Maelezo ya jumla
Vidonda vya tumbo (peptic ulcers) ni vidonda kwenye ukuta wa tumbo au duodeni (mwanzo wa utumbo mdogo). Vidonda vinawapata watu wengi siku hizi: Mmoja kati ya Watu 10 hupata kidonda kwa wakati fulani katika maisha yake. Sababu za vidonda vya tumbo ni maambukizi ya bakteria, matumizi ya muda mrefu ya dawa aina ”NSAIDs” kama vile ”aspirin” na ”ibuprofen”. Kwa mara chache, uvimbe wa saratani ndani ya tumbo au kongosho unaweza kusababisha vidonda. Vidonda vya tumbo havisababishwi na msongo wa mawazo au kula chakula chenye pilipili, lakini mambo haya yanaweza kusababisha hali ya vidonda vilivyopo kuwa vibaya zaidi.
Je! Nini dalili za vidonda vya tumbo?
Mara nyingi mgonjwa hujisikia vibaya tumboni. Anaweza kupata maumivu hafifu tumboni yasiyo makali, yanayoudhi na kukera.
- Yanakuja na kuondoka kila baada ya siku au wiki kadhaa.
- Yanayotokea saa 2 hadi 3 baada ya kula chakula
- Yanayotokea katikati ya usiku -wakati tumbo likiwa tupu
- Yanayopoa baada ya kula chakula
- Yanayopoa baada ya kunywa dawa aina ya antacid
Dalili zingine ni pamoja na:
- Kupungua uzito
- Kukosa hamu ya chakula
- Kuvimbiwa
- Kupiga mbweu sana
- Kichefuchefu
- Kutapika
Watu wengine hupata dalili kidogo tu na wengine hawapati dalili kali kabisa.
Dalili za dharura ukiwa na vidonda vya tumbo
Ikiwa una dalili zifuatazo, mwone daktari mara moja:
- Maumivu makali ya tumbo yanayotokea ghafla na yasiyopoa
- Kinyesi cheusi au chenye damu
- Kutapika damu au kutapika matapishi yenye rangi ya kahawia kama kahawa
Dalili hizo zinaweza kuwa ishara ya tatizo kubwa kama
- Kutoboka kwa utumbo/tumbo— kidonda kinaweza kuchimba ukuta wa tumbo/utumbo na kuutoboa
- Kuvuja damu tumboni — Kidonda au asidi ya tumboni inaweza kula kuta za mishipa ya damu na kusababisha damu kuvujia tumboni
- Kuzuia chakula kupita — Kidonda kinaweza kuzuia chakula kutoka kwenye tumbo kwenda kwenye utumbo mdogo
Ni nini husababisha vidonda vya tumbo?
Vidonda vya tumbo husababishwa na:
- Bakteria anayeitwa ”helicobacter pylori” au ”H. pylori” kwa kifupi
- Dawa aina ya ”Nonsteroidal anti-inflammatory” kama vile ”aspirin” na ”ibuprofen”
- Magonjwa mengine
Mwili hutengeneza asidi kali ambayo hutumika kumen’genya chakula. Kwenye tumbo na sehemu ya mwanzo ya utumbo mwembamba kuna utando mwembaba uliotengenezwa kwa uteteute.
- Utando huu hufanya kazi ya kulinda kuta za ndani za tumbo/utumbo zisiharibiwe na asidi. Ikiwa utando huu umeharibika/kupungua, asidi inaweza kula na kuharibu kuta za tumbo.
- ”H. pylori” na dawa aina ya ”NSAIDs” hupunguza utando wa uteteute huu. Kwa sababu utando umepungua, asidi inaweza kuzifikia kuta za tumbo/utumbo na kuziharibu.
Bakteria aina ya ”H. pylori” husababisha karibu theluthi mbili ya vidonda vyote. Watu wengi wana maambukizi ya ”H. pylori”. Lakini si kila mtu aliye na maambukizi atapata ugonjwa huu. Vidonda vingi vingine husababishwa na ”NSAIDs”. Na kwa mara chache vidonda husababishwa na magonjwa mengine.
Nani yuko kwenye hatari zaidi kupata vidonda vya tumbo?
Una uwezekano mkubwa wa kupata vidonda vya tumbo ikiwa :
- Una maambukizi ya ”H. pylori”
- Una tumia dawa aina ya ”NSAIDs” mara nyingi
- Unavuta sigara
- Unakunywa pombe
- Una jamaa ambaye ana vidonda kwenye tumbo
- Una umri wa miaka 50 au zaidi
Utambuzi wa vidonda vya tumbo
Ikiwa una dalili, mwone daktari . Daktari anaweza kuagiza kufanyika vipimo vifuatavyo:
- Picha yaeksirei ya tumbo na duodeni – Utakunywa uji unaoitwa ”barium” ili kufanya tumbo na sehemu ya mwanzo ya utumbo mdogo ”duodeni” kuonekana vyema kwenye eksirei na kisha picha itapigwa. Vidonda vya tumbo vinaweza kuonekana kwenye picha ya eksirei
- ”Endoscopy” – Kuangalia kuta za tumbo na duodeni kwa kutumia tube nyembamba yenye tochi na kamera ndogo mwishoni. Utameza dawa ili kukupunguzia kiwewe, na kisha daktari atapitisha mpira kupitia kwenye mdomo mpaka tumboni na duodeni. Daktari pia anaweza kuchukua kinyama kidogo kutoka tumboni ili kukipima kwa darubini. Utaratibu huu unaitwa biopsy.
Kama una vidonda vya tumbo, daktari atapima pumzi yako, damu, au tishu ili kuona kama vimesababishwa na bakteria.
Wakati gani utafute matibabu haraka?
Wahi kituo cha afya ikiwa:
- Umepata ghafla maumivu makali sana ya tumbo
- Tumbo linauma ukiligusa na limekakamaa na kuwa gumu
- Una dalili za mshtuko kama vile kupoteza fahamu, kutokwa jasho jingi, au kuchanganyikiwa
- Kutapika damu au kutoa kinyesi chenye damu (hasa ikiwa ni kahawia au nyeusi kama lami)
Omba msaada wa kufika kituo cha afya haraka ikiwa
- Unajisikia kizunguzungu
- Una dalili za vidonda vya tumbo
Uchaguzi wa matibabu kwa vidonda vya tumbo
Vidonda vya tumbo vinaweza kutibika. Dawa za kutibu vidonda vya tumbo ni:
- ”Proton pump inhibitors” au ”histamine receptor blockers Inhibitors” huzuia tumbo yako kutengeneza asidi
- Antibiotiki huua bakteria
Kulingana na dalili, unaweza kutumia dawa moja au zaidi kwa wiki kadhaa. Zitapunguza maumivu na kusaidia kuponya vidonda. Vidonda huchukua muda kupona. Endelea kutumia dawa hata kama maumivu yamepoa. Ikiwa dawa hizi zitakufanya ujihisi mgonjwa au kizunguzungu, au kusababisha kuhara au kichwa kuuma, daktari anaweza kukubadilishia dawa.
Ikiwa vidonda vimesababishwa na dawa aina ya ”NSAIDs” utapaswa kuacha kuzitumia. Kama unavuta sigara , acha, kuvuta sigara hupunguza uponyaji wa vidonda.
Mara nyingi, dawa huponya vidonda. Unaweza kuhitaji upasuaji ikiwa vidonda :
- Haviponi
- Vinarudi mara kwa mara
- Vimetoboa utumbo au tumbo
- Vimesababisa damu kuvujia tumboni
- Vimezuia chakula kutoka tumboni kwenda kwenye utumbo mdogo
Upasuaji unaweza:
- Kuondoa vidonda
- Kupunguza kiasi cha asidi kinachotengezwa tumboni mwako.
Dawa za kuepuka ukiwa na vidonda
Wagonjwa waliogunguliwa kuwa wana vidonda vya tumbo vinavyovuja damu, wanapaswa kuepuka kutumia dawa zaifuatazo:
- ”Ticlopidine”
- ”Prasugrel”
- ”Reserpine”
- ”Streptokinase”
- ”Vorapaxar”
Ikiwa umegundua kuwa una vidonda vya tumbo vinavyovuja damu,Wasiliana na daktari wako kabla ya kuanza au kuacha kutumia dawa yoyote kati ya hizi.
Namna ya kuzuia vidonda vya tumbo
Mabadiliko ya mfumo wa maisha yanaweza kusaidia. Baadhi ya mambo unayoweza kufanya ni pamoja na:
- Kuepuka kutumia ”aspirin”, ”ibuprofen”, ”naproxen”, na ”NSAIDs” nyingine. Badala yake jaribu kutumia ”paracetamol” . Ikiwa ni lazima utumie hizi dawa ongea na daktari kwanza.
- Usitafune tumbaku au kuvuta sigara.
- Punguza kunywa pombe.
Nini cha kutarajia?
Vidonda vya tumbo hurudi ikiwa havijatibiwa vizuri. Ikiwa utafuata maelekezo ya matibabu ya daktari na kutumia dawa zote kama ilivyoelezwa, maambukizi ya ”H. pylori ”yataponywa na utakuwa na uwezekano mdogo sana wa kupata vidonda tena.
Matatizo yatokanayo na vidonda vya tumbo
- Kuvuja damu ndani ya mwili
- Kuziba kwa utumbo kuankosababisha chakula kushindwa kutoka tumboni kwenda kwenye utumbo mdogo
- Kuvimba kwa tishu ambazo zinazunguka ukuta wa tumbo -kuvimba kwa fumbatio – ”peritonitis”
- Kutoboka kwa tumbo na utumbo
Leave feedback about this