VIFO VYA AKINA MAMA WAJAWAZITO

Maelezo ya jumla

Kifo cha mama, au vifo vya akina mama au kifo kinachotokana na uzazi ni kifo cha mwanamke kinachotokea wakati wa ujauzito au muda mfupi baada ya kujifungua. Mnamo mwaka 2000, Umoja wa Mataifa ulikadiria vifo vya akinamama ulimwenguni kote kuwa 529,000, ambapo chini ya 1% vilitokea katika nchi zilizoendelea. Sababu nyingi za vifo hivi zilikuwa za kuepukika kabisa, kwa sababu matibabu yake yalikuwa yanafahamika toka miaka ya 1950.
Kulingana na shirika la afya duniani, “kifo cha mama kinachotokana na uzazi” ni kifo kinachotokea wakati wa ujauzito au ndani ya siku 42 baada ya kujifungua au baada ya mimba kuharibika, hii haijalishi kama mimba ilitungwa nje au ndani ya mji wa mimba, haijalishi kama kifo kimesababishwa au kimechangiwa na ujauzito au matibabu, lakini kifo hicho kisiwe kimetokana na ajali au matatizo ya kijamii au mazingira [1]
Kuna tofauti kati ya kifo kinachotokana moja kwa moja na matatizo yanayotokana na ujauzito, kujifungua au matibabu yake na kifo kisicho cha moja kwa moja kinachosababishwa na tatizo jingine la kiafya lililokuwepo au lilijitokeza wakati wa ujauzito. Vifo vingine visivyohusiana na ujauzito ni kama vile ajali, matatizo ya kijamii au mazingira.

Sababu kuu za vifo vya akina mama

Sababu kuu za vifo vya akina mama ni maambukizi ya bakteria, kutokwa na damu nyingi wakati wa ujauzito, kutungwa kwa mimba nje ya mji wa mimba, maambukizi yanayotokea baada ya kujifungua na matatizo yanayotokana na utoaji wa mimba.
Kama ilivyosemwa kwenye ripoti ya shirika la afya duniani ya mwaka 2005 “Kila mama na mtoto ni wa pekee”. Sababu kuu za vifo ni:

 • Kutokwa na damu nyingi (25%)
 • Maambukizi (13%)
 • Kifafa cha mimba (12%)
 • Uzazi mgumu-mtoto kushindwa kupita/kupita kwa shida-(8%)
 • Matatizo yanayotokana na utoaji mimba (13%)
 • Matatizo ya moja kwa moja (8%)
 • Matatizo yasiyo ya moja kwa moja (20%).

Matatizo yasiyo ya moja kwa moja kama vile malaria, upungufu wa damu, UKIMWI na matatizo ya moyo. Matatizo haya husababisha ujauzito kuwa mgumu zaidi au ujauzito unaweza kusababisha ugonjwa kuwa mbaya zaidi.

Kiwango cha vifo vya akina mama

Kiwango cha vifo vya akina mama hupimwa kwa kuangalia uwiano wa vifo vinavyotokea kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa wakiwa hai. Uwiano huu hutumika kutathimini ubora wa huduma za afya nchini.
Nchi ya Sierra Leone ndio nchi yenye vifo vingi zaidi vya akina mama vinavyotokana na uzazi, wanawake 2000 hufa kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa, ya pili ni Afghanistan yenye kiwango cha vifo 1900 kwa vizazi 100,000, hii ni kulingana na taarifa ya Umoja wa mataifa ya mwaka 2000. Nchi zenye kiwango kidogo kabisa cha vifo vya akina mama ni Ice land, yenye vifo 0 kati ya vizazi 100,000 na Austria yenye vifo 4 kati ya vizazi 100000.
Kwa wanawake wanaoishi katika nchi zilizo chini ya jangwa la sahara, mwanamke 1 kati ya 16 yuko kwenye hatari ya kufa kutokana na ujauzito atakaobeba. Kwa nchi zilizoendelea hatari ya kufa ni mwanamke 1 kati ya wanawake 2,800.
Mnamo mwaka 2003, WHO, UNICEF na UNFPA zilitoa ripoti ya takwimu zilizokusanywa kutoka mwaka 2000. Wastani wa wanawake waliokufa ulimwenguni kutokana na uzazi ilikuwa 400 kati ya watoto 100,000 waliozaliwa. Wastani kwa nchi zilizoendelea ulikuwa 20 na kwa nchi zinazoendelea 440. Nchi zilizokuwa na vifo vingi zaidi ni pamoja na:

 • Sierra Leone (2000)
 • Afghanistan (1,900)
 • Malawi (1,800)
 • Angola (1,700)
 • Niger (1,600)
 • Tanzania (1,500)
 • Rwanda (1,400)
 • Mali (1,200)
 • Somalia, Zimbabwe, Chad, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Guinea Bissau (1,100 kila moja)
 • Msumbiji, Burkina Faso, Burundi, na Mauritania (1,000 kila moja)

Uwiano huu hutumika kutathimini ubora wa huduma za afya nchini.

Sababu zinazohusiana na sababu zinazoongeza hatari

Kiwango kikubwa cha vifo vya akina mama hutokea katika nchi zenye kiwango kikubwa cha vifo vya watoto wachanga, hii huashiria lishe duni na huduma duni za matibabu.
Mtoto anapozaliwa na uzito mdogo huongeza hatari ya mama kupata ugonjwa wa moyo. Kwa hiyo, kadiri uzito wa mtoto unavyokuwa mkubwa wakati wa kuzaliwa ndivyo na hatari ya kupata ugonjwa wa moyo unavyopungua.

Viwango vya vifo vya akina mama katika karne ya 20

Kiwango cha vifo kwa wanawake wanaojifungua kimepungua sana katika karne ya 20.
Mwanzoni mwa karne, viwango vya vifo vya akina mama vilikuwa juu sana. Karibu mwanamke 1 alikufa kwa kila watoto 100 waliozaliwa.
Kupungua kwa vifo vya akina mama ni kwa sababu ya kuboreshwa kwa usafi, upasuaji, kuongezewa maji na damu na huduma bora wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.

Marejeleo

 1. Lisa M. Koonin, M.N., M.P.H. Hani K. Atrash, M.D., M.P.H. Roger W. Rochat, M.D. Jack C. Smith, M.S. Maternal Mortality Surveillance, United States, 1980-1985 MMWR 12/1/1988; 37(SS-5):19-29. [2]
 2. Deneux-Tharaux D, Berg C, Bouvier-Colle MH, Gissler M, Harper M, Nannini A, Alexander S, Wildman K, Breart G, Buekens P. Underreporting of Pregnancy-Related Mortality in the United States and Europe. Obstet Gynecol 2005; 106:684-92.`

Takwimu zilizooneshwa hapa zinaakisi mwaka na wakati chapisho hili lilipochapishwa, zinaweza kubadilika – hakiki

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi