VIDOLE VINAPATA BARIDI SANA:Sababu,dalili,matibabu

Maelezo ya jumla

Vidole vinapata baridi sana – ni kawaida kwa vidole vya miguu au mikono kushikwa na baridi. Lakini kwa baadhi ya watu, vidole vinashikwa na baridi kali sana utadhani vimetoka ndani ya jokofu/friji. Mzunguko usio wa kutosha wa damu kwenda kwenye vidole vya mikono na miguu au upungufu wa homoni zinazotolewa na tezi dundumio ‘’thyroid gland’’ unaweza kuchangia vidole kuathiriwa sana na baridi.

Lakini sababu kubwa ya tatizo hili ni ugonjwa unaoitwa ‘’Raynaud’s’’, ukiwa na ugonjwa huu mishipa midogo ya damu inayopeleka damu kwenye vidole vya mikono (na wakati mwigine vya miguu) inasinyaa kabisa na kutoruhusu damu kupita baada ya kuhisi baridi. Vidole vinaanza kuwa baridi na kubadilika rangi kuwa vyeupe, baadae vinakuwa bluu. Damu inapoanza kurudi baada ya baridi kuisha, vinaanza kuwa vyekundu tena, vinawasha, vinaputa, vipata ganzi au maumivu. Ugonjwa huu wa ‘’Raynauds’’ unaweza pia kusababishwa na kufanya kazi na vifaa vinavyotikisika sana’’vibrating’’ kama vile msumeno wa umeme.
Unaweza kupata tatizo hili kwa sababu ya matumizi ya baadhi ya madawa au msongo wa mawazo.  Au unaweza kuwa na tatizo hili kama dalili ya ugonjwa mwingine unaoathiri mishipa midogo ya damu au maungio.

Mwone daktari kama

Panga kumwona daktari, kama vidole vya miguu au vidole vya mikono vinaathiriwa sana na baridi ili atambue sababu ni nini

Unachoweza kufanya wewe mwenyewe

Kama vidole vya miguu au vidole ya mikono vinaathiriwa sana na baridi, jaribu kufanya mambo yafuatayo ili kupunguza ukali wa dalili.

 • Epuka kushika vitu vya baridi kadri unavyoweza. Vaa glavu nzito au tumia taulo unapotaka kuweka au kuchukua chakula kutoka kwenye friji. Tumia kitambaa unapotaka kushika kinywaji baridi
 • Acha kuvuta sigara: ‘’nicotine’’ iliyo ndani ya sigara inasababisha mishipa kusinyaa na inaweza kuchangia kusababisha ugonjwa wa ‘’Raynauds’’
 • Punguza kunywa vinywaji vyenye kafeini ‘’caffeine’’ kama vile kahawa
 • Hakikisha unajitunza usipigwe na baridi, mwili ukiwa na joto unasaidia damu kuzunguka vizuri na kufika mpaka kwenye vidole vya mikono na miguu. Vaa mavazi ya kukukinga na baridi unapokwenda nje au mahali penye baridi kali

Vidole vinapata baridi sana

  • Vaa mavazi yenye tabaka kadhaa za kitambaa ili kusaidia kutunza joto karibu na ngozi yako
  • Vaa kofia na pasha mikono kabla ya kuvaa glavu za baridi. Kuna glavu maalumu zenye mfumo maalumu unaotumia betri kupasha joto vidole, unaweza kuulizia kama unaweza kuzipata
  • Vaa soksi nzito na weka vitu vya kutia joto miguu ‘’padding’’ kwenye viatu. Epuka kuvaa viatu au nguo zinavyobana kwa sababu zinaweza kusababisha ugumu kwa damu kufikia sehemu fulanifulani za mwili.
 • Kama vidole vimeanza kubadilika rangi na kuwa vyeupe na unahisi ganzi, izungusha mikono kwa kuitupatupa au kwa kuibembeza huku ukifinya au kukunja ngumi na kuachia. Chezesha vidole vya miguu ili kuogeza mzunguko wa damu. Unaweza pia kuiloweka miguu au mikono kwenye maji ya uvuguvugu ili kuitia joto (hakikisha kuwa maji sio ya moto yakakuunguza)
 • Hakikisha kuwa matandiko ya kitanda unacholala yanakupatia joto la kutosha unapokuwa umelala. Unaweza kununua na kutumia blanketi maalumu zinazopashwa na umeme ili kukutia joto. Vaa pia soksi unapokua umelala.

Kuzuia

Kama unapatwa na shida ya kupatwa na baridi kwenye vidole vya miguu au mikono mara kwa mara, unaweza kufanya mabadiliko kadhaa kwenye mfumo wa maisha ili kuzuia au kupunguza matukio

 • Fanya mazoezi mara kwa mara ili kuboresha mzunguko wa damu
 • Kama tatizo linasababishwa na msongo, jaribu kutumia mazoeizi ya upumuaji ‘’deep breathing exercise’’ na mbinu za mazoezi ya kulegeza misuli ‘’muscle relaxation techniques’’  ili kupunguza msongo. BONYA HAPA KUJIFUNZA MAZOEZI HAYO
 • Epuka kutumia vifaaa vinavyotikisika sana ‘’vibrating’’ kama vinasababisha upate tatizo hili

Vyanzo

https://www.mayoclinic.org/symptoms/cold-hands/basics/definition/sym-20050648
https://www.nhs.uk/conditions/raynauds/

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi