Magonjwa ya ndani ya mwili

UVIMBE KWENYE UBONGO:Sababu,dalili,matibabu

uvimbe kwenye ubongo

Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko

Maelezo ya jumla

Hakuna sababu inayojulikana ya kutokea kwa uvimbe kwenye ubongo. Ubongo ni sehemu ya mfumo mkuu wa neva. Ni chanzo cha mawazo, hisia, kumbukumbu, lugha, kuona, kusikia, kutembea, na kadhalika.  Kwa upande mmoja, uvimbe unaweza kuharibu moja kwa moja seli za ubongo. Kwa upande mwingine, unaweza kuharibu seli za ubongo kwa kuzibana, kuzikandamiza na kusababisha kuvimba kwa ubongo kunakosababisha kuongezeka kwa shinikizo ndani ya fuvu. Dalili za kawaida ni pamoja na degedege, Kufa ganzi sehemu fulani ya mwili, kichwa kuuma, homa, nk. Matibabu yake ni, upasuaji, tiba ya mionzi, tibakemikali, au mchanganyiko wa hayo.

Je, nini dalili za uvimbe kwenye ubongo?

Uvimbe kwenye ubongo unapokuwa bado mdogo, hausababishi dalili zozote. Kadri uvimbe unavyokua, dalili zifuatazo zinaweza kutokea:

  • Degedege
  • Kupungua kwa uwezo wa kuhisi kwenye eneo fulani la mwili
  • Kupata shida kuongea
  • Kupungua kwa uwezo wa kuona au kuona vitu viwiliviwili
  • Kupoteza uwezo wa kusikia
  • Mabadiliko ya tabia na hulka
  • Hisia zisizo thabiti (hisia zinazobadilika badilika)
  • Kwikwi

Matatizo mengine ya kiafya yanaweza kusababisha dalili hizi. Ni daktari pekee anayeweza kutofautisha kwa uhakika. Mtu yeyote mwenye dalili hizi anapaswa kumwambia daktari ili tatizo litambuliwe na matibabu yaanze mapema iwezekanavyo.

Aina za uvimbe kwenye ubongouvimbe kwenye ubongo

Uvimbe kwenye ubongo umegawanywa katika makundi kadhaa kulingana na eneo ulipo, aina ya tishu zilizothiriwa na kama uvimbe huo ni kansa au la. Uvimbe unaweza kutokea katika umri wowote, lakini aina nyingi za uvimbe hutokea katika umri fulani. Uvimbe aina ya ”gliomas” na ”meningioma” huwapata zaidi watu wazima.
”Glioma” hutokana na seli za ”glial” kama vile ”astrocyte”, ”oligodendrocyte”, na seli za ”ependymal” zinazopatikana kwenye ubongo. Kuna aina tatu za ”glioma”:

  • Uvimbe unaotokana na seli za ”astrocyte” (astrocytomas), huvamia na kuharibu ubongo taratibu.
  • Uvimbe unaotokana na seli za ”oligodendrocyte” (oligodendrocytic tumors), unaweza kuvamia ubongo na kuuharibu polepole au haraka sana .
  • ”Glioblastoma” ni aina ya uvimbe iliyo hatari zaidi, aina hii huvamia na kuuharibu ubongo kwa kasi sana.

”Meningioma” ni aina nyingine ya uvimbe wa ubongo. Uvimbe huu:

  • Kwa kawaida hutokea kwa watu wenye umri kati ya miaka 40 hadi 70
  • Huwapata zaidi wanawake
  • Takribani 90% si saratani, lakini kutokana na sehemu ulipo na ukubwa wake, uvimbe huu unaweza kusababisha matatizo makubwa na hata kifo. Baadhi, ni kansa kali sana.

Aina nyingine za uvimbe kwenye ubongo huwapata watu wazima kwa nadra sana. Hizi ni pamoja na:

  • ”Ependymoma”
  • Uvimbe kwenye pituitari
  • Uvimbe wa tezi za limfu za ubongo (lymphoma)
  • Uvimbe kweye tezi ya pineal
  • n.k

Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata uvimbe kwenye ubongo?

Tafiti za kitabibu zinaonesha kuwa, kutokea kwa uvimbe kwenye ubongo kunahusiana na mambo kadhaa.

  • Kukutana na mionzi
  • Historia ya familia
  • Matatizo ya mfumo wa kinga
  • Matumizi ya simu ya mkononi: Kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu hili katika miaka ya hivi karibuni.

Wakati gani utafute matibabu kama una uvimbe kwenye ubongo?

Mwone mtoa huduma ya afya kama una dalili za uvimbe kwenye ubongo. Kama ukipata mojawapo ya dalili zifuatazo, tafuta msaada wa kitabibu haraka iwezekanavyo:

  • Kupata usingizi au mzubao wa ghafla
  • Kupata shida ya kuona ghafla
  • Kupata shida ya kuongea ghafla
  • Matatizo ya ufahamu, kama vile, kupoteza fahamu, kuchanganyikwa, au kubadilika ghafla kwa hulka ya mtu

Utambuzi wa uvimbe kwenye ubongo

  • Magnetic resonance imaging (MRI): Ni kipimo muhimu sana kwa ajili ya kutambua tatizo lolote kwenye ubongo. Kipimo hiki hutumia nguvu ya sumaku kupiga picha bora zaidi ya tishu za ubongo.
  • Computed tomography (CT): Kipimo hiki hutumia nguvu ya mionzi kupiga picha ya ubongo. CT scan hutumika mara nyingi kugundua uvimbe kwenye ubongo. Inaweza kuonesha eneo ilipo kansa, tezi za limfu na maeneo mengine kulikoenea kansa. Ni muhimu kuwa na tarifa hizi ili kuamua hatua ya saratani na kama upasuaji ni chaguo bora la matibabu.
  • Positron emission tomography (PET) : Wakati wa kufanya kipimo hiki, kiasi kidogo cha miali nunurishi ”radioactive” huchomwa mwilini mwako na kuingia kwenye tishu na viungo vyote mwilini. Miali nunurishi hutoa nishati ambayo hutumiwa kuzalisha picha. ”PET scan” hutoa maelezo zaidi na muhimu kuliko ”CT” au ”MRI”. ”PET” ni muhimu sana katika kutambua kama kansa imeenea kwenda kwenye tezi za limfu au mahala pengine mwilini
  • Eksirei ya kifua: ”X-ray” ya kifua inaweza kufanyika ili kuona kama saratani imeenea mpaka kwenye mapafu.

 Uchaguzi wa matibabu ya uvimbe kwenye ubongo

Kuna machaguo mengi ya tiba kwa wagonjwa wenye uvimbe kwenye ubongo. Uchaguzi wa tiba hutegemea hatua ya uvimbe. Njia zinazotumika ni upasuaji, tiba ya mionzi, Tibakemikali, tiba ya kulenga, au mchanganyiko wa njia hizi. Wakati wa kufanya uchaguzi kuhusu njia ya matibabu, muulize daktari kuhusu madhara yanayoweza kutokana na tiba na ni kwa jinsi gani tiba inaweza kubadilisha maisha yako ya kawaida. Madhara yanayotokana na tiba ya saratani ni kawaida, hii ni kwa sababu, matibabu ya saratani  mara nyingi huharibu seli na tishu zenye afya pia.  Madhara yanaweza yasifanane kwa kila mtu na yanaweza kubadilikabadilika katika kipindi chote cha tiba.

  • Upasuaji: Kama hatua/stage na afya kwa ujumla inaruhusu, daktari wa upasuaji wa mfumo wa neva (neurosurgeon) atapendekeza kuondoa uvimbe kwa kadri inavyowezekana bila kuathiri kazi ya kawaida ya ubongo.
  • Tiba ya mionzi: Tiba hii hutumia mionzi yenye nguvu kuua au kuzuia seli za kansa zisikue.
  • Tibakemikali: Tiba hii hutumia madawa kuua au kuzuia ukuaji wa seli za saratani. Madawa yanayotumika ni pamoja na carboplatin, carmustine, cisplatin na etoposide.
  • Tiba inayolenga: Tiba hii hutumia madawa kama vile bevacizumab yanayolenga mabadiliko ya jeni (gene) katika seli zinazosababisha saratani.

Dawa za kuepuka kama una uvimbe kwenye ubongo

Wagonjwa wenye uvimbe kwenye ubongo wanapaswa kuepuka kutumia dawa zifuatazo:

  • Streptokinase

Kama una uvimbe kwenye ubongo, shauriana na daktari kabla ya kuanza au kuacha kutumia dawa hizi.

Magonjwa yenye dalili zinazofanana

  • Hali zinazosababisha degedege
  • Kiharusi
  • Kuvuja damu ubongoni
  • uvimbe wa tando za uti wa mgongo na ubongo ”meningitis”

Kuzuia uvimbe kwenye ubongo

Sababu ya kutokea kwa uvimbe kwenye ubongo haijulikani. Kwa sababu hiyo, hakuna njia ya kuzuia hali hii kwa sasa.

Nini cha kutarajia?

Matarajio hutegemea mambo yafuatayo:

  • Kama uvimbe unaweza kuondolewa kwa upasuaji
  • Eneo kwenye ubongo ulipo uvimbe
  • Hatua ya kansa: ukubwa wa uvimbe, kama saratani imeenea mpaka nje ya ubongo
  • Kama kansa ndo imegunduliwa au imejirudia tena
  • Afya ya mgonjwa kwa ujumla

Matatizo yanayoweza kutokea

  • Kubanwa kwa ubongo
  • Kupoteza uwezo wa kuwasiliana au kufanya kazi
  • Ubongo unaweza kupoteza uwezo wa kufanya kazi
  • Madhara yatokanayo na madawa, hii ni pamoja na tibakemikali
  • Madhara ya matibabu ya mionzi

Vyanzo

http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/ency/article/007222.htm

    • 1 year ago (Edit)

    Mie nna dalili hizo, wakati mwingine nahisi kama vile nataka kuanguka, wakati mwingine najihisi kama nataka kuzunguushwa kwenye kitu Cha kuzunguka, wakati mwingine najihisi uzito sana wa kichwa, na nakua napata shida kumbuka vitu nikianza kumbuka mpaka nahisi maumivu kichwani, napata shida kupata usingizi, na macho yanakua sometime yanaona nyotanyota. Kugeuka na kulala Chali pia kunanipa shida, misuli ya shingo inakaza pia.

    • 2 years ago (Edit)

    Mimi nasumbuliwa na maumivu ya kichwa na kichwa mda wote kinakuw kizito adi nakosa frah na adi sasa tabia zangu naona nmebadilikab mtu akinisemesha kidogo nakasilika yan cyo wa kucheka mara mara

      • 2 years ago

      Ni vzr kumwona daktari ili akufanyie uchunguzi, msongo wa mawazo au sonona inaweza pia kusababisha shida yako
      Kama hauwezi kufika kwa daktari, zungumza na mtu unayemwamini atakushauri pa kuanzia

Leave feedback about this

  • Quality
  • Price
  • Service

PROS

+
Add Field

CONS

+
Add Field
Choose Image
Choose Video
X