupungua au kuzidi kwa baadhi ya virutubishi mwilini ambapo husababisha lishe duni au unene uliozidi.  Utapiamlo unajumuisha kupungua kwa virutubishi mwilini/lishe duni pamoja na kuzidi kwa virutubishi mwilini.  Uwepo wa pamoja wa matatizo ya utapiamlo wa kuzidi kwa virutubishi mwilini na ule wa kupungua kwa virutubishi mwilini ni tatizo linalojitokeza katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

Utapiamlo unaotokana na upungufu wa virutubishi mwilini Utapiamlo

Upungufu wa virutubishi mwilini ni hali inayotokana na ulaji wa chakula chenye upungufu wa:

 • Virutubishi vinavyohitajika mwilini kwa kiasi kikubwa
 • Virutubishi vinavyohitajika mwilini kwa kiasi kidogo
 • Ufyonzwaji hafifu na matumizi duni ya virutubishi mwilini
 • Upotevu wa virutubishi unaosababishwa na maradhi
 • Ongezeko la uhitaji wa nishati lishe.

Kwa ujumla lishe duni ni matokeo ya upungufu wa kiasi na ubora wa chakula pamoja na magonjwa ya kuambukiza ya mara kwa mara. Kupungua kwa virutubishi mwilini/Lishe duni hujitokeza katika hali mbalimbali ambazo ni pamoja na: uzito pungufu, udumavu, ukondefu na upungufu wa madini na vitamini (Vitamin A, madini joto na madini chuma n.k.).

Utapiamlo wa muda mfupi

Hutokana na kukosa chakula cha kutosha katika kipindi cha muda mfupi na mara nyingine huchangiwa na maradhi ya mara kwa mara. Mara nyingi hujidhihirisha kwa kupungua uzito kwa muda mfupi kwa sababu ya kupungua/kupotea kwa mafuta mwilini na kukonda kwa misuli. Aina kuu mbili za utapiamlo wa muda mfupi ni:

 • Utapiamlo wa kadiri
 • Utapiamlo Mkali

Utapiamlo wa muda mrefu

Huu ni upungufu wa virutubishi kwa muda mrefu unaoathiri ukuaji hasa kuongezeka kwa kimo na maendeleo ya akili. Upungufu huu kwa mama mjamzito au anaenyonyesha unaweza kusababisha udumavu wa mwili na akili kwa mtoto.  Udumavu unaweza kujidhihirisha kwa mtoto kushindwa kukua na kuongezeka kimo (yaani uwiano usiosahihi wa urefu kwa umri).

Viashiria vya upungufu wa virutubishi mwiliniKiribatumbo

Vifuatavyo ni viashiria vya upungufu wa virutubishi mwilini:

 • Udumavu: ni hali inayojitokeza wakati uwiano kati ya urefu na umri unakuwa chini kwa vigezo vya ukuaji wa mtoto vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani.  Udumavu unaweza kusababishwa na:
  • Ulaji duni unaondelea kwa muda mrefu
  • Upungufu wa nishati – lishe au virutubishi vya madini na vitamini
  • Utapiamlo wakati wa ujauzito
  • Magonjwa ya mara kwa mara (au magonjwa ya muda mrefu).
 • Ukondefu: ni uwiano wa uzito na urefu unapokuwa chini kwa vigezo vya ukuaji wa mtoto vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani. Kwa watu wazima ni pale uwiano kati ya uzito na urefu (BMI) unapokuwa chini ya 18.5 kg/m2. Ukondefu unatokana na ulaji duni unaondelea katika kipindi cha muda mfupi ambao kwa kawaida huambatana na magonjwa ya mara kwa mara.
 • Uzito pungufu: ni uwiano wa uzito na umri unakuwa chini kwa vigezo vya ukuaji wa mtoto vilivyowekwa na Shirika ka Afya Duniani. Uzito pungufu unaweza kusababisha utapiamlo wa muda mrefu au utapiamlo wa muda mfupi. Sababu zinazopelekea uzito pungufu ni:
  • Ulaji duni wa muda mfupi au mrefu,
  • Magonjwa na
  • Wakati mwingine inakuwa ni ngumu kujua sababu.
 • Upungufu wa vitamini na madini: Ni hali ya upungufu wa vitamini na madini mwilini, pia hujulikana kama njaa iliyofichika, mfano; upungufu wa vitamini A, upungufu wa madini chuma, upungufu wa madini joto, n.k. Upungufu wa vitamini na madini unasababishwa na ulaji wa chakula chenye kiwango kidogo cha madini na vitamini kisichokidhi mahitaji kilishe ya mwili, pia maradhi ya mara kwa mara na mabadiliko ya kimwili (ujauzito na kunyonyesha) yanayoweza kusababisha ongezeko la mahitaji, matumizi au upotevu wa virutubishi.

Athari za lishe duni kwa watoto

Lishe duni kwa watoto husababisha matatizo yenye madhara ya muda mrefu kama yafuatayo: Madhara ya muda mrefu. Madhara hayo ni kama yafuatayo:

 • Udumavu wa kimo
 • Uwezo duni wa kuanza kuongea
 • Kudhoofika kwa mfumo wa kinga ya mwili.
 • Uwezo mdogo wa uzalishaji wakati wa utu uzima Inaathiri ukuaji wa ubongo na maendeleo ya mtoto

Uhusiano wa utapiamlo na maambukizi ya magonjwa

Lishe duni husababisha kushuka kwa kinga ya mwili na kupunguza uwezo wa mwili kupambana na maambukizi hivyo kupata magonjwa kwa urahisi. Magonjwa yanaweza kuathiri lishe kwa kupunguza hamu ya kula, kuongeza mahitaji ya virutubishi, kupotea kwa virutubishi na kuathiri ufyonzwaji wake mwilini. Hali hii inaathiri zaidi watoto wadogo kwa sababu husababisha maendeleo duni ya ukuaji wa mwili na akili.

Utapiamlo unaotokana na kuzidi kwa virutubishi mwiliniUkondefu

Utapiamlo unaotokana na kuzidi kwa virutubishi mwilini:ni hali inayotokana na ulaji uliopitiliza na kuzidi mahitaji ya virutubishi mwilini. Kuzidi kwa virutubishi mwilini kunaweza kusababisha:

 • Uzito uliozidi
 • Unene uliokithiri au kiribatumbo
 • Athari kwenye utendaji kazi wa mifumo ya mwili,
 • Magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo na baadhi ya saratani.

Sababu za Uzito Uliozidi na Kiribatumbo

Uzito uliozidi na kiribatumbo husababishwa na;

 • Ulaji usiofaa; kama vile ulaji wa vyakula vyenye nishati lishe kwa wingi mfano wanga, mafutana sukari (soda, juisi za viwandani na biskuti) na ulaji hafifu wa vyakula vyenye makapi lishe kwa wingi kama vile mbogamboga, matunda na nafaka zisizokobolewa
 • Kutofanya mazoezi na kazi; Hii ni tabia ya watu kutokufanya mazoezi ya mara kwa mara na kutopata muda wa kufanya shughuli mbalimbali za kutumia nguvu husababisha kuongezeka uzito na kiribatumbo. Inashauriwa mtu afanye mazoezi angalau kwa dakika 30 kila siku.

Kiribatumbo kwa Watoto

Kama ilivyo kwa watu wazima, watoto pia wanaweza kupata kiribatumbo, mambo yafuatayo yanachangia kiribatumbo kwa watoto:

 • Uzito uliozidi na kisukari cha mimba kwa mama mjamzito husababisha mtoto kuzaliwa na uzito mkubwa
 • Kutokuzingatia taratibu sahihi za unyonyeshaji wa maziwa ya mama mfano matumizi ya maziwa mbadala kabla ya mtoto kutimiza umri wa miezi sita
 • Kutozingatia taratibu sahihi za ulishaji wa chakula cha nyongeza mfano kumpatia mtoto vyakula vyenye mafuta au sukari kwa wingi
 • Maisha ya mtoto kukaa bila kucheza au kufanya mazoezi
 • Ulaji wa vyakula vyenye nishati lishe kwa wingi

Athari za uzito uliozidi na kiribatumbo

Uzito uliozidi na kiribatumbo kwa watoto husababisha ongezeko la magonjwa sugu na yasiyo ya kuambukizwa kama vile;

Vyanzo

https://www.tfnc.go.tz/publications/9

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi